Wengi
walishayapitia au wanayapitia haya! Unapanga nyumba au chumba unakuta nafasi ni
ndogo sana unaumiza kichwa kufikiria utahifadhije nguo zako maana ukiweka
kitanda tu nafasi imeisha huna pa kuweka kabati la nguo. Lakini maisha yanaendelea hayasimami na kwa
maana hiyo nguo pia lazima zihifadhiwe
na kutolewa ili zivaliwe. Usife moyo! Kuna namna ya
kufanya sehemu yako
hiyo ndogo iwe na mpangilio wa nguo zako na pakaonekana bomba kabisa.
Nimekukusanyia
njia kadhaa za kuweza kuhifadhi nguo zako bila kabati kama ifuatavyo:
Tengenezesha stendi rahisi ambayo unaweza kutundikia nguo
Stendi ya nguo ni
msaada wa ajabu unaoweza kuwa nao kwenye chumba chako cha kulala bila ya kuwa
na kabati la nguo. Iwe ni ile ya kutundika nguo kwa kutumia henga au ni ya
kutundikia moja kwa moja bila henga, stendi ni msaada mkubwa. Stendi inachukua eneo dogo sana la sakafu. Unaweza kuitumia
kwa kutundikia, blauzi, makoti, majaketi, suruali, magauni, sketi na hata
mabegi.
Si mbaya kutengenezea
kishelfu eneo la chini. Hapa panakuwa ni mwake kwa ajili ya kutandaza viatu
vyako na hivyo kutumia eneo la sakafu ambalo ungewekea viatu hivyo kwa shughuli
nyingine. Na pia inaweza kuwa nzuri zaidi kama utaweza kuwa na stendi yenye
ngazi zaidi ya moja ya shelfu. Hii yote itategemea na hitaji lako.
Ning’iniza bomba la kutundikia nguo
Kuning’iniza bomba la
kutundikia nguo kunaweza kukushangaza
lakini linafaa sana kama chumba ni kidogo sana kiasi kwamba hata kuweka stendi
unaona kama unamaliza nafasi. Unapohamia kwenye chumba au nyumba ndogo
inakupasa kuchanganya akili kadri uwezevyo kwa kutumia kila mbinu kuhakikisha
kuwa vitu vyako vyote vinakaa vizuri bila kuonyesha hali ya kurundikana na huku
ukibakiwa na nafasi ya kutosha. Ni rahisi, fundi anakuning’inizia kamba mbili
imara toka kwenye dari na kuzitumia kushikilia hilo pomba la kutundikia. Zaidi
ya kutundikia nguo zako na kuhifadhi eneo la sakafuni, muonekano wake pia ni
kivutio. Zingatia hizo kamba za kuning’iniza ziwe imara kwani fimbo itakapowekwa
nguo uzito utaongezeka sana. Hakuna kitu kinachoshtua kama usiku unaposikia
kitu kimenguka kwa nguvu ndani ya chumba ulicholala.
Funga mashelfu ukutani
Bila shaka ulishawahi
kuona mfanyibiashara anapohamia kwenye fremu mpya jinsi anavyoweka mashelfu.
Kwa mtindo huu huu kama una chumba ambacho hakitoshi kuweka kabati la nguo unaweza
kuchagua eneo la ukuta na ukafunga mashelfu kwa ajili ya kuhifadhia nguo zako.
Yanaweza kuwa ya gharama nafuu kabisa hata kama yanatokana na matenga ya nyanya! Cha muhimu ni kwamba yatakupa eneo salama na
safi la kuhifadhia nguo zilizokunjwa, viatu, vitabu, pochi na vingine vingi
ambavyo moyo wako unatamani. Unaweza ukayapamba kwa kuyapaka rangi mbaimbali au
hata kwa rangi moja.
Kuwa na ubao mrefu wa kitanda
Unapokuwa na kitanda
chenye ubao mrefu wa kichwani, unaweza kuchimbia kulabu nyuma ya ubao huo
ambapo utazitumia kutundika nguo ambazo utazivaa kwa wiki nzima. Zile za ziada
hifadhi kwenye masanduku na yaweke mvunguni mwa kitanda lengo likiwa ni
lilelile la matumizi mazuri ya nafasi. Itakapofika mwisho wa wiki, unachagua
tena nguo nyingine kwa wiki inayofuata. Kiukweli eneo la nyuma ya ubao wa
kitanda huwa linakaa tu bila kazi ambapo linaweza kutumika vizuri tu.
Kwa wewe uliyekuwa na
changamoto ya namna hii bila shaka umefaidika na elimu hii. Zaidi kwa ushauri wa namna ya kuweka mpangilio nyumbani kwako tuwasiliane 0755 200023
No comments:
Post a Comment