Thursday, February 12, 2015

MAKALA: Jinsi ya kupamba sebule ndogo


Sehemu zote ndogo zina changamoto ya kupamba, lakini kwakuwa sebuleni ndio mahali unapokaa kwa uhuru na mgeni wako kupamba iliyo ndogo ni sanaa unayopaswa kufahamu. Makala ya leo itakujuza ni kwa namna gani unavyoweza kuelezea na kuonyesha hisia zako za mapambo hata kama eneo ni dogo.

Ni kwa namna gani unaweza kuifanya sebule ndogo maridadi na wakati huohuo ukipata eneo la kutosha kukaa na kupita? Ni samani za aina gani unazopaswa kuchagua, na ni wapi utaziweka? Leo utaongezea ujuzi wako wa kufahamu jinsi utakavyoweza kupamba sebule ndogo na kuifaidi kila eneo. Kwamba haijalishi ni eneo kubwa kiasi gani tulilonalo kwenye nyumba  tunazoishi, kama tukiamua – tunaweza kuwa na sebule ya kuvutia. Tuanze hivi:

Kwa sebule ndogo na hasa kama ina madirisha madogo pia inaweza ikaleta hisia kama mkaaji yuko ndani ya boksi. Tengeneza sehemu ya kuelekeza macho na ongeza mwanga kwa kuweka  vioo na karatasi za ukutani. Kama utaweza kukiweka kioo kikatazamana na dirisha kitaakisi mwanga na kufanya kama kuna dirisha la ziada hivyo kuleta muonekano wa eneo kuwa kubwa.

Weka fenicha za umbo dogo, kwenye maduka ya vitu vya kiutamaduni/vitu vya sanaa unaweza kupata sofa na viti vya umbo dogo vitakavyofaa kwenye sebule yako ndogo na pia fenicha zilizotengenezewa sehemu za kuhifadhia zitafaa zaidi kuwezesha maeneo ya kuhifadhi kwa wingi kwa ajili sebule ni ndogo. Kwa mfano meza ya kahawa yenye eneo la kuhifadhia kwa chini itafaa kuliko iliyo wazi kote.

Ndio, chumba chako cha sebule ni kidogo lakini inawezekana ukuta wa dari ni mrefu, tumia fursa ya nafasi hiyo! Ingawa nafasi ya ukuta haitakuwezesha kuongeza sofa lingine ila unaweza kutumia faida ya nafasi ya huo ukuta kwa kuweka sanaa zako za ukutani.

Weka fenicha kwenye kona ambayo kujaza eneo lote la kona. Kwanini? Kwasababu fenicha kubwa itaifanya kona ionekane kubwa. Na kama utaamua kwenda hatua zaidi unaweza kutengenezesha sofa moja tu la kuendana na hiyo kona halafu lile eneo lililobaki ukaweka kiti cha mtu mmoja mmoja. Pia punguza wingi wa sofa, kuna seti za sofa zeenge sehemu tatu za kukalai na zile zenye sehemu mbili.

Kuendana na nafasi ya sebule yako unaweza weka ile sofa yenye sehemu mbili za kukalia badala ya ile yenye tatu.

Kuna sofa ambazo hazina eneo la mgongo, endapo utaweka sofa ya hivi karibia na ukuta huo ndio utakuwa unachukua nafasi ya mgongo wa sofa. Na hata kama sofa hii isiyo na mgongo utaiweka kati (endapo sofa ni ndogo sana ili isimalize eneo) utakuwa unaitumia sebule kila upande, ambapo itakuwa ni matumizi mazuri ya nafasi. Inakuwa kama kigawe kati ya hizo sehemu mbili za kukaa.

Huwezi amini unaweza kudhani mimea ya kijani sebuleni itapunguza eneo lakini kiuhalisia ni kwamba wanasaikolojia wanasema mmea wa kijani unapumbaza macho na kuona eneo ni kubwa. Ukiwa umewekwa kwenye kona unazipinguza makali na hivyo kutoonekana mwisho wa chumba. Kama huamini jaribu utaamini.

Kwenye sebule ambayo ni ndogo kabisa, haitawezekana kuwa na maeneo mengi ya kukaa kama ambavyo ungependa. Njia moja ya kutatua hili ni kuhifadhi viti  hasa kama ni vile vya kujikunja unaweza hifadhi mvunguni, vinapohitajika vitatolewa. Kumbuka kuwa kwa sebule ndogo uwezekano wa nyumba nzima kuwa ndogo nao ni mkubwa kwahivyo kuwa makini hata wakati wa manunuzi ukiwa unajua kuwa nyumba yako ni ndogo.

Kama vipi achana na sofa. Nani kasema ni lazima sebule iwe na sofa? Kama nafasi inabana badala yake  weka viti vyenye mikono vitatu ama vinne kuzunguka meza ya kahawa, na wakati huohuo meza ya kahawa ikiwa na eneo la kuhifadhia.

Hizo ni dondoo nilizoweza kukukusanyia jinsi ya kupamba sebule ndogo. Kama nilivyosema kabla, haijalishi ukubwa au udogo wa sebule yako, cha muhimu ni kuwa unaweza kukarimu wageni wako na hivyo kuweza kuonyesha ubunifu ulioko ndani yako wewe kama mtu unayeishi hapo mahali!

Niambie: Ningependa kuona picha ya sebule yako ndogo maridadi na nadhifu, tafadhali nishirikishe picha.

Makala hii imeandaliwa na Vivi ambaye ana mapenzi makubwa ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni ama maswali tembelea www.vivimachange.blogspot.com
.


2 comments: