Tuesday, May 3, 2016

Namna ya kuwa na bustani yenye afya

Faida za kuwa na bustani nyumbani ni nyingi na mojawapo ni kuleta hewa safi katika mazingira unayoishi. Kama sayansi inavyotuambia kuwa mimea inatumia hewa chafu na kuzalisha safi.  Ili kuwa na bustani yenye afya kinachoangaliwa sio ukubwa wa jitihada unazoelekeza kwenye bustani hiyo bali ni namna na wakati sahihi wa kuelekeza jitihada hizo.

Vitu hivi vitano ni muhimu ili
uweze kuwa na bustani yenye afya hapo nyumbani kwako.

Ng’oa magugu
Magugu machache hayakwepeki kwenye bustani yoyote ile, ila usiruhusu yashamiri.  Ng’oa magugu yatoke na mizizi yake aidha kwa kutumia kifaa cha kung’olea au kwa mkono mtupu wakati ardhi ikiwa mbichi na laini. Kama magugu yamekuwa mengi sana kwenye eneo moja, lima eneo hilo na uyaondoe yote pamoja na mizizi yake ndipo uoteshe ukoka au kama ni maua upya. Mbadala wa kulima ni kuyaunguza kwa dawa ya kuua magugu ambapo inazama hadi kwenye mizizi. Zingatia kuwa dawa hizi za kuua magugu zinawezekana pale tu aina ya magugu inapokuwa imetambulika, ndipo unaweza kutumia dawa husika kukwepa kuunguza uoto mwingine unayohitajika  kubaki.

Kata majani wakati muafaka
Bustani yenye afya haikatwi kwa kulazimisha kama baadhi wanavyoweza kudhani kuwa unapokatia chini sana ndivyo unavyoepuka kukata mara kwa mara. Majani unayopaswa kukatwa ni yale mepesi ya juu ambayo ndiyo yameongezeka. Ukanda mnene wa kati na chini unapaswa kubaki vilevile. Pia ni muhimu kufahamu kwamba usikate majani kabla hujaondoa magugu. Hii ni kwasababu ukakishakata majani huwezi kuyatambua tena magugu kirahisi kwani kipindi hiki ukoka wote  unaonekana sawa. Kwahivyo itakupasa kusubiri hadi kipindi kingine. Hii ni mbaya kwakuwa magugu yataendelea kuzaliana na kudhoofisha ukoka sahihi.

Reki majani makavu yote
Baada ya kukata majani kuna makosa yanayofanyika ya kuondoa kwa jujujuu majani yaliyokatwa bila umakini. Hii inasababisha majani hayo makavu kuzama kwenye vishina na mizizi ya bustani hasa pale umwagiliaji au mvua inaponyesha. Mrundikano wa majani makavu kwenye vishina na mizizi ya majani hai unafanya bustani idhoofike. Hii ni kwasababu  majani haya makavu yanazuia hewa kupenya vizuri kwani mimea yote inaihitaji kwa ajili ya kujitengenezea chakula na ubaya zaidi ni kwamba pia yanaozesha yale mazima. Tembelea bustani yako kuona kama kuna maeneo yaliyo na mabaki ya majani makavu. Yareki au yaondoe kwa namna yoyote ile haya kama ni kufagia kwa chelewa. Bustani itaonekana vibaya lakini baada ya majuma mawili itarejea kwenye afya tele.

Jaza uoto maeneo yaliyodhoofika
Kwa kawaida kuna maeneo ya kwenye bustani yanayoweza kuwa ukoka haujajaa vizuri. Ongezea mbegu na yamwagilie kuhakikisha mizizi inakomaa kuwe sawa na kwingine.

Mwagilia na kulisha ukoka
Upe ukoka unyevu wa kutosha hasa kipindi cha joto kali na ukame. Kama tujuavvyo mimea inakuwa usiku ni vyema zaidi kumwagilia nyakati za jioni. Endapo utamwagilia wakati wa jua kali ni kama unapoteza maji yako bure tu. Ilishe bustani yako kwa kuweka mbolea angalao mara mbili hadi tatu kwa mwaka. Wakati wa masika ndio mzuri kwa mbolea ili maji ya mvua yaisaidie izame chini kwenye mizizi. Pia ni vyema kuzingatia muda na kila hatua. Kwa mfano usiweke mbolea bustani ikiwa bado ina magugu na pia usiweke mbolea ndipo ukate majani. Badala yake weka mbolea baada ya kufanya hivi vyote.

 Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment