Mara
baada ya sikukuu za mwisho wa mwaka kuanza kumalizika na mapambo yake kuanza
kuondolewa ni wakati wa kuweka mikakati ya namna ya kuishi mahali pasafi kwa
mwaka huu mpya.
Na sio jambo la kushangaza kuwa wengi wanaweka mikakati ya
mwaka mpya kwahivyo bila shaka moja ya hiyo ni kuhusu mahali unapoishi. Hii ni mikakati ya kukuwezesha kusafisha na kutunza mazingira ya nyumbani kwa mwaka
2016. Jitahidi ufanikiwe katika hili.
1. Tenga
fungu kwa ajili ya usafi na matunzo ya nyumba. Bila shaka maisha ni magumu na wengi wanafikiria mbinu
mbalimbali za kubana matumizi, na hili halina ubishi hata kwa nyumbani. Pamoja
na hayo ni vyema tukumbuke kuwa mazingira safi kwa ubora wa afya zetu ni
kipaumbele namba moja. Unaweza kutumia njia mbalimbali za kuwa katika mazingira
mazuri ya nyumbani kwa kubana matumizi, na mojawapo ni kufanya mambo kadha wa
kadha bila kumuita fundi au nguvukazi ambayo itaongeza gharama. Kwa mfano,
wanafamilia wanaweza kushiriki kutunza bustani na maua bila kuhusisha mtunza
bustani wa nje.
Pia unaweza kuweka majani ya kuhifadhi unvevu kwenye bustani
yako ya maua na kukufanya uwe na matumizi kidogo ya kumwagilia. Kwa upande wa
kusafisha kama vile vyombo, kutumia maji ya uvuguvugu kutapunguza matumizi
makubwa ya sabuni kwahivyo unakuwa umeshabana matumizi. Tumia sabuni za
kusafishia ambazo zina matumizi zaidi ya moja na tunza vizuri vifaa vya usafi.
2. Jifunze
kusafisha haraka zaidi. Ni watu wachache dunia hii ambao wanapenda kutumia muda
mwingi kusafisha nyumba zao. Kwa wengi wetu ambao tuna majukumu mengi ambayo ni
lazima tuyakamilishe kwa siku, kujifunza kusafisha haraka haraka ni mkakati
mzuri. Ili ufanikiwe katika kusafisha kwa haraka hakikisha unahifadhi vifaa
vyako vya usafi eneo moja. Haifai unataka kudeki huku unaanza kutafuta dekio na
kukasirika hulioni kiasi kwamba hata ari ya usafi inaondoka. Pia anza na eneo
ambalo sio chafu sana na usipoteze muda kusafisha sehemu ambayo sio chafu. Kwa mfano
umesafisha jokofu wiki iliyopita basi wiki hii usihangaike kusafisha tena.
Kuepuka kurudia rudia safisha kuanzia juu kushuka chini.
3. Epuka
mrundikano. Nyumba iliyovurugwa inahitaji kitu zaidi ya usafi. Kuwa na mkakati
wa kupunguza vitu ndani ya nyumba yako ili kuepuka mrundikano. Kuondoa mrundikano ni njia kuu ya
kukufanya uweze kusafisha kwa haraka bila kupoteza muda. Nyumba isiyokuwa na
mrundikano ni rahisi kusafisha kuliko ya kinyume chake.
4. Kuwa
na mpangilio. Mara mrundikano unapoondioka, hatua nyingine kubwa inayofuata ni
kupanga vizuri vitu vilivyobakia. Mara kila kitu kinapokuwa na makao yake ndani
ya nyumba yako mrundikano unakuwa sio hoja tena na kusafisha kunarahisishwa.
5. Andaa
ratiba ya kusafisha. Kila dakika kuna kitu cha kusafisha, lakini huwezi
kusafisha kila dakika. Kuwa na ratiba ya usafi kunawezesha urahisi wa kusafisha
kwa siku, kwa juma na kwa mwezi. Ratiba ya kusafisha ina faida ya kuu kuwa
hupotezi muda wako kusafisha vitu ambavyo haviko kwenye ratiba ya kusafisha
siku hiyo.
6. Hamasika
zaidi kusafisha. Kuna wakati hamasa ndio kitu kinakosekana kwenye utunzaji wa
nyumba zetu. Sio rahisi kila wakati kuhamasika kusafisha, lakini kuna vitu
rahisi ambavyo vinaweza kukuhamasisha. Hamasa ya kusafisha inafanya usafi uende
haraka. Tafuta hamasa inayokufanya usafishe, labda unataka upige picha baada ya
kusafisha au unataka uache nyumba safi au unapenda ugeni wa mara kwa mara, au
ni kujaribu sabuni mpya ya kusafishia au ni kupanga upya chumbani na kadhalika.
7. Shirikisha
wana familia wote kwenye kusafisha. Kugawa majukumu ya kusafisha hata kwa wale
wanafamilia wadogo kabisa ni mkakati mzuri wa kufanya mazingira ya nyumbani
yawe masafi. Mtu anaposafisha anaelewa ugumu wake kwahivyo hata kuchafua
anapata ukakasi. Na kwa wale wanaoweza kusafisha vizuri wanasaidia zoezi zima
limalizike kwa uzuri na haraka.
8. Nyumba
safi ni pamoja na kufanya ukarabati. Hakikisha pale panapohitaji ukarabati
panarekebishwa mapema iwezekanavyo.
Na wewe msomaji wangu nishirikishe mikakati unayotumia kuhakikisha unaishi mahali pasafi.
Nijulishe kwa simu/whatsapp 0755 200023
No comments:
Post a Comment