Monday, May 30, 2016

Hata maua yasiyo hai yanafaa kupendezesha nje ya nyumba

 
Japo wengi wanapendelea kupamba maua yasiyo hai (artificial) ndani ya nyumba, lakini pia maua haya yanapendeza nje ya nyumba. Ili yavutie inakupasa uchague yale ambayo kimuonekano yanakaribiana kabisa na yaliyo hai. Yapo maua yasiyo hai ambayo hadi mtazamaji ayaguse ndipo anaweza kugundua sio hai.

Unaweza kupata maua yasiyo hai  kwa
namna mbalimbali kama vile mti kamili, majani tu, ua na majani machache yani kishina na ua na vilevile ua peke yake.  Eneo la nje unaloweka ua lako linaamua matokeo chanya au hasi.

Mara zote maua haya yanapendeza yakiwa kwenye vyungu vyenye mvuto na si vile vya kawaida vya kuweka udongo kama vya kuoteshea maua yenye uhai. Vyungu hivi ni vizuri na gharama kwani vingi ni vya seramiki. Kwahivyo zingatia kwamba watoto wanaocheza nje hawatavivunja. Kama ni eneo la kuning’iniza kuna vyungu vyenye muonekano kama wa kiota cha ndege, hivi vinapendeza badala ya vile vya plastiki vya kuoteshea maua hai. Vinaweza kupeperushwa kama eneo lina upepo mkali, basi weka mawe ndani kuongeza uzito ili kuhimili upepo.

Uamuzi wa chungu unategemea lengo hasa la kuweka ua fulani eneo fulani. Kama eneo ni karibu sana na mwonaji anakopita, yakupasa uweke chungu kizuri kwani wakati mwingine chungu pekee kinapendezesha bila hata kuwa na ua. Kwa mfano weka kwenye pande mbili za mlango wa mbele.

Mahali pengine pa kuweka maua yasiyo hai nje ya nyumba ni katika eneo la kukaa kwenye bustani. Ning’iniza vyungu vyenye maua yasiyo hai yanayofanana kabisa na hai jamii ya mitambaazi.

Unaweza kuchanganya maua hai na yasiyo hai kwa mfano kutupia maua yasiyo hai kwenye chungu au kitalu cha maua hai na ikaonekana kama vile yale hai ndio yamechanua yale yasiyo hai, hasa pale haya yasiyo hai yanapokuwa ni ya rangi za kuonekana sana kama vile meupe, mekundu au njano. Mchanyiko huu unavutia mno na unamchanganya mtazamaji asiweze kuelewa ni kwa vipi maua yamechanua vizuri hivyo.

Kwa wale wasiopenda usumbufu wa kumwagilia na pengine udongo kuchafua ukuta, simika vyungu vya maua yasiyo hai ukutani. Pia mvuto unapatikana pale unapoyawekea taa za rangi kwa karibu.

Maua yasiyo na uhai yana faida nyingi kama vile unafuu wa bei na uwezekano wa kuyabadili wakati wowote unaotaka. Ni rahisi kuyatunza kwa ajili yanaendana na kila majira hayana cha masika wala kiangazi. Huyamwagilii wala huweki mbolea au kupulizia dawa za kuua wadudu.
Yametengenezwa kwa vitambaa vya hariri na mpira kwahivyo hayapauki.

Yapo ya aina nyingi, unaweza ukapata yoyote unayotaka iwe ni yaliyo kama mimea mitambaazi, ya kusimama yenyewe au yaliyo pamoja kama kichaka.


Nifuate instagram @vivimachange

No comments:

Post a Comment