WASICHANA 22 walioingizwa nchini na
mmiliki wa Continental Night Club na Hunters Club, Omprakash Singh kwa ajili ya
kufanya biashara ya ukahaba wanarudishwa leo Nepal na India walikotoka.
Akizungumza jana na Mtanzania kwa
njia ya simu, Kamishna wa Uhamiaji Udhibiti na Usimamizi wa Mipaka, Abdallah Abdullah, alisema wasichana hao wanatarajia kuondoka leo baada ya
kumaliza matibabu waliyokuwa wakipata.
“Wasichana waliokuwa wanaugua TB na
UTI wote wamepona, tiketi zilichelewa kidogo lakini zimepatikana wanasafiri
kesho (leo),”alisema.
Alisema Singh ameshalipa faini ya Sh
milioni 15 alizoamuliwa kulipa na mahakama, pamoja na kulipa mishahara ya
wasichana hao Dola za Marekani 30,625.
Tangu wasichana hao walipobainika
walikokuwa wamefichwa, Idara ya Uhamiaji imekuwa ikiwasimamia kwa kuwapa
matibabu na kufanikisha safari ya kurudi nchini mwao.
Hata hivyo idara hiyo ilifanya
mawasiliano na mashirika ya kimataifa kuona jinsi watakavyowasaidia wasichana
hao mara watakapofika huko.
Hivi karibuni Singh alitiwa hatiani
na Serikali kutaifisha magari yake matatu baada ya kupatikana na hatia ya
kuwaingiza nchini wasichana hao kutoka India na Nepal kwa ajili ya kuwafanyisha
kazi ngumu ikiwamo biashara ya ngono.
Singh alitiwa hatiani katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka baada ya
kukiri kosa lililokuwa linamkabili la kuwaingiza nchini wasichana hao, ambapo
aliwatumikisha kazi ngumu na alikuwa akiwauza kwa ngono na kujipatia fedha.
Mahakama ilimpa adhabu ya kulipa
faini kila kosa Sh milioni tano hivyo kwa makosa matatu alitakiwa kulipa Sh
milioni 15 na magari yake matatu yalitaifishwa na Serikali.
Pia mahakama ilimtaka kuwalipa
wasichana hao 22 mishahara yao na endapo mshtakiwa angeshindwa kulipa faini
angekwenda jela miaka 10.
Mshtakiwa alikuwa akiishi
Mwananyamala, alikuwa Mkurugenzi wa Dhamaka Entertainment Center Limited,
kampuni ambayo aliisajili Tanzania.
Inadaiwa alikuwa Tanzania mwaka 2010 kwa nia ya kuanzisha dancing club. Mwaka
2011 alifungua Night Club Kinondoni, TX Market inayoitwa Hunters Club.
Wakili wa Serikali Prosper
Mwangamila alidai baada ya miezi michache alifungua club nyingine maeneo ya
clock tower, barabara ya Nkrumah inayoitwa Continental Night Club na zote mbili
ziko chini ya Kampuni ya Dhamaka na ziliajiri madansa kutoka India na Nepal.
Mwangamila alidai madansa hao
walisafirishwa na mshtakiwa kutoka kwao kuingia nchini, aliwakatia viza, kibali
cha kufanya kazi nchini, mahali pa kulala, chakula na mahitaji mengine.
Ilidaiwa kuwa kati ya Mei na Desemba
mwaka jana mshtakiwa alipokea madansa 21 kutoka Nepal na dansa mmoja kutoka
India, walipofika mshtakiwa alichukua hati zao za kusafiria, simu zao na
kuwalazimisha kujiingiza kufanya ngono kisha yeye akusanye fedha huku
akiwafanya hao wasichana ni sehemu ya biashara yake.
Idara ya Uhamiaji ilipata taarifa za
mshtakiwa, Desemba 19 mwaka jana walikwenda alikokuwa akiishi nyumba namba 531,
Block 9 inayomilikiwa na Thuraya Mohammed Abdullah na kuwakuta wasichana hao
22.
Maofisa wa uhamiaji walifanya
upekuzi katika chumba cha mshtakiwa na kukuta hati za kusafiria 22 na simu 27
ambazo ni za wasichana hao.
‘’Uchunguzi ulibaini kwamba
mshtakiwa alikubaliana na wasichana hao kuwalipa kila mwezi ujira kati ya Dola
za Marekani 500 mpaka 1000 lakini aliwalazimisha kusaini mkataba wa ujira
unaoonesha kwamba atawalipa kila mwezi Dola za Marekani 200 mpaka 500,”anadai
Mwangamila.
Alidai uchunguzi ulibaini kwamba
wakati tofauti mshtakiwa alikuwa akiwatoa wsichana hao kutoka nyumba waliyokuwa
wakiishi Mwananyamala na kuwapeleka Hunters na Continental na mahali kwingine
kwa nia ya kuwafanyisha kazi kwa nguvu na ngono.
Mshtakiwa katika safari hizo alikuwa
akitumia gari lenye namba za usajili T540 CBN aina ya RAV4, namba T111CCS
Toyota Vox Noah na Toyota Hiace namba T111CRZ.
No comments:
Post a Comment