Stika
za mapambo ni karatasi nyepesi ambazo zimekatwa katika miundo tofauti ya maua.
Stika hizi zinabandikwa ukutani kwa ajili ya kupendezesha nyumba. Bila shaka
msomaji wangu umeshasikia kuhusu karatasi nyingine za ukutani maarufu kama
wallpaper. Tofauti ya stika na wallpaper ni kwamba stika inawasilisha ua likiwa
limejitegemea/limejitenga, wakati wallpaper ina maua mengi pamoja na hata kama
sio maua yapo maumbo mengine mengi kama ya mawe ya mtoni, vitofali na
kadhalika. Ila kwa upande wa stika hizi za ukutani za mapambo nyingi ni za
muundo wa maua tu.
Ili
stika zijishike vizuri ukutani na kuonekana maridadi unatakiwa uzibandike kwa
usahihi. Kwanza ni lazima ukuta
unaobandikwa stika uwe umeandaliwa sawasawa. Stika za ukutani zinahitaji ukuta
laini, hazijishiki kwenye kuta zilizo rafu au chafu. Kama ukuta uko rafu
unapaswa kumwita fundi aufanyie finishing ikiwa ni pamoja na kuupaka rangi. Hakikisha
rangi unayopaka haifanani na stika ili kufanya ua la stika lichomoze na
kuonekana bila kuumiza macho.
Unatakiwa
kutumia sponji lenye maji na sabuni kusafisha eneo unalotaka kubandika stika
ili kuondoa uchafu wa vumbi, mafuta na mwingine wowote unaoweza kuwepo. Baada
ya kusafisha acha ukuta kwa muda kuruhusu ukauke kabisa.
Kuwa
makini wakati unapobandika stika kwani lengo kuu la stika za ukutani ni kwa
ajili ya kupendezesha ukuta tu. Hii ina maana unapaswa kuangalia lile eneo
unalotaka kubandika, je stika itaonekana na itavutia? Hutataka kuingia gharama
ya kununua stika halafu uibandike mahali ambapo baadaye patawekwa kabati au chochote
ambacho kitaificha.
Kawaida
huhitaji gundi ya nyongeza kubandikia kwani tayari ipo nyuma ya stika.
Nakushauri kwamba kabla hujabandua karatasi ya nyuma inayohifadhi gundi, chukua
tepu za mafundi ujaribu kubandika stika nzima kwanza ili usimame kwa mbali uone
itakavyokuwa baada ya bandiko halisi. Hapo unaweza kurekebisha hadi
kujiridhisha halafu weka alama kwamba ndipo utakapobandika stika yako. Na pia
kuna stika ambazo zina vipande zaidi ya
kimoja. Kwahivyo hii pia itakusaidia kuona ni kwa namna gani vitahusiana katika
muonekano unaotaka mwishoni.
Sasa
unakuwa umefikia wakati wa kubandika kwa uhalisia. Kukwepa uharibifu bandua kwa
hatua ile karatasi ya nyuma inayohifadhi
eneo la gundi. Anza kubandua eneo dogo huku ukiendelea kubandika ukutani eneo
unalobandua. Yaani usibandue yote kwa pamoja kwanza halafu ndio ubandike kwani
gundi zinaweza kushikana pengine kwasababu ya upepo na ukashangaa stika yako
imeharibika usiweze tena kuibandika.
Tumia kiganja cha mkono wako wa pili kukandamiza na
kusambaza stika ili isiache mituno. Ukishamaliza kubandika taratibu bandua karatasi
nyepesi ya juu ambayo watengenezaji wanaiweka ili kukinga mikwaruzo au
uharibifu wowote wa maua ya stika. Ndiposa unafurahia mng’ao wa stika yako na tayari
unakuwa umekamilisha.
Simu 0755 200023. Kununua stika click kwenye VINAVYOUZWA hapo juu. Asante
No comments:
Post a Comment