Wakazi wakiri kula kinyesi bila kujua wilayani Karagwe
Karagwe. Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha
Kafunjo, Kata ya Kiruruma, wilayani Karagwe, mkoani Kagera, wamesema
wamekuwa wanakula kinyesi bila kujua kutokana na kutokuwa na vyoo bora.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara kijijini hapo mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya kutembelewa na Ofisa wa Afya kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu Wilaya ya Karagwe, kuwaelimisha jinsi ya ujenzi wa vyoo bora na matumizi yake.
Mmoja wa wakazi hao, Renatus Kanyabuhura alisema kutokana na kutokuwa na vyoo bora, walikuwa wakila kinyesi kwa sababu walikuwa wakitoka chooni bila kunawa mikono na kuvuta sigara huku wengine kula matunda.
“Kutokana na kutokuwa na vyoo bora, unakuta nzi
wanaotoka chooni wanatua kwenye chakula na huku mlaji anaendelea, jambo
linalojionyesha tunakula kinyesi,” alisema Kanyabuhura.
Naye Ofisa wa Afya, Moses Aligawesa alisema magonjwa mengi yanatokana na matumizi mabaya ya vyoo na kula kinyesi kwa njia tofauti.
Aligawesa alitaja magonjwa yanayotokana na kula kinyesi kuwa ni, kipindupindu, kuhara, kichocho, safura (minyoo) na kwamba, magonjwa hayo yanaathiri kila mmoja kuanzia familia, kijiji, kata hadi taifa. Alisema choo bora ni shimo lenye urefu wa futi 12 na kuendelea, kinachosafishika, kuezekwa bila kusahau kunawa mikono kwa kutumia maji na sabuni.
No comments:
Post a Comment