Moja
kati ya manunuzi muhimu zaidi ambayo utafanya ukiwa mahali unapoishi ni
kitanda. Kitanda chako ndio mahali unapopata usingizi unaouhitaji sana ili
mwili wako uweze kuchaji kwa ajili ya pilika za siku inayofuata. Kuhakikisha
kuwa unapata faida zote za usingizi unatakiwa kuwa na kitanda sahihi ambacho
kitapumzisha mwili wako vizuri.
Na hii ndio sababu unatakiwa kuwa na godoro la
uhakika pamoja na fremu ya kitanda imara kukidhi matakwa ya mwili wako. Mbali
na usingizi mnono unaopata kutokana na kitanda sahii, vilevile kitanda hicho
kinaleta mvuto kwenye chumba cha kulala.
Kwa
maana hiyo fremu ya kitanda ni jambo muhimu la kuchunguza kabla ya kufanya
uamuzi wa kununua. Kazi kubwa ya fremu hii ni kubeba godoro na kufanya kitanda
kiwe tayari kwa kutumika. Fremu ya kitanda inaweza kutengenezwa kwa malighafi
zozote lakini malighafi mbili kubwa ni mbao na chuma. Wakati wa kuchagua fremu
hii ya kitanda vigezo vikubwa huwa ni ladha binafsi ya mnunuzi, bajeti na uimara
unaohitaji.
Katika
kuandaa makala hii nimefanya mahojiano na Bi Janet Moshi ambaye ni mjasiriamali
anayetengeneza fenicha za chuma na ameeleza kwa kina faida na changamoto za
kitanda cha chuma.
Anaeleza
dondoo zifuatazo kuhusiana na faida za
kitanda cha chuma. Dondoo hizi zitakusaidia wakati wa kufanya uamuzi wa
manunuzi ya fremu ya kitanda.
Uimara-
Kama unataka kununua kitanda ambacho kitadumu muda mrefu na kinahimili uchakavu
basi nunua cha chuma. Kitanda cha chuma hakiharibiki kirahisi na hata pale
vinapokuwa ni viwili pamoja vya kubebana juu na chini hukuti vikilegea na
kuchezacheza. Utunzaji unaotakiwa sanasana ni mmoja tu nao ni kupaka rangi
baada ya kipindi. Kutokana na uimara wake, bila
shaka hutakaa ujutie kuwekeza kwenye kitanda cha chuma.
Wepesi-
Kitanda cha chumba ni chepesi ukilinganisha na kitanda cha mbao ngumu kwa maana
ya mkongo na mninga. Hii inarahisisha usogezaji wa pasipo kufungua sukuruu pale
unapotaka kukihamisha toka eneo moja la chumba kwenda lingine ndani ya chumba
hicho chicho.
Gharama-
Faida kuu muhimu ya kitanda cha chuma ni kuwa bei yake iko chini, kwa mfano
wakati kitanda cha chuma cha futi sita kwa sita ki nauzwa shilingi laki sita,
kile cha ukubwa huohuo cha mninga au mkongo kinauzwa shilingi milioni 2. Baadhi ya watu wanadhania vitanda vya chuma ni ghali
kutokana na urembo wake, lakini kumbe sio. Fremu ya kitanda inapokuwa ya
gharama nafuu inakuwezesha kuwekeza hela zaidi kwa ajili ya kununua gogodo
imara zaidi.
Matumizi-
Uraisi wa kukibomoa pale ambapo unakihamisha toka eneo moja hadi lingine. Kitanda cha chuma kimeunganishwa kwa sukuruu na nati na
ndio maana ni rahisi kukifungua na kukibeba vipandevipande.
Upatikanaji- Unaweza kupata kitanda cha chuma cha ukubwa wowote na
chenye vizuizi vya kuzuia godoro lisikimbie angalau kila mahali penye mafundi
vyuma. Na hata kama unatafuta cha mtoto unapata na kwa rangi unayohitaji.
Muonekano- Kitanda cha chuma kina muonekano rahisi kabisa hadi ule
ambao una mapambo mengi mno. Vitanda vya chuma vinaambatana na mionekano mingi
maridadi na ya kipekee. Na kwa maana hiyo chumba kizima cha kulala kinaonekana
kuwa na mvuto kutokana na urembo wa kitanda. Pia ni rahisi kubadili mapambo ya
kitanda cha chuma pale unatakapohitaji kufanya hivyo.
Mvungu-
Kwa kawaida kitanda cha chuma kimeenda juu kuliko cha boksi cha mbao. Na hii inawezesha urahisi wa kufanya usafi eneo la chini ya
kitanda. Zaidi ya hilo, eneo chini ya kitanda cha chuma linaweza kutumika
kuhifadhi baadhi ya vitu na hivyo kukuongezea mahali pa kuhifadhia hapo
chumbani.
Changamoto za kitanda cha chuma ni
hizi zifuatazo:
Endapo ile mipira kwenye miguu ya
kitanda cha chuma itasagika na kutokurudishiwa mipya basi kuna uwezekano wa
miguu ya kitanda kuharibu sakafu pale kinaposogezwa kwa kuburuzwa.
Chuma kina kawaida ya kubadilika
kuendana na hali ya joto au baridi. Endapo chumbani kuna baridi basi tegemea
chuma za kitanda nazo kuwa na baridi. Vilevile kwa upande wa joto.
Kitanda cha chuma kinaweza kisiwafae
watu wa mabondeni ambao nyumba zao zinasimamisha maji sakafuni. Endapo nyakati
za mvua sakafu ya chumba chenye kitanda cha chuma inasimamisha maji kwa siku
mbili au tatu na kuendelea basi kuna uwezekano mkubwa wa miguu ya kitanda cha
chumba kuharibiwa na kutu.
Msomaji wangu hizo ni faida na
changamoto za kitanda cha chuma. Nina uhakika kuwa utafanya uamuzi sahihi pale
utakapoamua kufanya manunuzi. Tukutane makala ijayo!
Je, unauza
bidhaa au huduma inayohusu nyumba na bustani ambayo unataka Watanzania waijue?
Nijulishe simu/whatsapp 0755200023
No comments:
Post a Comment