Hakuna
sakafu ambayo ni laini na yenye hisia za kifahari kama ya zulia. Ndio maana ni
utamaduni wa dunia nzima kwa watu mashuhuri kutembea juu ya zulia wakati wa
dhifa mbalimbali za kitaifa na kimataifa.
Zulia
ni sakafu yenye usalama zaidi kwa michezo ya watoto na hata
uwezekano wa wao
kuanguka na kuumia ni mdogo. Ni ukweli kuwa zulia linahitaji utunzaji wa ziada
ukilinganisha na sakafu nyingine kama za marumaru au tarazo. Kuwepo kwa rangi,
malighafi na mitindo mingi ya mazulia, inaweza kukuwia vigumu kuchagua lililo
sahihi kwa ajili ya nyumbani kwako. Rangi nyingine zinaweza kuhitaji usafi wa
kila mara ambapo haitaendana na ratiba yako ya mchakamchaka wa kila siku. Vilevile
mazulia yenye rangi moja na zilizokolea sana yana tabia ya kupauka. Endapo
unaweka zulia la namna hiyo sehemu linayopitiwa zaidi ina maana sehemu hiyo itaacha
alama za kupauka. Mazulia ya hivi
yanafaa zaidi kwenye chumba cha kulala kuliko sebuleni au kwenye corridor. Zulia
lisilo sahihi linaweza kuchakaa haraka, kupauka au kung’ang’ania madoa hata
kama utalisafisha vipi. Tumia fedha zako kwa akili wakati wa kununua zulia kwa
kuzingatia dondoo hizi.
Bajeti
Bajeti
ni dondoo muhimu sana ambayo ndio itasimamia nyingine zote zinazofuata. Utagundua
kuwa kuna tofauti kubwa ya bei kati ya mazulia ya manyoya ya unene fulani ukilinganisha
na ya unene wa tofauti yake. Ukiwa tayari una bajeti yako ni rahisi kuamua ni zulia
lipi unaloweza kumudu.
Ubora
Ubora
hapa tutauangalia katika nyanja mbili, kwa zulia jipya au la mtumba. Kwa
mazulia mapya najua baadhi ya wanunuzi hapa nchini hasa kwenye miji mikubwa wamezoea
kwenda kununua kwenye eneo moja tu kwa sababu labda ndilo wanaloamini kuwa
wanaweza kupata mazulia. Ila kiukweli kuna showroom nyingi zenye mazulia
tofauti tofauti ya kutoka nchi mbalimbali na ubora wake vilevile ni wa ngazi
tofauti tofauti. Zulia unalotaka kununua
hakikisha lina manyonya yaliyojishindilia. Hutataka kununua lenye manyoya
machache kiasi kwamba baada ya muda mfupi linachakaa. Unahitaji zulia lenye
ubora wa hali ya juu ambalo linakuhakikishia kuwa nalo miaka mingi hadi
ulichoke mwenyewe uamuae kulibadilisha.
Kwa
upande wa zulia la mtumba cha muhimu ni kuhakikisha unachagua lile lililo
kwenye hali nzuri zaidi ambayo unaweza kuiamini. Uzuri wa mazulia mengi ya mitumba ni kwamba yanaonyesha
mwaka yaliyotengenezwa kwahivyo ni rahisi kugundua ubora wake kwa kuangalia ni
muda gani limetumika.
Na
pale unapotaka kununua vizulia vidogo vya milangoni au bafuni, ni vyema
kuhakikisha vina ule mpira eneo linaloshikana na salafu ili kuzuia utelezi na
pia majimaji kupenya kwenye manyoya.
Ukubwa
Ukubwa
wa zulia unalotaka kununua ni kigezo muhimu cha kufanya maamuzi. Hakikisha
unapima eneo unalotaka kuliweka ili uweze kutambua ukubwa sahihi wa zulia unalohitaji.
Sichoki kusisitiza kuwa fenicha zinatakiwa zikae juu ya zulia na miguu ya
mkaaji inatakiwa nyayo zitue kwenye zulia. Kizulia kidogo sana kwenye chumba
kikubwa huwa kinaleta ukakasi na kuonekana kama kitu kilisicho mahali pake.
Rangi na michoro
Mwanzoni
nimegusia kidogo kuhusu rangi. Kabla hujatoka nyumbani kwenda kununua zulia
piga picha ya vyumba unavyotaka kuweka mazulia hayo. Kuna rangi ambazo
zinasaidia kupunguza ukali wa rangi nyingine. Kwa mfano, kama chumba kina rangi
za mwanga, zulia la rangi nzito/giza litafaa ili kupunguza ule mwanga. Fikiria
je unataka rangi na michoro ya zulia iwe ndio kitovu cha chumba?
Rangi
na michoro ya giza inasaidia kuficha madoa. Mara zote angalia sampo ya rangi ya
zulia unayotegemea kununua kabla hujafanya maamuzi.
Ahsante
ReplyDelete