Kama
tujuavyo sikukuu za mwisho wa mwaka zimekaribia. Na sikukuu maana yake ni
sherehe na shamrashamra kwa wingi. Hivyo basi kwa lengo la makala hii nimefanya
mahojiano na Asna Mshana ambaye ni mtaalam wa kuandaa sherehe na anaelezea ni
kwa njia gani rahisi kabisa unaweza kuandaa sherehe yako nyumbani msimu huu wa
sikukuu. Twende pamoja tuelimike na dondoo hizi za kuandaa sherehe ndogo ya
sikukuu nyumbani bila kutoa jasho.
·Kwanza kabisa unapaswa kujiuliza ni
muda gani sherehe
itafanyika?
Unapaswa kuamua unataka kufanya sherehe
ya chakula cha mchana au usiku. Sababu ya kufahamu hili ni mahitaji
yanayotakiwa kwa mfano baadhi ya maeneo, saba mchana jua ni kali sana kiasi
kwamba wageni wako watahitaji kivuli wakati kwa chakula cha usiku kivuli
hakihitajiki. Vilevile swala la mwanga linazingatiwa kuendana na muda wa
sherehe.
·Andaa orodha ya wageni na mialiko
Mara baada ya kuamua ni sherehe ya
muda gani unayoandaa (kwa maana ya chakula cha mchana au usiku), jihakikishie
tarehe, muda, orodha ya wageni na menu. Ukishaweka pamoja orodha ya watu unaowaalika
ndipo unaamua ni kwa jinsi gani unawafahamisha. Kusema ukweli kwa sherehe hii
ndogo tu ya nyumbani huna haja ya kuingia gharama za kutuma kadi za mialiko kwa
kipindi hiki cha mitandao lukuki ya mawasiliano. Unaweza kutuma mialiko kwa
ujumbe wa simu, barua pepe au hata kwa kuwapigia waalikwa simu. Tuma mialiko
angalau wiki mbili kabla ya sherehe kwakuwa sherehe kipindi hiki ni nyingi na
pia watu wanasafiri kwenda maeneo mbalimbali.
·Chagua menu rahisi
Watu wanaosambaza vyakula kwenye sherehe wana menu nyingi.
Chagua ambayo ni rahisi kwani sikukuu vyakula ni vingi kwenye nyumba nyingi.
Bila shaka wageni wako walishakula mno huko walikotoka. Chagua chakula kimoja
kimoja ili kupata menu kamili kwa ajili ya sherehe yako. Pia sherehe za buffet
huwa ni rahisi zaidi: Hii ina maana watu wa vyakula wanaweka vyakula tayari na
wageni wanajichotea wenyewe. Na hii inasaidia sana kwa maandalizi ya sherehe
kuliko kupika mwenyewe nyumbani.
Kama kwenye menu yako utachagua
viburudisho kama icecream itapendeza zaidi.
·Bandika vyakula majina
Kwa urahisi kwa wageni kujihudumia
vyakula vibandikwe majina, ili ijulikane kabisa hiki ni chakula fulani.
·Tengeneza eneo la vinywaji
Weka vinywaji, glasi sahihi na
barafu mahali hapo kwa ajili ya wageni wote wakiwa ni wale wanaopenda
kujihudumia wenyewe na baadhi wanaopenda kuhudumiwa. Endapo utakuwa unafahamu
idadi kubwa ya wageni wako wanatumia vinywaji gani (kutokana na ukaribu wako
kwao na sio kuwauliza kabla ya siku ya sherehe) itakusaidia sana kufanya
maandalizi kwa upande wa vinywaji.
·Vinywaji vya ziada
Weka vinywaji vya ziada ndani (mbali
na eneo la sherehe) ikiwa ni pamoja na napkini, barafu na glasi sahihi. Hili ni
jambo muhimu sana kuepuka aibu ya kuagiza vinywaji vya nyongeza dukani mbele za
wageni.
·Amua kuhusu mapambo
Kwa swala la mapambo usifikirie
mambo makubwa. Acha nafasi mezani kwa ajili ya vyakula na vinywaji kwa kuweka
ua dogo tu katikati ya meza na mshuma endapo ni chakula cha usiku.
·Tengeneza orodha na ratiba ya matukio
Angalau siku moja au mbili kabla ya
sharehe tengeneza orodha na ratiba ya nini kinatakiwa kifanyike na kwa muda
gani na mhusika ni nani. Hakikisha saa nzima kabla sherehe haijaanza kila kitu
kipo tayari ili kukupa muda wewe muandaaji kutulia na kufurahia mapokezi ya
wageni wako.
·Andaa kila kitu kiwe tayari kabla wageni hawajawasili
Vyakula na vinywaji vyote viwe mahali
pake kabla wageni hawajafika. Tumia msambaza chakula mwenye vifaa vya moto kwa
ajili ya kuweka vyakula katika hali ya moto muda wote. Ingawaje kuna baadhi ya
vitu huwezi kuviweka kabla ya ugeni (kwa mfano vipande vya barafu), ila
jitahidi kazi kubwa ya maandalizi iwe imekwishafanyika kabla ya kuingia wageni.
Kama utakuwa kwenye mpangilio na kila kitu kuwa tayari utakuwa kwenye nafasi
nzuri ya kuhudumia wageni wako.
·Sheherekea kwa furaha!
Mwisho lakini si dogo ni kufurahia
sherehe yako! Kama utakuwa na wakati mzuri wageni wako watakuwa na furaha pia.
Je, unauza
bidhaa au huduma inayohusu nyumba na bustani ambayo unataka Watanzania waijue?
Nijulishe simu/whatsapp 0755200023.
No comments:
Post a Comment