Thursday, June 9, 2016

Alama za onyo kwenye vifaa vya umeme vya nyumbani

 
Unavyoishi maisha ya kila siku hapo nyumbani, unategemea vifaa vya umeme vilivyopo zaidi ya hata unayoweza kudhania. Pale tu kifaa kinapoharibika ndipo unaanza kuona umuhimu wake. Nyumba nyingi za kisasa ni kawaida kukuta vifaa vya
umeme kama vile jokofu, kipasha na kisaga vyakula, kifaa cha kupashia maji moto, jiko na hata baadhi ya nyumba hizo zikiwa na nyongeza ya vifaa vingine kama vile mashine ya kufulia, viyoyozi, tanuri na hata mashine ya kuoshea vyombo. Nimeungana na fundi vifaa hivi ndugu James Urio na anatujuza dalili za kifaa chako kuhitaji matengenezo au kukibadilisha kabisa na kuweka kingine. Twende pamoja msomaji wangu.

·        Kifaa hakiwaki:
Ni ukweli kuwa kama kifaa hakiwaki ina maana kwamba huwezi kukitumia kabisa kwahivyo kinahitaji matengenezo. Kabla hujanyanyua simu kumuita fundi hakikisha kwamba kifaa kimechomekwa vizuri kwenye chanzo cha umeme na pia hapo mahali pawe na umeme. Mara unapogundua kuwa tatizo liko kwenye kifaa mwite fundi aje akiangalie.

·        Matumizi makubwa ya umeme isivyo kawaida:
Kutokutengeneza kifaa inaweza kuonekana kuwa ni njia nzuri kuhifadhi pesa yako, lakini kama bili ya umeme ndani ya mwezi ni kubwa kuliko kawaida ya miezi ya nyuma, inaweza kumaanisha kuwa  vifaa vyako kimoja au zaidi havifanyi kazi ipasavyo kwahivyo vinatumia umeme mwingi kuliko kawaida. Matengenezo yanaweza kukifanya kifaa hicho kufanya kazi kama awali na kurudisha gharama za umeme hapo nyumbani kwako katika hali ya kawaida.

·        Dalili nvingine za ubovu:
Ukishatumia kifaa baada ya muda unakizoea na kujua kabisa namna kinavyofanya kazi, kama kipo kinachoanza kutoa dalili za ajabu ajabu, huenda kinahitaji matengenezo. Kwa mfano, jokofu linaloanza kuchuruzisha maji au kipasha chakula ambacho inabidi kurudia mara mbili ili uweze kupata matokeo unayotaka au labda pasi ambayo  haishiki moto mkali hata pale unapoiwasha hadi kiwango cha juu kabisa. Zote hizo ni dalili kuwa matengenezo yanahitajika.

Ili kuamua kama kifaa ni cha kutengeneza au kununua kipya unapaswa kuangalia mambo yafuatayo:
·        Fuata kanuni ya 50%:
Hii ndio njia nzuri kuliko zote za kukusaidia kuamua kama ni bora hela yako ukaitumia kwenye matengenezo au kwenye kununua kifaa kingine. Kanuni ya asilimia 50 inasema kuwa kama kifaa kina zaidi ya asilimia 50 ya uhai wake na kukitengeneza pia ni zaidi ya asilimia 50 ya gharama ya kununua kipya, ni vyema ununue kipya.  Wakati wa kununua kifaa unapewa wastani wa uhai wake. Fundi mwelewa ana uwezo wa kukuchambulia haya yote kwa kukupa gharama zote na ndipo unaweza kufanya tathmini yako ili kufanya uamuzi sahihi.

·        Fikiria waranti:
Kama kifaa chako kimeanza kuleta matatizo wakati ambapo bado ni kipya na kiko kwenye waranti, wasiliana na ulikokinunua na kuwajulisha mara moja. Matengenezo na spea unaweza kupewa bure kabisa kama waranti inasema hivyo.

·        Zingatia kuwa kifaa kipya kina gharama zilizojificha:
Gharama ya kununua kifaa kipya zinaweza kuwa zaidi ya zile unazopewa dukani. Kama kifaa kinahitaji usimikaji wa kitaalam kutakuwa na gharama za ziada za fundi. Vilevile kifaa kipya kinaweza kisifiti kwenye eneo la mwanzo, ambapo inaweza kukugharimu kupafanyia mabadiliko/maboresho. Angalia gharama zote hizi zilizojificha wakati unapoamua kubadilisha kifaa kibovu ili kuweka kipya.


Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment