Tunapotaka kupendezesha nyumba zetu,
tunajikuta tuna vingi vya kuzingatia. Tunakuwa makini kwenye kuchagua rangi na
michoro iliyopo kwenye kuta, fenicha na sakafuni. Lakini ni mara chache
tunapeleka umakini huohuo kwenye taa na jinsi mwanga wa taa unavyoweza kubadili
muonekano wa namna chumba kinavyoonekana. Kutokana na hilo ni
vyema kufahamu
kuwa suala la taa za ndai ya nyumba si jepesi kivile.
Unatakiwa kujiuliza maswali kadhaa kama
vile ni taa zipi unazohitaji kwenye chumba kipi kwani kila chumba kina mahitaji
yake. Na je ni za wati ngapi, ni za kuning’inia, ni za ukutani au ni za
kupachikwa kuzamishwa kwenye dari? Taa mbili za mezani au moja ya sakafuni?
Maswali ni mengi ila usiwe na shaka kwani kwenye makala hii tunaangalia makundi
matatu ya taa kwa matumizi tofauti ambayo ni kundi la taa za lazima, taa za
kuelekeza na taa za kupendezesha.
Tukianza
na taa za lazima ni zile taa ambazo ni za msingi
kwamba utakapoingia kwenye chumba cha giza lazima uiwashe hiyo kwanza. Kiasi
cha mwanga kinachozalishwa na taa hizi lazima kiwe cha kutosha kwa ajili ya
kuweza kumulika kila sehemu vizuri chumbani. Kwa mfano taa mbili za mezani
haziangukii kwenye kundi hili lakini taa inayoning’inia darini imo kwenye taa za
lazima katika chumba hichohicho. Hapo unaweza kuona tofauti kati ya kazi za taa
hizi za aina mbili.
Fungu la pili la taa ni zile taa za
kuelekeza kwenye maeneo maalum kusaidia kuongeza mwanga wakati wa shughuli kama
vile ya kusoma, kufanya kazi kwenye kompyuta au wakati wa kula. Lengo la taa
hizi ni kupeleka mwanga wa moja kwa moja pale unapohitajika badala ya
kuusambaza kila mahali. Taa za namna hii ni kama zile za vivuli za kuweka
kwenye vimeza vya kando au kusimamisha sakafuni.
Kundi la tatu la taa ni zile
zilizowekwa kwa lengo la kupamba/urembo. Kwa mfano taa za rangi kwenye kabati
ulilosambaza sanaa za mapambo. Au pia zile za kwenye kabati la vyombo la kioo
zenye lengo la kuweka msisitizo kwenye vyombo vyako zako za kifahari.
Katika makundi haya matatu ya taa,
ili kupata lengo ulilokusudia unapaswa kuchagua balbu sahihi kwa kukupa kiasi
na aina ya mwanga unaotaka. Fundi umeme John Mangowi anajutuza kuwa kwa kundi
la kwanza la taa ambazo ni za lazima, endapo ni chumba cha kawaida cha nyumbani
unahitaji baibu ya wati 40 hadi 60.
Kwa taa za kuelekeza na za urembo ni
muhimu kutokuwa na mwanga mkali sana. Ambapo unahitaji za bailbu za wati kati
ya 10 na 25.
Mwisho ni vyema kufahamu kuwa mwanga
wa taa na kupendezesha ndani ya nyumba kwa taa, jambo kubwa la kuzingatia ni
muundo, ukubwa na kiasi cha mwanga wa taa husika. Inawezekana umeipenda sana
taa ya kuning’inia darini ya umbo fulani, lakini kama nyumba haina dari ndefu
taa ya hivyo haikufai.
No comments:
Post a Comment