Sunday, February 9, 2014

News Zihusuzo Makazi/Nyumba: Wakazi waomba ulinzi


WAKAZI wa kijiji cha Kidago katika Halmashauri ya wilaya ya Morogoro
ambao walivunjiwa makazi yao kwa kile kinachodaiwa kuvamia shamba la
mwekezaji Martin Shem, wameiomba serikali na vyombo vya usalama mkoani
Morogoro kuwawekea ulinzi.
Wamesema hali hiyo inatokana na kupokea vitisho kutoka kwa mwekezaji
huyo, hali inayowafanya waishi kwa wasiwasi. Januari 10 mwaka huu kaya
45 zenye wakazi 180 katika kijiji hicho walivunjiwa makazi yao kwa amri
ya Mahakama kwa madai ya kuvamia shamba la mwekezaji huyo.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara mara baada ya kutembelewa na
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, wakazi wa hao wamemuomba
kamishna wa ardhi nchini kushughulikia kwa haraka mgogoro uliopo katika
shamba namba nne ili iweze kujulikana nani mwenye haki ya umiliki.
Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Morogoro aliwataka wakazi wa kijiji
hicho kutokuwa na wasiwasi na kuwataka waishi kwa amani kwani jambo hilo
serikali inalishughulikia.
Aidha aliwataka wakazi hao kuendelea na shughuli za kilimo katika
shamba hilo wakati Serikali ikiendelea na utaratibu wa kuirudisha ardhi
hiyo mikononi mwa wananchi hao.
Awali katika kikao cha wadau wa ardhi pamoja na makamishna wa ardhi
kilichofanyika mkoani hapa, Naibu Waziri wa Ardhi, George Simbachawene
alishangazwa na kitendo cha mwekezaji huyo kuvunja makazi ya wananchi
hao na hivyo kuziagiza mamlaka husika kushughulikia suala hilo ili
kuondoa mgogoro uliopo.
Mgogoro wa shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 1,080 ulianza tangu mwaka 1999 ambapo hadi sasa haujapatiwa ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment