Teknlojia inawapa fursa zaidi
wanaojenga kuchagua aina ya paa wanalotaka kuezekea nyumba zao. Mhandisi David Sembuyagi
anatujuza faida na changamoto za paa la zege.
Ingawa paa la zege linaweza kuwekwa
kwa mitindo mbalimbali, kwenye makala haya tutaangalia paa la zege lililo
flati.
Paa la zege ni mchanganyiko wa
saruji, mchanga, kokoto na
maji kwa uwiano unaokubalika.
Hata hivyo paa la zege kwa Watanzania
sio maarufu hasa kwenye nyumba za makazi.
Hii huenda ni kwa sababu wengi hawana uelewa juu ya paa hili na wengine
wanaogopa gharama japo kiukweli hawajatafiti kujua gharama halisi na pia wapo
ambao hawajashawishiwa kujua faida za paa la namna hii au kuona miundo yake
mbalimbali ya kuvutia kuliko hata mapaa mengine kama ya bati na vigae.
Hebu tuangalie faida na changamoto
za paa la zege ili tulifahamu zaidi na kama unatarajia kujenga uweze kufanya
uamuzi sahihi kwa kuona ni paa lipi linakufaa.
Faida namba moja ya paa la zege ni
kuwa linadumu miaka mingi hadi miaka 50 hasa pale linapokuwa limewekwa vizuri. Halihitaji
matengenezo ya mara kwa mara na linaondoa wasiwasi wa kushika moto.
Paa la zege haliwezi kuezuliwa na
upepo ukilinganisha na paa la bati. Hii ni faida hasa kwa wale walio maeneo
yanayokumbwa na upepo mkali kwenye majira fulani ya mwaka.
Ni rahisi kusafisha. Kupanda juu ya
paa la zege na kusafisha kwa maji yenye msukumo mkubwa kuna usalama zaidi kuliko
kwenye mapaa mengine kama yale ya vigae. Paa la zege haliharibiwi kwa
kulikanyaga. Ila changamoto ya paa la zege lililo flati ni
kwamba linakusanya takataka zaidi hasa kama nyumba iko chini ya miti kulinganisha
na mapaa mengine ambayo takataka zinateleza na kudondoka .
Paa
la zege halisababishi joto ndani ya nyumba na pia mvua ikinyesha halipigi kelele.
Unaweza
kutumia eneo la juu ya paa la zege kwa ajili ya matumizi mengine kama vile kukaa
na kubarizi, na pia kuwekea matanki ya maji ya akiba.
Paa la zege linahitaji msingi na
kuta za nyumba husika ziwe imara kwa vile zege ni zito sana kwahivyo vilivyo
chini yake vinatakiwa kuwa na nguvu ya kulibeba.
Japo wanaojenga wamekuwa wakiogopa
kuwa gharama za paa la zege ni kubwa, kiuhalisia inawezekana isiwe kweli. Kwani
paa hili linajitosheleza, halihitaji malighafi nyingine zozote kama vile gypsum
na nyinginezo za kupaulia. Kwahivyo utaona kwamba kwa malighafi za kisasa na
kupaua ni kama vile gharama sawa na paa la zege.
Mawasiliano 0755 200023
No comments:
Post a Comment