Friday, June 17, 2016

Unavyoweza kupendezesha nyumba kwa fenicha nyeupe



Hebu fikiria muonekano wa ndani ya nyumba yako utakuwaje pale unapoamua kupendezesha maeneo ya wazi kwa fenicha nyeupe. Maeneo ya wazi ndani ya nyumba ni yale ambayo mtu yeyote awe ni mgeni au mwenyeji anaweza kwenda. Maeneo hayo ni sebuleni, jikoni na chooni.

Wengi wanapenda kubadili mionekano ya ndani ya
nyumba zao ambapo mabadiliko hayo lengo kuu huwa ni kuboresha ili  kuonekane freshi na kwa kisasa zaidi. Kabati la luninga jeupe, kabati la vyombo jeupe, shelfu za vitabu nyeupe, meza ya kahawa na hata makabati ya jikoni meupe ni fenicha unazoweza kutumia zikiwa na rangi nyeupe kwani rangi hii haipitwi na wakati.

Muulize mbunifu wa ndani yeyote atakuambia kuwa nyeupe ni chaguo sahihi kwa chumba chochote ndani ya nyumba.

Fenicha nyeupe zinaleta hisia ya usafi, zinafanya chumba kionekane kikubwa na mwanga wa kutosha. Hii inasaidia sana hasa kwa vyumba vidogo ambapo kuwa na rangi za giza kunavifanya vionekane vidogo zaidi.
Hebu fikiria uzuri wa kuwa na kabati la luninga jeupe halafu unaweka luninga nyeusi. Wote tunajua namna nyeupe na nyeusi zinavyopendeza pamoja. Kabati ya luninga jeupe pamoja na mashelfu havikosei kwani vinaendana na rangi nyingi zozote za vitu ulivyo navyo sebuleni.

Au kabati la vyombo jeupe kwenye chumba cha chakula huku ukiwa umetandaza sahani zako za rangi, maua na michoro mbalimbali kwenye zile shelfu za wazi. Tafiti miundo mbalimbali ya makabati meupe ya luninga au vyombo na uwe mbunifu wa ndani mwako. Yale makabati ya luninga ambayo yanakuja na mashelfu yanamsaidia mwenye nyumba kupata eneo la kutandaza picha za familia, sanaa na vitabu. Pia zinakuwa na droo za kufunga kwa kuhifadhia vile vitu usivyopenda vionekane wazi.
Kiukweli kabati jeupe la luninga linaweza kuvutia sana. Chaguo ni lako wewe unayetaka kupendezesha nyumba yako.

Mashelfu meupe yawe ni ya vitabu au ni yale madogo ya kutundikwa ukutani kwa ajili ya kuwekea picha, maua na vitupio mbalimbali vya kupendezesha ukuta yana mvuto wa kipekee. Shelfu nyeupe zinaposimamishwa mbele ya ukuta ambao nao una rangi ya mwanga chumba kinaleta hisia nzuri.

Makabati meupe jikoni na kwenye bafu za kisasa ni kwa ajili ya kuhifadhia karatasi za chooni na vitu vingine vinavyohusika na huko wakati yale ya  jikoni yakihifadhia vitu vikavu ikiwa ni pamoja na vyomba na vyakula.

Aina gani ya fenicha nyeupe utumie ni chaguo lako binafsi. Kutegemea na vitu ulivyonavyo iwe ni vitabu, vitupio vya mapambo, vitu vya burudani au chochote kile. Wengi mtagundua kuwa kutumia nyeupe ni chaguo zuri kwani ni rangi ya wakati wowote. Na hata pale unapoamua kubadili rangi inakuwa rahisi zaidi kama rangi ya awali ni nyeupe.
Yeyote anayetaka kuwekeza kwenye fenicha za ndani rangi nyeupe ina mvuto usiopingika.

Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment