Friday, November 11, 2016

Namna ya kutunza bustani katika majira ya vuli

Hata uwe na maji mengi kiasi gani ya kumwagilia bustani, ni ukweli kuwa kiangazi kinatesa bustani nyingi. Watunza bustani wanatumia muda mwingi kuitunza kuliko majira mengine ya mwaka. Sasa majira yanabadilika tunategemea mvua za vuli na ni
fursa nzuri ya kuirudisha bustani yako kwenye uhai wake.
Zifuatazo ni dondoo za namna ya kutunza bustani katika majira ya vuli, ili ianze tena kung’aa kwa kile kijani ambacho kimepotezwa na kiangazi kirudi.

Kwanza kabisa ni vyema ufahamu wakati wa kukata majani na kukatia maua. Hii ni muhimu kwa ajili hata wakati wa kiangazi hupaswi kukata majani kila mara au pia kuyakata yawe mafupi sana! Nimewahi kuona bustani nyingi ambazo zinakatiwa chini kiasi kwamba unaogopa kama majani yatachipua tena.

Maadam vuli inakuja na mvua kiasi japo sio kama masika, kwa bustani inatosha tofauti na mazao mengine. Majani bila shaka yatachipua na muonekano mzima utakuwa wa kuvutia.

Kumbuka kuweka mbolea. Kipindi cha mvua za vuli ni kizuri kwa ajili ya kuweka tena mbolea bustanini. Mbolea ya wanyama hasa kuku inafaa sana kurutubisha majani yashamirishe kijani chake ambacho kilipotezwa na majira ya nyuma.

Kupunguza au kuacha kabisa umwagiliaji. Kuendana na mkoa uliopo huenda mvua za vuli zikakurahisishia sana kazi ya umwagiliaji wa bustani. Kwa sababu mvua zitanyesha hutapaswa kumwagilia kivile. Kama uko mikoa ya baridi ni kwamba hutamwagilia kabisa kipindi cha majira ya vuli wakati wale wa mikoa ya joto (ukanda wa pwani) wanapaswa kumwagilia kwa kiwango kidogo sana.

Zalisha mboji. Vuli ni wakati mzuri wa kuzalisha mbolea ya mboji ambayo ni mbolea inayotokana na majani. Wakati wa kiangazi majani yanakauka na hayawezi kutengeneza mbolea, kwahivyo kama kuna majani makavu ulikusanya wakati wa kiangazi sasa ni wakati muafaka wa kuyatandaza kwenye vitanda vya maua ili yapigwe na mvua yaoze kutengeneza mbolea.

Zuia mbu. Hili ni jambo ambalo wengi wanasahau wakati wakiandaa bustani zao kwa mvua za vuli. Kama tujuavyo mbu wanazaliana kwenye maji yaliyosimama. Tembea ndani ya bustani yako na nje ya nyumba kwa ujumla kuhakikisha kuwa hakuna kitu ambacho kitasimamisha maji na kusababisha mbu kuzaliana.
Kitu chochote ambacho ni chanjo cha maji kusimama ni tatizo kwani mbu wanaweza kuzaliana hata kwenye maji yaliyosimama katika mfuniko wa chupa ya soda (kisoda).

Kuwa makini na mabadiliko ya tabia nchi. Ingawa tunasema ni ujio wa kipindi cha mvua za vuli lakini sio lazima ziwepo kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya tabia nchi.

Kutunza bustani ni zaidi ya kuifanya ivutie. Dondoo hizi zitakusaidia kuwa na busatani yenye afya ambayo inaweza kuitunza yenyewe na hatimaye kupunguza kazi kwa upande wako. Utaifurahia vuli huku ukisubiri kiangazi kije tena.


Nifuate instagram @vivimachange

No comments:

Post a Comment