Wednesday, May 4, 2016

Mapambo haya matano madogo yanapendezesha nyumba


Nyumba kupendeza ni mkusanyiko wa rangi na vitu mbalimbali vilivyomo ndani mwake. Mapambo haya matano ni kati ya yale madogo kabisa lakini yataleta mguso wa kipekee ndani ya
nyumba yako.

Vesi za maua
Ingawa zinajulikana zaidi kama vesi za maua ila kiukweli vesi zinaweza kupendezesha nyumba kwa njia mbalimbali. Yenyewe tu bila chochote ikiwekwa kwenye shelfu au juu ya meza tayari ni pambo. Vesi inaweza kutumika kwa njia mbalimbali kuendana na mahali ilipo. Inaweza kutumika kama kibebeo cha vitu vingine vigododogo kama vile kalamu endapo ipo kwenye chumba cha ofisi ya nyumbani. Vilevile vesi ya kwenye meza ya chakula inaweza kuhifadhia vitu vidogodogo kama vile kosta na bila kusahau ile ya meza ya kahawa inaweza kubeba rimoti za luninga, chaja za simu, funguo na kadhalika. Kuna vesi zinazowekea mawe ya urembo na pia zipo za kuwekea maua halisi na hata yale yakukaushwa viwandani.

Mimea ya ndani
Hii pia inaweza kuoteshwa kwenye vesi. Siku za karibuni kumekuwa na mimea mingi ambayo haina usumbufu wa kuoteshwa ndani ya nyumba kwani si mikubwa sana na wala haihitaji maji mara kwa mara. Vesi zenye rangi na maumbo ya kuvutia, nyingine zikionekana mithili ya kikombe kikubwa na kisosi chake zimekuwa zikitumika kuoteshea mimea midogo yenye majani manene yaliyotuna inayojulikana kama succulents. Mimea hii imekuwa ikileta mvuto wa kipekee ndani ya nyumba iwe imewekwa juu ya meza, sakafuni au kwenye stendi za maua. Pia mimea hai ndani ya nyumba, kitaalam  imekuwa ina faida ya kusafisha hewa ya ndani kwa kunyonya ile chafu na kuachilia safi.


Mishumaa
Mishumaa ina historia toka enzi za himaya ya Roma.  Mishumaa ya kileo inakuja kwa  rangi na manukato zinazonukia vizuri. Bila shaka ni pambo dogo unalopaswa kuwa nalo ndani ya nyumba.  Pia mishumaa inatumika kuleta mwanga wa kimahaba wakati wa mapumziko nyumbani.

Vioo
Kioo ni pambo lingine dogo ambalo zaidi ya kuleta mvuto kinaweza kikaongeza mwanga na pia hisia za ukubwa wa chumba hasa kinapokuwa kimewekwa kimkakati. Vioo vinaendana na mapambo mengi ya ndani na ni kitu cha lazima bafuni na katika  chumba cha kulala.


Kazi za sanaa
Sanaa ni njia mojawapo sahihi ya kuchangamsha ukuta. Sanaa zimesambaa za aina mbalimbali na unaweza kupata inayoendana na mandhari ya nyumba yako. Ukuta mtupu ukining’inizwa mchoro wa kanvasi unabadilisha kabisa muonekano wa awali.
Pia picha za familia zilizowekwa kwenye fremu zilizosanifiwa vizuri zinatoa utambulisho na kuonyesha historia ya familia hiyo. Na uzuri wa ziada wa kazi za sanaa ni kwamba msanii anaweza kutengeneza mchoro wa sura yako au familia yote endapo utataka akufanyie hivyo.

Simu 0755 200023


No comments:

Post a Comment