Thursday, February 20, 2014

My article for newspaper: Kabla hujanunua microwave

Mambo unayotakiwa kufahamu kabla ya kununua microwave

Wanasema, “kama huwezi kuhimili joto, kaa mbali na jiko.” Microwave inakataa usemi huu wa zamani kwa kuweka joto mbali ukilinganisha na jiko lako la gesi, umeme, mkaa, kuni ama jiko lolote lile lingine. Teknolojia imefanya microwave isiwe tu kifaa cha kupashia chakula, bali kuiwezesha kumudu mahitaji ya mapishi mbalimbali. Kifaa hiki kinaweza kutumika kuchoma, kuoka, kuchemsha, kupasha, kuyeyusha na hivyo kufungua ulimwengu mpya kabisa wa mapishi rahisi kwako. Swali kuu:

Ni mambo gani unayotakiwa kufahamu kabla ya kunua microwave?
Hununui tanuri ya microwave kila mara kama unavyonunua vifaa vingine vya jikoni. Kabla hujaenda dukani kuna baadhi ya mambo ya kuzingatia. Ni vizuri kufikiria mambo haya kwanza na kulinganisha huduma zinazoweza kutolewa na microwave husika kwa hivyo kuwa na uamuzi wa busara.

Kununua microwave ni rahisi mno kwa ajili sokoni kuna wigo mpana wa  microwave zisizo za gharama kubwa. Unatakiwa ujue mahitaji yako kabla ya kuamua kuwa microwave fulani itakufaa. Zipo modeli zinazoweza kupika na kupasha kwa pamoja na zipo za kupasha peke yake. Fahamu ni chakula gani utakachoweza na usichoweza kupika kwa microwave. Microwave zina vipengele vinavyoelekeza haya yote. Hapa ni mambo ya kuzingatia kabla hujanunua.

Kama huitumii sana, uwezekano mkubwa ni kuwa unaitumia kwa kuyeyusha, kupasha au labda kuchoma bisi. Kwa maana hiyo huhitaji yenye vipengele vingi kwa hiyo usinunue ya namna hiyo!
Kama unapenda kupika na unathubutu kujaribu mapishi mbalimbali mapya kila siku, nunua microwave ya kisasa zaidi yenye vipengele vingi kuendana na mahitaji yako.

Je kuoka ni pendeleo lako na unapenda kuchoma sandwich, vitafunwa mbalimbali na pia kuoka keki? Micowave ambayo inaweza kufanya yote haya ni wazo zuri jikoni kwako.
Kama watoto wako wadogo pia watatumia microwave unayotaka kununua basi vipengele vya urahisi wa matumizi na usalama ni muhimu zaidi.

Je, matumizi ya nishati ya microwave unayotaka kununua yakoje? Wati kubwa zitapika chakula haraka ziadi. “Microwave nyingi zinahitaji nishati ambayo inaangukia kati ya wati 600 hadi 1500,” anasema Ali Maftaha ambaye ni meneja mauzo wa duka la vifaa vya jikoni. Vyakula vilivyobainishwa kuwa vinafaa kupikiwa kwenye microwave husika vinatumia nishati ya angalau wati 800 ili viweze kuiva sawasawa.

Ni wapi unapoenda kuweka microwave yako? Modeli za kuweka juu ya kaunta za jikoni ni maarufu zaidi – unachomeka tu kwenye umeme na kuanza kutumia. Microwave za kujengea zinahitajika kusimikwa kwa utaalamu, na kwa ujumla zina nguvu zaidi  na vipengele vingi zaidi. Kwa hivyo kuwa na ukakika ni wapi utaweka microwave yako kabla ya kuinunua. Kwa mfano hizi za kuweka juu ya kauta panahitjika nafasi ili kuifikia kirahisi kurahisisha matumizi.

Utashangazwa na vipengele ambavyo microwave inavyo. Kipo kipengele cha vyakula vya kupika kutokana na microwave kusoma hisia ya kiwango cha moto kitakachohitajika kwenye tanuri kutokana na mvuke unaozalishwa na chakula kinachopikwa. Vyakula vya kupika kwa programu vinaanza kupikwa kwa mguso mmoja tu: unaingiza chakula, unakiambia kifaa ni nini unapika, na kinaanza kupika. Microwave nyingi zina sehemu zilizosetiwa automatiki kwa kupika vyakula kama bisi na supu. Zinachagua zenyewe kiasi cha moto na muda utakaotumika.

Kuna kipengele cha kuyeyusha. Kwa mfano nyama imeganda na huna muda wa kuisubiri iyeyuke yenyewe. Microwave zote zina kipengele hiki, anasema Maftaha. Kipengele hiki nacho ni bora ukachagua microwave yenye kile cha automatiki ambapo utahitajika kuyeyusha kwa kubonyeza tu aina na uzito wa chakula. Microwave yenyewe ndio inachagua kiwango cha moto na muda utakaotumika kuyeyusha.

Kipengele kingine cha muhimu sana cha kuangalia kwenye microwave unayotaka kununua ni loki ya watoto. Hasa kama una watoto wa umri wa kutoweza kuitumia. Loki ya umeme (kama vile kubonyeza kitufe fulani) kitasaidia kuwazui wasiharibu kwa kuwasha tanuri kwa bahati mbaya.

Nunua microwave kwa kuzingatia ukubwa wa familia yako. Kwa jinsi familia ilivyo kubwa ndivyo microwave inatakiwa iwe kubwa. Kwa mfano hakikisha bakuli unalotumia litatosha kwenye tanuri ya microwave unayotaka kununua.

Mwisho kwenye mambo haya ya kuzigatia usisahau urahisi wa kusafisha microwave yako. Modeli za microwave ambazo zimetengenezwa kwa jinsi ambayo ndani hakunasi vyakula ni rahisi kusafisha.

Baadhi ya watu wanaogopa kutumia microwave kwa ajili wanaamini kuwa zinabadilisha kemikali ya asili ya chakula au zinasababisha uvimbe kutokana na mionzi.. Hata hivyo jambo hili limekataliwa na watafiti wengi. Mionzi inaweza kupenya pale tu mlango wa microwave unapokuwa umepasuka au haufungi vizuri, anasema mkemia Enos Kwai. Hata kama  ni kwa sababu hiyo, kuvuja kwa mionzi kunakuwa ni kidogo mno kuweza kusababisha tatizo lolote la kiafya.

Akili bora kabisa zinanolewa jikoni Miili bora kabisa ya mazoezi inalishwa hapa pia. Ni hii sehemu ambayo harufu nzuri zaidi ndani ya nyumba zinakotoka. Kutoka kwa bibi yako hadi kwa mama yako, ladha ya chakula kilichoandaliwa nyumbani sio cha mtu yeyote kusahau utamu wake. Unatamani hata kupika chakula hicho kwa mapishi mbali mabli lakini huna muda wa kutosha mikononi mwako. Jitwalie microwave ya vipengle mbalimbali viwe ni kupasha, kupika, kuoka, kuyeyusha na kuchoma leo ili ikurahisishie mambo.


Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange.  Vivi ni mjasiriamali  upande wa usafi wa nguo, mazulia na magari; pia ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment