Sofa mpya ni gharama na kwa bei ya
chini kabisa ya seti nzima si chini ya shilingi milioni moja. Nimehojiana na
wauzaji na wabunifu wa sofa na kuwauliza utaalam wao wa nini mnunuzi azingatie
kabla ya kuanza mchakato wa kununua sofa.
Chukulia utaalam huu kama ni maswali
ambayo unatakiwa kujiuliza wewe unayehitaji sofa mpya.
·
Je linatimiza lengo unalokusudia?
Mara zote fikiria ni kwa jinsi gani
sofa litafanya kazi ndani ya sebule yako. Unatakiwa ukilikalia ujisikie
burudani na
pia ujue linatosha kukalia watu wangapi.
·
Litatosha unapotaka kuliweka?
Ni rahisi kushawishika na muonekano
wa sofa huku ukisahau kama ukubwa na muundo wa fremu yake utaendana na sebule
yako. Ni vyema ukafahamu kuwa chumba cha sebule chenye kuta zilizojikunja kinapendeza
kikiwekwa sofa la muundo wa hivyo na kile chenye muundo wa kuta zilizonyooka za
pembenne nacho kinapendeza kwa sofa la pembenne. Tukizungumzia ukubwa wa chumba
unachotaka kuweka sofa, fikiria pia kuwa ingawa ni maalum zaidi kwa sebuleni,
inaweza kufika wakati ukahitaji kuweka jipya na kuhamishia hilo la zamani
chumbani.
·
Ukilikalia unapata pumziko?
Ni kweli kuwa tumezoea zaidi
kuangalia umaridadi, lakini pia pumziko tunalopata tunapokalia sofa husika ni
muhimu kulifahamu. Kama jinsi miili ya binadamu isivyo sawa ndivyo na sofa
zilivyo. Zipe majaribio ya kuzikalia kabla ya kununua na fikiria ni kwa namna
gani fremu na mito inakufanya ujisikie. Kwa mfano kama unahitaji sofa ambayo
utaweza kupumzika vizuri huku ukiwa unaburudika na vinywaji na vitafunwa
vilivyo kwenye meza ya kahawa, basi hakikisha unanunua ambalo halinesinesi
kiasi cha kukuzamisha chini ukiwa umelikalia yani kubonyea zaidi.
·
Utawezaje kupata ya gharama nafuu?
Usiridhike na kupita kwa wauzaji wachache
na kufanya maamuzi ya kununua! Kuna wajasiriamali wengi wazuri na wabunifu
wanaotengeneza sofa za viwango ambapo unachagua muundo, unatoa oda unatengenezewa.
Kwahivyo unajikuta umepata sofa lenye ubora kwa gharama nafuu. Fanya utafiti
uende kama mnunuzi mwenye uelewa.
·
Je lina ubora?
Unapotaka kununua sofa fikiria vitu
vitatu ambavyo ni malighafi iliyotengenezea fremu, malighafi iliyojazwa ndani
na ile ya juu iliyolifunika. Unatakiwa ununue sofa ambalo fremu yake ni ya mbao
ngumu (au chuma) na sio playwood. Pia hakikisha kuwa malighafi iliyojazwa ndani
ya mito sio ya kusinyaa baada ya muda na kuicha ikiwa flati kama chapati. Kwa
upande wa malighafi iliyofunika sofa jiulize kama unataka ngozi, kitambaa au mchanganyiko
wa ngozi na plastiki. Hii inategemea na gharama unayoweza kumudu na pia tamanio
binafsi. Zingatia kuwa sofa zenye rangi nyepesi zinaonyesha uchafu kwa haraka wakati
zile za rangi nzito hazionyeshi uchafu/doa kirahisi.
No comments:
Post a Comment