Thursday, December 12, 2013

My article for newspaper: Uzio Sahihi



Jinsi ya kuchagua uzio sahihi wa nyumba yako kwa bajeti yako

Uzio ni moja ya sura au tuseme kipengele cha makazi ambacho kinaweza kuwa kwa ajili ya kazi na pia kwa ajili ya urembo kwa jinsi ambavyo unataka kiwe. Kutegemea na bajeti yako, ubunifu, hitaji la ulinzi na pia ladha yako binafsi kuna aina nyingi za uzio kwa ajili yako kuchagua. Hapa ni baadhi ya dondoo zangu ninazoamini zitakuwezesha kupata uzio utakaokufaa.
Kwa ujumla walau kila nyumba inawezekana kuzungushiwa uzio, iwe ni kwa ajili ya ulinzi, usalama, faragha au muonekano. Uzio ulio imara unaongeza pia thamani ya mali yako hiyo.
Ili mpango wako wa kuweka uzio ufanikiwe na bila kujutia hela yako jiulize mambo yafuatayo kabla ya kuweka uzio wako:

Jambo la kwanza kabisa jiulize ni nini nia yako ya kuweka huo uzio. Je unataka kujiweka mbali na macho ya majirani wapelelezi? Kuzuia mbwa wako wasitoroke unapowafungulia? Au ni kwa ajili tu ya kuongeza urembo wa makazi yako? Kwa hivyo kabla hujaamua kuchagua mtindo au vifaa vya kutengenezea uzio wako hakikisha umejua kuwa lengo lako la kuweka uzio ni nini. Hapana shaka kuwa wewe msomaji wangu umeshawahi na bado unaona uzio zilizowekwa zikaacha maeneo ya wazi ambayo baadaye wenyeji wameamua kuyaziba ama kwa makuti au kwa bati.

Jambo la pili la kufikiria ni utunzaji wa uzio wako. Aina ya uzio utakayochagua itasema ni gharama kiasi gani ya utunzaji wake uko tayari kuitumia. Kwa mfano uzio wa mbao unatakiwa kupakwa rangi mara kwa mara na pia mbao zinaoza baada ya wakati kwa hivyo zinahitaji maboresho ya muda mfupi mfupi. Wakati huo huo uzio za wavu (chain-link) hauna gharama kubwa kwenye utunzaji kwani nguzo zake ni za zege na zile chuma hazipati kutu lakini huenda usikupe faragha sahihi. Orodheha gharama ya vifaa mbali mbali na linganisha bajeti yako na hitaji lako ili kupata uzio sahihi.

Jambo la tatu la kuzingatia kabla ya kuweka uzion ni muundo au mtindo wa uzio wenyewe. Kwa kuwa imeonekana watu wengi wanaendeleza sehemu za nje ya nyumba zao kwa shunguli nyingi za maisha ya kila siku kwa (mfano makala iliyopita tulizungumzia watu kuwa na eneo la kukaa kwenye bustani), muonekano wa uzio umekuwa ni jambo la kuzingatia kuliko ilivyowahi kuwa. Lango kuu na taa nazo zinaboresha muonekano huu. Na kwa kupunguza gharama labla au hata kupata hewa safi unaweza ukaweka uzio wa aina fulani eneo la mbele  na aina nyingine eneo la nyuma. Kwa mfano, nimeona baadhi ya watu walioweka uzio wa gharama kubwa eneo la mbele ya nyumba na upande wa uani wakaweka uzio wa chain-link  ikishirikiana na miti ya uzio aina ya michongoma. Hii itategemea ni kwa jinsi gani uzio wako wa eneo hilo utakavyoweza kukubaliana na lengo na bajeti yako.

 Jambo la nne ni kuhusu faragha na ulinzi. Jua ni nini uzio wako utaruhusu uweze kuacha nje ya nyumba na ni  nini lazima kiingizwe ndani. Uzio unaoacha nafasi nafasi au matundu matundu hauna faragha na wala hauwezi kukulinda vya kutosha, ila unakupa starehe ya kuangalia kinachoendelea nje ya makazi yako unapokuwa umejipumzisha bustanini.

Baada ya kuweka akili sawa kwa hayo mambo manne ya kuzingatia, anza kufanya utafiti wako wa aina za uzio zilizopo. Kwa mazingira yetu ya Kitanzania zipo uzio za aina mbali mbali kama vile tofali, mbao, miti, makuti, chuma, aluminiam, wavu, bati, PVC na kadhalika. Karibia kila aina ya uzio ina faida na hasara zake linapokuja swala la bei, utunzaji, umaridadi na lengo lake. Fikia ni uzio upi ungependa kuweka na tembelea masoko si chini ya matatu ili ulinganishe gharama kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.

Sasa umeshafanya utafiti wako wote na uko tayari kuanza kujengea uzio wako. Jambo la mwisho lakini sio dogo ni juu ya ujirani mwema. Kabla hujaweka uzio wako cheki na majirani kuhakikisha kuwa uzio unaoamua kuweka hautaleta usumbufu kwao. Kwa mfano, uzio wa miti itayooteshwa karibia kabisa na nyumba ya jirani huenda ikaleta mgogoro. Na pia kuna uzio ule ambao vibati vinawekwa juu tuseme uzio ni wa ukuta na una marembo yake, wenye nyumba wengine wanapendelea kuweka vibati vya plastiki kwa juu ili ukuta usiloe ukaoza. Maji ya mvua kwenye hivi vibati kama yameelekezwa kumwagika kwa jirani inaweza ikaleta kero. Jua mipaka yako kwa kukumbuka kuwa uzio usiloleta kero kwa jirani unafanya ujirani mwema, kuwa jirani mzuri kwa kuweka uzio ambao hautamkera jirani yako.

Zaidi ya yote fahamu sheria za mipango miji juu ya kujenga uzio. Kwa mfano uzio wa tofali wa urefu fulani hauruhusiwi kwenye makazi.

Sio siri kuwa kuchagua uzio kwa ajili ya nyumba yako inaweza kuwa uzoefu mgumu. Kuwa na dongoo hizi kichwani, pamoja na bajeti yako na kipaumbele cha staili itakuhakikisha kuchagua uzio sahihi kwa ajili ya nyumba na familia yako.
 
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment