Ndege iliyokuwa imembeba rais mstaafu wa Marekani, Bill
Clinton na mwanaye Chelsea, juzi ilipata hitilafu katika moja ya injini zake na
kulazimika kutua Dodoma kwa ajili ya matengenezo kabla ya kuendelea na safari.
Ndege hiyo aina ya DHC 7 yenye namba za usajili 5Y-CDK,
iliyokuwa ikitokea
mkoani Iringa kuelekea Ziwa Manyara, ilitua saa 10.15 jioni
juzi na kuondoka saa 10.24 jioni.
Chanzo cha habari kutoka uwanja huo wa ndege, kilisema
ndege hiyo ilikuwa na tatizo dogo na lilirekebishwa wakati Clinton na abiria
wengine wakiwa ndani ya ndege.
“Tulimuuliza rubani wa ndege hiyo kama angehitaji msaada
wowote kutoka kwetu, lakini alisema kuwa ni tatizo dogo tu na angeweza kutua
mwenye bila msaada na akafanya hivyo,” alisema mpashaji habari huo aliyeomba
jina lake lisitiriwe.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, meneja wa Mamlaka ya
Usafiri wa Anga, (TCAA), Ludovic
Ndumbaro alikataa kulizungumzia kwa madai yeye si msemaji wa mamlaka hiyo.
“Mtafute mkurugenzi ndiyo msemaji wa mambo yote
yanayohusu mambo ya anga,” alisema.
Clinton na binti yake Chelsea walifika Tanzania kukagua
miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na mfuko wa familia ya Clinton.
Gazeti la mtandaoni la CBSNews.com jana liliandika kuwa
ratiba ya safari ya Clinton inaonyesha kuwa ndege hiyo haikutakiwa kutua
Dodoma, lakini kwa sababu ya hitilafu iliyojitokeza rubani akaamua kutua ili
kutatua tatizo.
Hata hivyo, CBSNews.com lilimkariri msemaji wa mpango wa
maendeleo wa Clinton aliyesema hakukuwa na dharura yoyote.
Clinton ataendelea na ziara yake ya siku tisa katika nchi
za Kenya, Liberia na Morocco. Miradi inayosimamiwa na mfuko wa Clinton ni ya
kilimo cha kibiashara.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment