Dari
naweza kuliita ni ukuta wa tano wa chumba lakini, mara nyingi haipati rangi
nyingine zaidi ya nyeupe. Kwa muda mrefu toka nyumba za kisasa ziwepo, nyeupe
imechukuliwa sio tu kama rangi salama bali pia sahihi kwa ajili ya dari. Kuna
wakati kweli nyeupe inaweza kuwa ndio chaguo muhimu na pekee, lakini kama hujawahi
kufikiria rangi nyingine mbali na
nyeupe huenda ukawa unapoteza wigo mpana wa
kupendezesha na kuongeza manjonjo ya chumba.
Ifuatayo
ni mikakati na njia zitakazokuwezesha jinsi ya kuchagua rangi ya dari.
Tukianza
na mkakati wa rangi nyeupe ambao ni kawaida kwenye dari nyingi kwani wengi
wanaamini kuwa ina faida kwamba hutakuwa na haja ya kuibadili mara kwa mara. Kwamba wanaweza kubadili rangi ukutani lakini dari
ikabakia na nyeupe yake ile ile. Rangi nyeupe darini inakifanye chumba king’ae
na pia hisia ya kuwa kuta ni ndefu.
Mara nyingi rangi nyeupe ndio chaguo sahihi la dari
kwani inafanya hamu ya kutazama juu isiwepo na kuelekeza mvuto kwenye kuta,
fenicha na samani.
Kwenye
vyumba ambavyo vinapokea mwanga wa jua kidogo, dari nyeupe inasaidia kuupokea
na kuusambaza maeneo mengine ya chumba.
Namna nyingine ya kuchagua rangi ya
dari ni kuipaka rangi sawa na ya kuta. Njia hii inakifanya chumba kiwe na hisia
ya kuwa na utajiri wa rangi na pia ukamilifu.
Vilevile unaweza kupaka dari rangi
ambayo inapishana kidogo na ya kuta. Ni namna ambayo rangi za kuta na dari zinakuwa
za jamii moja lakini rangi ya kimojawapo ikawa inaelekea kwenye upande wa nzito
zaidi au nyepesi zaidi. Nyepesi ya bluu na njano ya siagi ni rangi
zinazopendeza darini. Bluu inakupa hisia ya anga.
Namna hii ya kuchagua rangi ya
kupaka dari inakupa pia ile hisia kwamba bado uko chumba kilekile.
Namna nyingine ya kuchagua rangi ya
dari ni kwa kupaka rangi nzito kwenye dari kuliko ya kwenye kuta na rangi hizi
mbili ziwe ni kutoka jamii tofauti kabisa. Mpishano wa rangi hizi mbili una
kawaida ya kutengeneza muonekano wa kuvutia. Ni vyema kufahamu kuwa rangi nzito
darini inatengeneza hisia ya kwamba kuta ni fupi na pia hisia ya mahaba zaidi. Kwahivyo
ni sahihi kwa chumba chenye kuta ndefu hasa kikiwa ni kile cha kulala au cha bafuni.
Na kumbuka kuwa endapo kuta zote za bafu zimefunikwa kwa marumaru, darini ndio
mahala pekee pa kujidai kwa kupaka rangi. Kuwa makini usijepata rangi nzito
darini kama kuta za chumba ni fupi kwani na itatengeneza hisia kwamba chumba
hicho kinataka kukufukia!
No comments:
Post a Comment