Sunday, February 22, 2015

SHAMIM MWASHA: Mmiliki wa 8020 asiyepigia hesabu mali za mume

 “Kila kunapokucha naumiza kichwa nifanye nini ili niweze kutengeneza pesa zitakazoniwezesha kuendesha maisha yangu licha ya kuwa nimeolewa na kumkuta mume wangu tayari ana uwezo,” ndivyo anavyosema Shamim Mwasha, mmiliki wa blogu maarufu ya 8020fashions.

“Pamoja ya kuwa nimeolewa na mtu ambaye uwezo wa kiuchumi sio mbaya lakini hata siku moja sijawahi kupigia hesabu mali zake ndiyo maana naendelea kujishughulisha.”

Shamim ameweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kufungua na kuendesha blogu katika kipindi cha miaka tisa iliyopita hali iliyomuwezesha kujijengea umaarufu mkubwa.

Anakiri kuwa wengi wamemfahamu kupitia blogu hiyo, lakini harakati zake za kujikwamua kama mwanamke zilianza muda mrefu mara tu baada ya kuhitimu mafunzo yake ya uandishi wa habari na kujiunga na Kampuni ya IPP.

“Nikiwa IPP ndipo ikaanzishwa tovuti ya darhotwire.com na kwa bahati nikapata kazi kama mhariri wa habari.”
Shamim wenye watoto watatu anaeleza kuwa huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kujishughulisha na masuala ya mtandao.

Anasema wazo la kuanzisha 8020 alilipata baada ya kufungua duka la nguo alipoona kuna umuhimu wa kufungua blogu ili kumuwezesha kutangaza bidhaa zake.
Anasema kuwa katika kipindi chote ameweza kuendesha maisha yake kwa kutegemea blogu hiyo ambayo ina idadi kubwa ya watembeleaji na kupata matangazo mengi ya biashara yanayomuingizia kipato.

Anaeleza kuwa licha ya wengi kumuona maarufu, anaishi maisha tofauti na wanavyofikiria akiwa nje ya kazi yake. “Napata wakati mgumu kuona wananichukulia mimi kama malaika, yaani wananiweka kwenye kundi la mastaa tena mastaa wa Ulaya… Hapana sijafika huko mimi wa kawaida sana kuna wakati najuta hata kwanini nilijitambulisha kama Shamim, bora watu wangeijua 8020 kuliko ilivyo sasa. Naangaliwa kama mtu wa tabaka jingine, kitu ambacho siyo sahihi.”


Shamim anakiri kuwapo kwa migogoro na hali ya kutokuelewana kwa baadhi wanawake wanaomiliki blogu hapa nchini na kueleza kuwa hilo linasababishwa kwa kiasi kikubwa na chuki miongoni mwao na kutafuta attention. Anasema wengi wanajikuta wakiingia kwenye migogoro kutokana na kukosa fikra mtambuka na kushindwa kuwavutia wasomaji hali inayofanya kutafuta namna nyingine isiyo rasmi.

No comments:

Post a Comment