Chochea
furaha na msisimko wa kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kupamba ndani
na nje ya nyumba yako. Vitu rahisi hata kama ni vijipambo vya meza tu huleta tofauti
kubwa ya muonekano wa mazingira ya nyumbani.
Baadhi ya njia tofauti unazoweza
kuhuisha muonekano wa kizamani wa nyumba yako ni kama ifuatavyo:
Ongeza picha na michoro: Kuongeza picha nyumbani kwako
kunaongeza muonekano mpya mara moja kutoka ule wa zamani. Ni njia rahisi kabisa
kuhuisha sebule yako. Unaweza kuongeza picha za familia ama nunua picha za
fremu kuleta muonekano wa kipekee.
Ongeza mimea na maua: Pamba mazingira ya ndani na nje ya nyumba kwa maua na mimea. Vyungu
na vesi za maua nje na ndani ya nyumba vinaleta mvuto.
Badili pazia: Pazia za kila siku zinafanya
nyumba isionekane tofauti. Hakuna kitu kinacholeta tofauti kubwa kwenye
muonekano wa nyumba kama pazia.
Paka rangi: Huisha kuta za mazingira ya nyumbani kwako
japo kwa kuongeza mkono mmoja tu ya rangi.
Weka mito mipya: Badilisha mito ya sebuleni na
uweke ya rangi mbalimbali hasa zile zinazoendana na sikukuu. Mito yenye rangi
kali zilizokolea kwenye sofa zako au hata ile mikubwa ya kukalia sakafuni
inabadilisha muonekano wa ndani ya nyumba bila ya kutumia gharama na nguvu
kubwa.
Panga vitu upya: Kuhamisha fenicha toka eneo moja
hadi lingine kunasaidia kubadili muonekano wa chumba.
Weka mapambo madogodogo: Kipindi hiki cha sikukuu
mapambo ni mengi madukani. Tumia nafasi za wazi kama vile juu ya kabati au
shelfu na kadhalika kuweka mapambo katika kila chumba kuleta ladha ya sikukuu. Pia unaweza kuzungushia
taa zisizo na gharama za kumeremeta za msimu huu wa sikukuu kwenye miti ya
bustanini au eneo la lango kuu au hata eneo la ngazi ili kuleta mvuto.
Kama tujuavyo
sikukuu za mwisho wa mwaka zinazokuja ni krismasi na mwaka mpya hivyo usisahau
kupamba kwa mti wa krismasi! Mti huu umekuwa ni pambo la kipekee kwenye nyumba
nyingi duniani na hata maeneo ya jumuiya na ofisi nyingi kila mwaka kwenye
sikukuu ya krismasi.
Bila
shaka utatumia njia kadhaa kati ya hizi kupamba nyumba yako sikukuu hii.
Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange. Nitumie picha ya namna
ulivyopamba sikukuu hii. Simu/whatsapp 0755 2000 23
www.vivimachange.blogspot.com
No comments:
Post a Comment