Wednesday, May 11, 2016

Namna ya kuchagua rangi ya sofa

Iwe unaliita kochi au sofa, rangi ya hiyo fenicha kubwa sebuleni kwako inaweza kuleta matokeo makubwa kwenye muonekano wa chumba hicho. Kama zilivyo fenicha nyingine kubwa unazonunua kwa ajili ya nyumbani, sofa lako mpya unategemea kuishi nalo kwa miaka mingi. Sofa, kitanda na meza ya chakula ni fenicha kubwa tatu nyumbani ambazo zinachukua hela nyingi kuzinunua.

Huenda ni
nyumba mpya imeshakamilika na sasa umeanza kuweka vitu, ni muhimu kuchagua sofa kwanza kwani ni rahisi kupamba  kulizunguka. Baadhi ya wenyenyumba wanapendelea rangi ya sofa kuwa ya jamii moja na ile ya ukuta ili kuleta umoja wa chumba. Hili ni wazo zuri lakini inaweza kuwa changamoto pale utakapotaka kubadili rangi ya ukuta. Uamuzi mzuri ni wa kuachagua rangi ya sofa ambayo itaendana na mapambo mengine yatakayokuwepo sebuleni.

Kwanza kabisa jiulize je unataka sofa ya rangi nzito au nyepesi?
Wengi tunasahau kuzingatia rangi ya sakafu pale tunapochagua rangi ya sofa. Kwa mfano unapochagua sofa ya rangi nzito jiulize je itaendana na zulia la rangi nzito pia utakaloweka sakafuni? Kwa sababu kawaida sofa ni kubwa na limejaa, la rangi ya nzito/giza linaweza kunyonya mwanga na ukashangaa chumba kimekuwa cha giza.

Ujanja wa kufanya unapotaka kujiridhisha na rangi ya sofa ni kununua kipande cha kitambaa chochote cha bei rahisi kinachofanana na cha rangi ya sofa unayohisi itapendeza ili ukifanyie majaribio. Chukua japo kiti ukiweke sebuleni unapotaka kuweka sofa halafu kifunike kwa kitambaa hicho. Ndipo utaona muonekano wa rangi hiyo utakuwaje. Kizuri ni gharama, unaweza kujipatia mita chache za vitambaa vitatu tofauti ndipo ukafanya uamuzi.  Hiyo itakupa picha ya rangi itakavyoonekana hapo sebuleni, kama rangi ya sofa itakuwa nyepesi sana au nzito sana kwa chumba.

Kama unaweka sofa nyeusi kwenye sakafu nyeusi, itafanya chumba kisionekane. Endapo utaweka sofa ya rangi nzito, hakikisha sakafu au zulia lina rangi nyepesi kuzidi ya sofa. Meza ya kahawa yenye rangi nyepesi au ya kioo ndio itafaa kwa sofa hizo nyeusi. Ili kuzisaodia zionekane. 

Sofa ya rangi nyepesi/mwanga ina changamoto tofauti. Kubwa zikiwa ni kuonyesha madoa na uchakavu kirahisi. Kabla ya kuchagua sofa nyeupe au rangi nyingine nyepesi, fahamu namna sebule itakavyotumika kwa hali halisa na sio ya kufikirika. Kama mkakati wako ni kama wa baadhi wanaochukulia kuwa sofa ni kitanda cha sebuleni basi rangi za mwanga/nyepesi hazikufai. Lakini ingawa sofa zako zitatumiwa na watoto, kulalia na kadhalika lakini bado ungependa za rangi za mwangi basi rangi za malighafi za kuosheka kwa kufuta tu kirahisi zitakuvaa. Au pia sofa za kuvalisha kava za kuondoa na kufua nazo zitakuwa sahihi kwako.  

Ukishaamua kuwa unataka sofa ya rangi nzito au nyepesi sasa unakuwa ni wakati wa kufikiria rangi halisi. Baadhi ya watengenezaji, watumiaji na wauzaji wa sofa nilioongea nao wanasema sofa za rangi zisizoegemea upande wowote (neutral) ndio chaguo la wengi. Sofa zenye rangi hizo ni rahisi kupamba chumba na zinaonekana kutokupitwa na wakati hata baada ya miaka kadhaa. 
Sofa za rangi zisizoegemea upande wowote ni pamoja na rangi za krimu, kijivu na ugoro. Sofa za rangi hizi zinaweza kuendana na mapambo yoyote na bado zikawa na mvuto wa kisasa.

Usisahau rangi za mito na mitandio utakayotupia kwenye sofa zako mpya.


 Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment