Kuwa na
pazia zinazovutia inaweza kuwa changamoto.Kuna mambo mengi unayopaswa
kuzingatia kuhakikisha kwamba pazia husika zinaoana na rangi na mapambo ya
chumba chako na mpangilio wake. Baadhi ya mambo hayo ni haya yafuatayo:
·
Kwanza kabisa
weka pembeni suala la muonekano kwani lengo namba moja la pazia ni kufunika
dirisha. Kwa sehemu kubwa lengo hili ndilo litakubana kwa njia nzuri unapochagua
pazia zako. Kama unataka pazia zinazoleta faragha au giza kabisa, unatakiwa
kuwa na pazia zenye kitambaa cha pili (lining) kwa ndani. Kitambaa hiki
kitaongeza gharama lakina kina faida nyingi kama vile: kuzuia kile kitambaa cha
nje cha pazia (ambacho ndio maridadi) kisiharibiwe na jua na hivyo kudumu muda
mrefu. Kitambaa cha ndani pia kinaongeza uzito wa pazia na hivyo kulifanya limwagike
vizuri na kutulia bila kuhamahama hata kama umewasha pangaboi. Na vilevile
lining linafanya pazia kuonekana la kifahari. Pazia za hivi nyingi ni za
kushonesha, huzikuti zikiwa zimeshonwa tayari.
Ni vizuri ifahamike kuwa pazia zinaweza kutofautiana
kimatumizi kati ya chumba na chumba. Kwa mfano kwenye chumba cha chakula pazia
zinaweza kuwa na lengo la kimuonekano zaidi, ikimaanisha nyembamba, nyepesi na
zenye urembo mwingi wa matobotobo. Kama unalala chumba ambacho kina dirisha
linalopokea mwanga mwingi wa asubuhi, pazia zenye rangi za giza zitakusaidia
kuzuia jua na kuongeza muda zaidi wa kulala siku za mwishoni mwa wiki bila jua
kukusumbua wakati umelala.
·
Zingatia
rangi za pazia unazotaka kununua ukilinganisha na mapambo mengine ya ndani. Kwa
mapambo ya ndani rangi ya pazia ikiwa ya giza kuliko ile ya ukuta inafanya
chumba kipendeze zaidi. Kwa mfano kama ukuta una rangi ya bluu iliyofifia basi pazia
ziwe na bluu iliyokolea. Pia ukichagua rangi ya pazia ambayo haijashamiri
kwenye rangi nyingine zilizoko hapo chumbani huwa chumba kinaleta mvuto zaidi. Ile rangi ya
kipekee (iliyokolea tofauti na nyingine zote) ya pazia inaleta mshtuko wa uzuri.
· Urefu wa pazia.
Pazia la kufika sakafuni ndio sahihi, vinginevyo kuwe na sababu ya kipekee. Na
uzuri pazia nyingi zilizoshonwa tayari zinakidhi urefu huu. Kama unanunua kwa
mita pima kutoka sakafuni hadi kwenye fimbo utakayotundikia pazia. Kama
linazidi kumwagika sakafuni ni bora kulipunguza kwa sindano ya mkono kuliko
pazia fupi.
· Pazia liwe pana
kiasi gani? Ili pazia liwe na marinda na limwagike vizuri linatakiwa kuwa na upana
mara mbili hadi mbili na nusu zaidi ya upana wa dirisha. Isipokuwa kama unaweka
pazia kwa ajili tu ya kufunika dirisha basi hata upana wa zaidi ya mara moja na
nusu ya dirisha utafaa. Pazia pana lililojaa marinda ndio halali ya dirisha.
· Umbali wa
kutundika pazia toka juu ya dirisha uwe wa kutosha. Angalao kuwe na inchi 4
hadi 6kutoka kwenye dirisha hadi pale pazia lilipoanzia. Lakini vilevile
lisikabe dari. Kwahiyo kumbuka kuhesabia urefu huu wa ziada wakati unaponunua
au kushonesha.
· Kuhusu muonekano
wa juu linakoanzia pazia. Kwenye ule ukanda wa juu kabisa wa pazia ndiko
kunasemea uzuri wa pazia zima. Ingekuwa pazia ni mwanamke hapa ndipo tungesema
ni uso wa pazia. Marinda, vyuma na kulabu katika eneo hili zinatakiwa kukaa
vizuri maridadi na katika umbali wa kulingana. Hapa ndipo panafanya ufunguzi na
ufungwaji wa pazia uwe rahisi au mgumu.
· Pazia linapotundikwa.
Je, linatundikwa kwenye boksi ama fimbo za pazia. Na je likifunguliwa
linafungwa kwa tai au linajiachia lenyewe? Yote haya unatakiwa kuyafahamu kabla
hujaanza huo mradi kwa kufunga pazia. Na je tai ni zile zimejengewa ukutani au
ni zile za vitambaa? Unapaswa kufahamu yote haya ili pazia zikidhi malengo ha
wakati huohuo zikionekana maridadi.
Makala hii imeandaliwa na Vivi.
Je, unauza
bidhaa au huduma inayohusu nyumba na bustani ambayo unataka Watanzania waijue?
Nijulishe simu/whatsapp 0755200023. www.vivimachange.blogspot.com
No comments:
Post a Comment