Thursday, February 26, 2015

Polisi Arusha wakodishwa kuvunja mikono ya mdaiwa wa sh 250,000/

Mkazi wa Loksale, Samweli Shani (47), akiwa amefungwa POP baada ya kuvunjwa mikono yake na polisi, kushoto ni ndugu yake Gabriel Shani akionyesha picha za X-ray alizopigwa zikionyesha jinsi mikono ilivyovunika.

Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas, amekiri kupokea malalamiko ya mkazi mmoja wa Loksale wilaya ya Monduli, Samwel Petro Shani (47) ya kuvunjwa mikono yake miwili kutokana na kipigo cha askari Polisi wa kituo cha Leskale.

Hata hivyo amesema kwamba kwa sasa yupo likizo ila aliwasiliana na mkuu wa kituo cha polisi Monduli (OCD) ili kupata undani wa tukio hilo.

Imedaiwa kuwa kipigo hicho kimesababishwa na mfanyabiashara mmoja ambaye alikodisha askari ili kumfunza adabu kwa kushindwa kulipa fedha zake anazomdai zipatazo 250,000.

Hata hivyo mfanyabiashara huyo ambaye alijitambulisha kwa jina la ,Shamimu alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi alikana kukodisha askari wa kumpiga na kumvunja mkono mlalamikaji .

Alisema yeye kama mwananchi alienda kulalamika kituo cha polisi kuhusu deni lake kwamba kilichotokea huko baada ya yeye kuondoka  hafahamu.

Kwa mujibu wa maelezo ya mlalamikaji Samweli, askari hao hawakutaka kumkamata bali kuitoa roho yake kwani walikuwa wakitumia chuma kinene kumpiga na kumvunja mikono yake miwili huku mwingine alikuwa akimshambulia kwa rungu na mateke.

Alieleza kuwa tukio hilo lilitokea Februali 6,mwaka huu majira ya saa 3 usiku na kwamba aliwatambua askari wawili waliomtesa kwa kipigo kuwa ni Steven na Justini wote ni askari wa kituo hicho cha Loksale.

”Mnamo tarehe 6 mwezi huu majira ya saa 3 usiku,walikuja askari wawili wakiwa wamevaa nguo za kiraia ,walinikuta nimekaa kwenye ukuta nikiwa na kijana mmoja,walinikamata na kunifunga pingu wakiwa wamenikandamizia chini ,walinipiga sana na kunivunja mikono yangu miwili”alisema Samweli

Akisimulia chanzo cha tukio  hilo alisema, mfanyabishara Bi. Shamimu alienda katika kituo hicho cha polisi na kuwaeleza askari hao kuwa alikuwa akimdai shilingi 250,000 na kwamba sikuwa nimemlipa deni hilo.

”Ni kweli Shamimu alikuwa akinidai shilingi 250,000 ila nilishamlipa shilingi laki moja na kubaki sh,150,000 ,hizo hela kuna msichana nilimdhamini alikuwa mfanyakazi wa duka lake aliyedai alimwibia,ndipo mimi kwa kuwa nilikuwa na mahusiano na msichana huyo nilikubali kulilipa deni hilo”alisema Samweli

Alisema askari hao walimvamia na kumkaba kabari kisha askari mmoja alimfunga pingu na kuanza kumshambulia kwa kumpiga na rungu na chuma na walipoona wamepoteza fahamu baada ya kumvunja mikono walimkokota hadi kituo cha polisi na kuendelea kumpiga sehemu zingine za mwili ikiwemo miguuni.

”Baadae usiku wakiwa wamenifungia lokapu alikuja mkuu wa kituo na kuniangalia ,alikuta hali yangu ni mbaya na kuondoka bila kusema lolote”alisema.

Hata hivyo askari hao waliingiwa na woga kutokana na hali yake na kuamua kumchukua usiku huo wa manane na kumpeleka katika kituo cha afya kwa ajili ya matibabu.

Alieleza kuwa kesho yake askari hao walimchukua na kumpeleka kituo cha polisi wilaya ya Monduli na kumweka lokapu.

Aliongeza kuwa mkuu wa upelelezi wa wilaya OC CID,aliyemtaja kwa jina moja la Bw. Abichi alimfuata akiwa lokapu na kumwambia kuwa anataka ampatie dhamana ila alitakiwa akubaliane na masharti ya dhamana .

”OC CID aliniambia kuwa nataka nikupatie dhamana ila kwenye maelezo yako unatakiwa ueleze kuwa ulikuwa unatoroka ulinzi halali wa polisi ukiwa na pingu ,na wakati ukikimbia ulianguka na pingu zikakuvunja mikono yako ”alisema bw Shani.

Aliongeza kuwa hakukubaliana na kauli hiyo ndipo OC CID alipoamua kumrudisha lokapu ,ambapo alikaa kwa muda wa siku nne wakimbembeleza akubaliane na maelezo ya polisi .

Alisema kuwa aliamua kuwa na msimamo huo,hadi tarehe 12 walipoamua kumfikisha mahakama ya wilaya ambapo alisomewa shitaka , la kuvunja na kuiba na kujaribu kutoroka polisi akiwa na pingu, suala ambalo ni uongo uliolenga kupoteza haki yake ya kulalamikia jeshi hilo.

Imeandaliwa na Woinde Shiza wa libeneke la kaskazini blog

No comments:

Post a Comment