Wakati wa sikukuu za mwisho wa mwaka uko karibu sana na kama
wengi wetu walivyozoea ni wakati wa familia kukaa pamoja kwa ukaribu zaidi kwa
kipindi walau kisichozidi wiki mbili. Kwa mfano baba mama na watoto hukutana
pamoja na familia za watoto wao wakubwa ambapo huwa ni pamoja na wajukuu na
kama Mungu amewaweka wazazi hawa huenda na vitukuu wakawepo. Pia ndugu jamaa na
marafiki hutembelea na kusheherekea sikukuu pamoja. Sasa basi kwa vile
wanafamilia ndani ya nyumba wanakuwa wengi inabidi kuwa na maandalizi ya mahali
pa kulia chakula. Na mahali hapo ni kwenye chumba cha chakula. Kwa maana hiyo wakati
huu chumba cha kulia chakula inabidi kiwe tayari kwa ajili ya familia na wageni
watakaotembelea kukaa pamoja.
Chumba cha chakula ni mahali ambapo patatumika
kwa mlo wakati huo wote wa sikukuu.
Kwa kawaida mara nyingi milo ya kila siku familia huwa sio
rasmi, isipokuwa wakati wa milo ya sikukuu maalum. Hata hivyo milo na wageni
inaweza kukurusha roho wewe mwenye nyumba. Kwa maana hiyo maandalizi ni
hayakwepeki kipindi hiki.
Kwa kuwa chumba cha kulia chakula kilicho rasmi kinaweza
kisiwe burudani kwa milo ya kawaida, watu wengi wanapamba chumba hiki kwa kuwa
na muonekano rasmi pale tu wanapokuwa na eneo la pili la kulia chakula. Lakini
kama una chumba kimoja cha kulia chakula ambacho unategemea kwa ajili ya milo
yote miwili yaani ile rasmi na isiyo rasmi bado unaweza kufurahia dunia zote
hizi mbili.
Kwanza kabisa tuangalie muonekano halisi wa chumba cha
kulala. Meza na viti vya kulia chakula ndio utambulisho rasmi wa chumba cha
chakula. Meza hii yaweza kuwa ya umbo la duara, yai au pembe nne. Meza za umbo
la yai na duara huwa sio rasmi sana kama zile za pembe nne. Najua msomaji ya
kuwa unaona shughuli zote rasmi huwa meza zinazowekwa ni za pembe nne. Meza za
duara na yai zinampa kila mtu uhuru sawa, na zinawezesha mazungumzo kirahisi
kwa kila mmoja mezani wakati zile za pembe nne
ni rasmi zaidi na huwa zinawaweka wakaaji katika ngazi tofauti tofauti,
kama vile eneo la mwenyeji au mgeni
rasmi na kadhalika. Andaa meza ya chakula ya ukubwa ambao utatosha
wageni wako.
Kitamaduni, viti vya mikono vinatumika kwenye miisho ya meza
za pembe nne. Viti visivyokuwa na mikono vinaruhusu upenyaji wa kirahisi. Andaa
meza yako vyema kwa kuwa na kitambaa cha meza na kama kitambaa hicho kikiwa na
rangi za msimu itakuwa bora zaidi. Tukumbuke kuwa rangi za msimu huu wa sikukuu
ni nyekundu, nyeupe na kijani. Vesi ndogo ya maua hata kama ni kutoka kwenye
bustani yako itaongeza mvuto. Kila wakati wa mlo hakikisha kuwa mezani kuna napkin
hasa zile za kipambaa – zinatumika muda wote wa tukio kwa kufuta alama za
vyakula, glasi baridi, matone na mengine mengi. Hizi za kitambaa ni nzuri zaidi
kuliko zile za karatasi na hata ni rafiki zaidi kwa mazingira.
Andaa kuta na sakafu za chumba hiki kwa ajili ya ujio wa
familia kubwa. Paka kuta zake rangi za kuvutia zitakazoongeza hamu ya kula
chakula na kutengeneza sehemu ya kukaa na kuongea. Zulia sakafuni ni upendeleo
wa mtu binafsi, wengine huona kuweka zulia chuni ya meza ya chakula ni
changamoto hasa kama kuna watu wadogo ambao wanaweza kuwa wanadondosha vyakula
wakati wa mlo. Hata hivyo kuna aina nyingi za mazulia ambazo ni rahisi
kusafishika kwa dawa zilizopo na hivyo kufanya kazi ya usafishaji iwe rahisi na
zulia kuonekana jipya kila wakati.
Chanzo cha mwanga kwenye chumba cha kulia chakula huwa ni
ile taa maalum ya kwenye chumba cha chakula. Hata hivyo taa hii sio lazima iwe
chanzo kikuu kama sio ya kuweza kurekebisha kiasi cha mwanga kwani wakati
umekaa na wageni wako waweza kuhitaji kupunguza ukali wa mwanga. Kwa hiyo kama
kuna taa nyingine za mwanga hafifu basi zitumie wakati huo ili kupunguza msongo
wa mwanga mkali kwenye macho na pia kujenga mandhari yenye mvuto.
Fremu za picha za ukutani
sio muhimu chumba cha kulia chakula. Zile rangi maridadi za kuta zinatengeneza
mvuto wa kutosha kwenye nyumba hasa kwa kuwa kitovu kitakuwa ni wageni walioko
mezani.
Mwisho kabisa weka mazingira ya burudani wakati wa milo. Watu
wanataka burudani kwa hivyo hawatapendelea kukaa muda wote kwenye viti vya meza
ya chakala hasa pale kwenye tumazungumzo twa hapa na pale. Wanafamilia wengine
wanaweza kukaa kwenye sofa ila hii haimaanishi kutofuata utaratibu wa wakati wa
mlo pamoja. Mfanye kila mmoja wa wanafamilia wako afurahie kulia sikukuu ya
kipindi hiki nyumbani kwako kwa kuweka mazingira ya starehe wakati wa mlo kwa
jinsi itakupendeza wewe mwenyeji wao.
Makala hii imeandaliwa
na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na
mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni
au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment