Thursday, September 1, 2016

Namna ya kupanga na kupendezesha kabati la vyombo



Bila shaka kabati la vyombo ndio fenicha kubwa zaidi kwenye chumba chako cha chakula ikifuatiwa na meza, kwa maana hiyo linachukua nafasi kubwa zaidi ya muonekano wa chumba hicho.

Kwa kawaida muundo wa kabati la vyombo una sehemu mbili. Ipo sehemu ya juu  yenye
vioo ambapo vyombo vinaonekana vilivyotandazwa. Sehemu ya pili ya kabati ni ile ya chini yenye droo na kabati ambapo vyombo havionekani bila kufungua milango. Kwa sababu fulani baadhi ya watu wanadhania kuwa kabati la vyombo kazi yake ni kuhifadhi vyombio tu. Vizuri, wako sahihi kwa kiasi tu. Eneo kubwa la kuhifadhi vyombo ni lile la chini lenye milango isiyoonyesha kilichomo ndani. 

Eneo la juu lenye milango ya kioo huwa ni kwa ajili ya kuonyesha vyombo kwa kuvitandaza na  mara nyingi eneo hili lina taa ndani. Hapo nyumbani kwako eneo hili la juu la kabati la vyombo  ni kwa ajili ya kutandaza vyombo vyako vya kifahari ulivyonunua kwa gharama kubwa. Sio eneo la kuweka napkin, nyaraka, vitabu vya mapishi vitambaa vya meza au kujaza vyombo kwa wingi.

Unapoamua kupendezesha kabati la vyombo eneo linalokupa fursa hiyo ni lile la juu lenye vioo na ni wakati wa kufikiri tofauti, wakati wa kuonyesha vyombo unavyopenda zaidi. Ni fursa pia ya kuona ni nini uongeze ili kuongeza mvuto. Ni wakati pia wa kuwa unatandaza  vyombo hivyo kuendana na msimu. Haimaanishi kuwa unatakiwa kuwa na seti tofauti ya vyombo vya chakula kwa kila msimu, hapana. Inamaanisha kuwa unaweza kufurahia kutupia vitupio vya mapambo ya msimu husika.

Hatua ya kwanza ya kupendezesha kabati la vyombo ni kuondoa kila kitu na kuanza upya. Baada ya hapo chambua vyombo vizuri ambavyo ungependa vionekane.
Kwa kawaida vikubwa vinakaa nyuma. Kama majagi marefu basi ndizo yaanze kuingia kabatini. Wakati mwingine huenda ikawa ni sahani ndefu ndio zinaingia kwanza. Panga sahani pembeni huku katikati ukiweka vyombo vingine kama majagi, glasi na vikombe vichache vile vyenye mvuto tu. Sahani zinasambazwa vizuri zikiwa kwenye stendi zake.

Baada ya kusambaza vyombo vyako vya kuvutia kwenye eneo la vioo la kabati, kinachofuatia ni kuweka mapambo mengine kama vile vesi ndefu nyembamba katikati ya vyombo hivyo na hata unaweza kuongezea na vitu kama picha za familia ili kuzidi kufanya muonekano kuwa wa kipekee na kukamilisha historia ya kabati.

Mara sehemu ya juu ya vioo ambayo ni maalum kwa maonyesho ikishakamilika ndipo unaweza kuendelea na upangaji wa vyombo vingine ambavyo ndio vingi na visivyokuwa na mvuto wa kutisha kwenye eneo la chini la kabati.

Hakika kwa mpangilio nadhifu kabati linavutia mno.

No comments:

Post a Comment