Tuesday, February 10, 2015

Kutokana na ajali za nyumba kuungua moto Jeshi la Zimamoto linakushauri unapojenga nyumba weka milango na madirisha ya dharura


Mwananchi linaripoti kuwa:
Siku tatu baada ya ajali ya moto kutokea  katika eneo la Kipunguni A jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu sita na nyumba kuteketeatu, Jeshi la Zimamoto limejitetea kuwa lilishindwa kufika haraka kwenye tukio kwa sababu ya ubovu wa mawasiliano kati yao na wananchi.
Katika tukio hilo, Emmanuel Mpira ambaye ni mtoto katika familia hiyo ndiye aliyenusurika kwani alikuwa matembezini ambapo aliporudi alikuta moto umeshaanza kuwaka na baadhi ya vitu vilishaanza kuteketea.

Inspekta wa Jeshi la Zimamoto, Puyo Nzalayaimis ameeleza kuwa wananchi wasiwalaumu kwa sababu taarifa zilichelewa kufika ofisini kwao na kuongeza kuwa mawasiliano yalikuwa mabovu.
Amesema alipokuwa anatoka kuelekea eneo la tukio walipotea njia na kuelekea hadi Kituo cha Polisi cha Sitaki Shari na badae wasamaria wema waliwaelekeza hadi eneo la tukio.
“Katika nyumba hiyo hakikuwezwa kuokolewa hata kitu kimoja kwasababu vitu vyote vilishaanza kushika moto na zima moto walipofika eneo la tukio waliweza kumalizia kuuzima na kutoa miili ya marehemu na kukabidhi kwa Jeshi la Polisi,”amesema Nzalayaimisi

Ameongezea kwa sasa jeshi hilo linakabiliwa na changamoto nyingi  ikiwemo uhaba wa  magari  , mawasiliano mabovu na kutojua mitaa mingi ya jijini Dar es Salaam.

Aliwashauri wananchi kutoa taarifa kamili na watu wanapojenga nyumba wahakikishe wanakuwa na milango na madirisha  ya dharula.

No comments:

Post a Comment