Vimeza
vya pembeni ni vimeza vidogo vya kando ambavyo vina msaada mkubwa na tofauti tofauti katika chumba chochote.
Kama hukuwa navyo, utakavyokuwa navyo utashangaa ni kwa namna gani uliweza
kuishi bila kuwa navyo.
Vipo
vilivyotengenezwa kwa malighafi mbalimbali lakini kama unahitaji vimeza vya
kando imara ambavyo vinaweza kudumu miaka mingi basi chaguo namba moja ni
vilivyotengenezwa kwa mbao ngumu. Mbali na kuwa imara vimeza vya pembeni vya
mbao vina mvuto na ni rahisi kuvitunza miaka nenda rudi. Pia zaidi ya kutumika,
vimeza hivi ni kwa ajili ya kupendezesha pale vilipo.
Kama
sehemu ya fenicha za kwenye sebule yako, vimeza vya pembeni vina faida zaidi
pale vinapokuwa mwishoni mwa sofa au baada ya kiti, pale ambapo unaweza kukaa
na kuwekea juu yake kinywaji, kitabu au jarida kuwa karibu na wewe na
kukuondolea usumbufu wa kunyanyuka mara kwa mara. Vilevile kwa upande wa
sebuleni unaweza kutumia kimeza cha kando kwa ajili ya kuwekea taa za vivuli
kuipa sebule mvuto au vilevile kutumia kimeza cha kando kuwekea mapambo na
albam za picha za kumbukumbu za familia.
Kwenye
chumba cha kulala wengi wanapendelea kuweka vimeza vya pembeni mwa kitanda ambavyo
vina muonekano sawa na wa kitanda. Vimeza hivi ni murua kwa kuwekea taa za
mezani za pembeni mwa kitanda ambazo zinatumika wakati umejinyoosha huku
ukijisomea kitabu chako ukipendacho kabla hujashikwa na usingizi. Au pia
unaweza kukitumia kuwekea glasi ya maji, kitabu, simu au kifaa kingine
chochote. Baada ya kuperuzi mitandaoni ukiwa kitandani, utahitaji sehemu ya
kuweka laptop yako. Kimeza cha pembeni ndio suluhisho namba moja. Unaweza
kuwekea laptop bila kukuhitaji kunyanyuka toka kitandani.
Watu
wengi wanatumia saa zenye kengele ziwaamshe muda wa kujiandaa kwenda kazini.
Sehemu sahihi ya kuweka saa yako au simu yenye kengele ya kukuamsha ni juu ya
kimeza cha kando kilicho karibu yako. Picha ya kwenye fremu na maua ni vitu ambavyo
pia vinaweza kuwekwa juu ya kimeza cha pembeni mwa kitanda.
Zaidi
ya kuwa inawezekana una seti ya fenicha
iliyokamilika katika chumba cha chakula, kuongeza kimeza cha kando inaweza
kukupa msaada mkubwa. Ni sehemu sahihi ya kuweka chupa zilizo wazi zinazoendelea
kutumika wakati wa chakula, au pia kuweka bakuli la matunda na hata maua au pambo
uliloondoa mezani lipishe wakati wa kula.
Kwenye
chumba cha chakula, kimeza cha kando chenye droo kinaweza kuwa msaada mkubwa wa
kuhifadhia vitambaa vya meza, visu, vijiko na uma.
Licha
ya kuwekwa vyumbani, kimeza cha kando chenye droo kwenye korido ni suluhisho
kwa kuhifadhia bila kusahau kupendezesha. Hakika vimeza vya kando vina faida
nyingi kwenye kila chumba
No comments:
Post a Comment