Monday, May 16, 2016

Ili zulia lako lidumu usilifanyie mambo haya matano

 
Zulia sio ngumu kulitunza kama baadhi ya watu wanavyofikiri, ila kama ilivyo kwa kitu kingine chochote linapaswa kutunzwa ili liweze kudumu na kubaki kwenye ubora wake kwa muda mrefu. Kama ndivyo, hivi ni vitu vitano ambavyo hupaswi kuvifanya kwenye zulio hilo.

Usilisugue kwa
brashi likiwa kavu
Inapotokea kitu cha kusababisha doa kimemwagika kwenye zulia kwa bahati mbaya ni ukweli kuwa unahamaki. Kadri unavyoshughulikia doa mapema ndivyo unavyoepusha kulifanya lisikomae. Sasa basi, badala ya kuhamaki na kukimbilia  brashi maji na sabuni, sugua eneo hilo kwa kutumia maji na sabuni au dawa ya kuondoa madoa kwenye mazulia kwa sponji au kitambaa. Zulia limetengenezwa kwa nyuzi zenye manyoya zilizosokotwa pamoja ili kuliongezea uimara. Kwa kusugua manyoya haya kwa brashi inayasababishia kufumuka na kutengeneza udhaifu kwenye hili eneo na bila shaka pataonekana tofauti na kwingine.

Unaweza kujiuliza je inakuwaje tunapopeleka mazulia kusafishwa kwa maji ya msukumo na brashi? Ni kwamba pale ni zulia lote linasafishwa na sio kisehemu kimoja tu, kwahivyo ingawaje mfumuko wa nyuzi unakuwepo lakini kwakuwa ni zulia zima tofauti haionekani. Na pia kumbuka uoshaji huu wa zulia kwa maji mengi unaweza kuwa unafanyika mara moja au mbili tu kwa mwaka laa zaidi ya hapo kuwe na sababu maalum.

Usilisafishe kwa dawa za madukani ambazo sio maalumu kwa zulia
Kuna dawa, sabuni na kemikali nyingi za kusafishia vifaa mbalimbali vya nyumbani kama vile za vyombo, za mbao za vioo, za nguo na za kila kitu (multipurpose) Ni vyema kusafisha zulia kwa kemikali iliyoandikwa kwamba inahusika na kusafisha zulia. Ilishawahi kutokea kemikali ya kusafisha vioo kwa kutokujua ikasafishia zulia na matokeo yake ikatengeneza doa la kudumu kwenye zulia lile.

Usitembee na viatu juu ya zulia
Mazulia mengi ya nyumbani yametengenezwa kwa manyoya laini ili kuleta hisia nzuri kwenye nyayo. Si sawa kutembea juu yake ukiwa umevaa viatu. Kuvua viatu mlangoni kila mara unapoingia ndani ni moja ya njia rahisi na sahihi ya kufanya zulia lako lidumu. Zaidi utaepuka kuingiza uchafu na rangi za viatu kuacha alama kwenye zulia (fikiria soli zinazotoa rangi).

Usiburuze fenicha
Kuburuza fenicha juu ya zulia hasa linapokuwa lile la ukuta kwa ukuta, inaweza kuonekana ni njia rahisi ya kuhamisha fenicha hiyo kutoka eneo moja hadi lingine. Ila pia ni moja ya njia rahisi kabisa kuweka alama kwenye zulia. Nyanyua kitu juu ya zulia kabla ya kukihamisha, kama ni kizito omba msaada wa mtu mwingine.

Usitumie mashine ya upepo kila siku
Kimsingi mashine ya kusafisha zulia inafanya kazi kwa msukumo mkubwa wa upepo ambapo pamoja na kunyonya vumbi na taka ndogondogo zilizo kwenye zulia, vilevile inanyonya nyuzinyuzi dhaifu za zulia. Na ndio maana zulia linalonyonywa kila siku baada ya muda unakuta linakwaruza nyayo badala ya kunesanesa kwa ajili nyuzi zote laini zimenyonywa na mashine.


Makala haya yameandaliwa na Vivi. Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment