Mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kununa jiko
Umeamua
kuwa kwenye vifaa vyako vya jikoni vya
zamani vinaondoka vipya vinaingia. Au labda unaanza mwanzo kabisa kwa kuwa ni
jiko ama nyumba mpya. Kwa sababu yoyote ile ya uamuzi wako wa kununua jiko
jipya makala hii itakufahamisha mambo muhimu ya kuzingatia kabla hujaingiza
mikono yako mfukoni kutoa hiyo hela yako uliyopata kwa jasho.
Kwanza tuwekane sawa kuwa kwa lengo
la makala hii, jiko litamaanisha kifaa kizima kinachotoa moto kwa ajili ya
kupikia chakula. Jiko hili litakuwa na pande mbili ambapo upande wa kwanza wa
jiko ni pale panapobandikwa sufuria na tutapaita stovu na wa pili ni pale pa
kuokea na tutapaita tanuri. Kwa maana hiyo jiko linakuwa ni kifaa chote cha
kutoa moto wa kupikia na sio chumba kizima cha jiko. Kwa ufafanuzi huo sasa
tunaweza kuendelea.
Kununua jiko jipya ni uamuzi muhimu.
Jiko jipya (au lililotumika) linaweza kuwa bei kubwa, na litaleta mabadiliko
kwenye shughuli zako za mapishi na linagusa pia mapambo ya nyumba yako. Kuna
mambo kadhaa ya kuzingatia wakati wa kuchagua jiko ambayo ni pamoja na ukubwa,
nishati itakayotumika, umaridadi na bajeti. Baada ya kujichunguza, kutafakari
na kulinganisha majiko yaliyopo sokoni, unaweza kuchagua jiko sahihi kwa ajili
ya chumba chako cha jiko.
“Mambo ya kuzingatia kabla ya kununua jiko jipya
mara nyingi yanategemea na kama unanunua jiko kwa mara ya kwanza au hapana,” anasema
Nassoro Ali, muuzaji msaidizi wa duka la vifaa vya nyumbani. “Kama ulishanunua
jiko kabla, kwa kawaida walau utakuwa na mawazo ya ziada juu ya ni kitu gani
hasa unatafuta,” anasema. Ali anasema kuwa watu wanaonunua majiko yao ya kwanza
“hasa kwa uchumi huu,” wanaamua tu
kukimbilia modeli za bei rahisi zilizopo.
Ali anasema kuwa kwanza unatakiwe ujue kuwa utaweza kumudu chanzo kipi cha nishati kwa ajili ya jiko lako, je ni gesi au umeme. Baadhi ya wanunuzi wanamudu vyote. Hata hivyo, Ali ameongelea modeli mpya za majiko zilizopo ambazo zina stovu za gesi juu na tanuri ya umeme chini. “Wanunuzi wangu wengi wanapenda kupikia stovu za juu za gesi na kuwa na matokeo mazuri zaidi ya kuoka kwenye tanuri ya umeme. Modeli hii yenye kutumia nishati za aina mbili inakupa kilicho bora kwa dunia zote mbili,” anasema.
Kama
unanunua jiko kwa mara ya kwanza, kitu cha muhimu zaidi kuzingatia ni ukubwa
ili lifiti vizuri jikoni kwako. Ali anasema kuwa ukubwa wa kawaida zaidi kwa
jiko la nyumbani ni upana wa inchi 30, ila kuna modeli nyingine ndogo hadi
upana na inchi 26 na kubwa hadi upana wa inchi 48. Kama unaondoa jiko la zamani
ili uweke jipya, ni vizuri zaidi kununua jiko la ukubwa uleule ili kuepuka
gharama za marekebisho mapya ya kaunta na kabati zilizo jirani na jiko. Kama ni
jiko jipya basi unaweza kununua jiko la ukubwa wowote kuendana na ukubwa wa
chumba na ladha binafsi. Hakikisha fundi anayekujengea chumba chako cha jiko
anakupa vipimo sahihi kabla ya kununua jiko jipya.
Kitu kinachofuata cha kuzingatia, anasema Ali, ni mtindo wako wa mapishi. Je unataka jiko lenye zile stovu tu kama huvutiwi na kuoka? Je unataka jiko lako liwe la stovu mbili, nne au tano? Idadi ya stovu itategemea na ni watu wangapi mara kwa mara unawapikia, vyakula unavyopendelea kupika na kama unafurahia kuoka vyakula.
Vyakula vingi vya mapishi ya kukaanga na kuchemsha vinafaa zaidi kupikiwa kwenye stovu ya gesi kwa kuwa ni rahisi kudhibiti kiasi cha moto. Pia ule muonekano wa moto unaleta hisia halisi ya mapishi na pia visahani vya stovu havichukui muda kupoa. Wataalamu wanasema tanuri la umeme kwa ajili ya kuoka linafaa zaidi kwa kuwa umeme unaleta joto lenye uwiano. Ila hala hala zile koili zinashika moto kwa muda mrefu hata baada ya kuzimwa kwa hivyo umakini mkubwa unahitajika!
Amua kama
unahitaji jiko la kujengea ndani kwa ndani ama la kusimama peke yake. Stovu na
tanuri la kujengea humo humo ni mtindo unaowezesha kuhifadhi nafasi na pia ni
muonekano wa kisasa zaidi, ila linaweza kuwa gharama kusimika, kutengeneza ama
kurudishia. Majiko ya kusimama peke yake ni bei rahisi zaidi na yanapatikana
kwa wingi. Maamuzi yako juu ya kipendele hiki hayatategemea tu bajeti na
muonekano bali pia usanidi wa chumba cha jiko lako. Ijulikane pia kuwa haya ya
kusimama peke yake yanaweza kujengewa ila ukarabati wake unahitaji matengenezo
makubwa.
Zingatia
umaridadi wa jiko lako. Majiko yanakuja kwa rangi mbali mbali kama nyeupe,
nyeusi, silva ya kutoshika kutu na rangi nyingine nyingi. Fikiria rangi za
chumba chako cha jiko na vifaa vyako vingine hapo jikoni labla ya kuamua ununue
jiko la rangi gani.
Baada ya
hayo yote sasa ni wakati wa kuanza kupiga misele kwenye maduka ya wauzaji wa majiko
ya nyumbani. Kuna makampuni lukuki ya nje yanayotengeneza majiko, fanya utafiti
wa jiko, lifungue uone mlango wa tanuri unafungukaje. Angalia koili na shelfu zikoje.
Muulize muuzaji maswali, omba vipeperushi na majarida yanayooneysha jiko
litakavyoonekana baada ya kusimikwa nyumbani kwako. Kama una dishi la kuokea
ama kikaangio ukipendacho sana nenda nacho unajaribu kitaaje kwenye jiko
unalotaka kununua.
Ukiweza kufanikisha haya yote naamini utapata jiko la ladha na mfumo wako wa maisha. Mpishi anafurahia kufanya kazi yake kwenye jiko linalokidhi viwango.
No comments:
Post a Comment