Huenda uko kwenye mchakato
wa kumalizia chumba cha jiko au labda unakifanyia marekebisho. Jiko la rangi
moja linapooza, ukiongeza rangi ndipo unajisikia kweli unapika.
Hizi hapa ni njia
unazoweza kutumia ili kuongeza rangi jikoni:
Kuweka marumaru za rangi
tofauti kwenye eneo dogo la ukutani.
Marumaru hizo zinaweza kuwa ni zile za
michoro inayohusiana na mambo ya jikoni kama vile zilizochorwa vyakula, laa
zinaweza kuwa ni ukanda mwebamba wa rangi tofauti na ya zilizoko kwenye sehemu
kubwa ya ukuta. Eneo hilo liwe ni la juu ya kaunta ili paonekane vizuri. Cha
muhimu ni ziwe na uwiano wa rangi na maeneo mengine ya jiko.
Kuboresha makabati. Huna
haja ya kuyaondoa ila unaweza kuyapaka rangi mabayo unadhani itafanya jiko
lichangamke na liwe na mvuto. Vilevile kumbuka kupaka rangi ambayo
itashirikiana na ya kuta. Kwa kupaka makabari rangi ya kuchangamka utaliongezea
jiko lako uhai kwani sehemu kubwa ya jiko inayoonekana ni makabati kuliko hata
ukuta.
Weka vitendea kazi ambavyo
vinaongeza rangi. Vifaa vya jikoni kama vile jokofu, kipasha chakula na visaga
vyakula unaweza kuvipata kwa rangi tofauti tofauti. Kama nia yako ni kuongeza
rangi jikoni basi chagua vitendea kazi vya rangi mbalimbali.
Weka sanaa za rangi
mbalimbali. Rangi kama nyekundu, zambarau na jamii za bluu zinavuta jicho
kuzitazama zaidi. Sanaa za kuning’niza zinatengeneza maeneo ya mvuto jikoni na
pia zinatoa utambulisho wa mwenye nyumba. Sehemu yenye nafasi nzuri ya
kuzitundika ni juu ya dirisha, na hii ni kwakuwa pia wengi hawaweki pazia
jikoni kwahivyo mahali hapo ni sahihi kutundika sanaa zako za ukutani za
jikoni.
Ongeza rangi kwenye
shelfu. Kuna wale wenye majiko makubwa yenye eneo la shelfu za wazi. Kama
umebarikiwa kuwa na jiko la aina hii basi unaweza kutumia eneo hilo aidha
kulipaka rangi au kuweka vyombo vya rangi. Kama utaamua kupaka shelfu rangi
basi weka sahani nyeupe, ila kama utaacha shelfu na rangi yake ya asili au na
rangi nyeupe basi weka sahani na vyombo kama vile majagi na mabakuli makubwa ya
rangi. Kwa namna hii ni kama mashelfu yanaongea na mtazamaji.
Zama kwa undani zaidi. Maadam
mkakati wako ni iwe iwavyo unataka kuongeza rangi jikoni basi zama hadi kwenye
vitu vidogodogo. Hapa ni pale ambapo umeshafikiria yale maeneno makubwa kama
makabati, kaunta, ukuta, sakafu na vifaa. Sasa zama kuongeza rangi kwa kupitia
vitu kama vile vikombe, glasi na vikontena vya kuhifadhia vyakula.
Bila shaka msomaji wangu
kama ulikuwa unawaza ni kwa namna gani upambe jiko lako, makala hii itakuwa
imekupa mwanga wa nini cha kufanya.
Ukishapamba nishirikishe kwa
simu/whatsapp 0755 200023 ili tuzidi kuelimisha na wengine.
No comments:
Post a Comment