Kwa nyumba nyingi ambazo wenyeji wana magari watakubaliana na
mimi kuwa matairi chakavu wakati ulipoyaondoa kwenye gari kama hukuyaacha kule
gereji basi yameishia kurundikana eneo la nje ya nyumba yakikusanya vumbi, taka
mbalimbali na makazi ya wadudu. Badala ya kuyaacha gereji au kuyatupa je,
kwanini usiyabadilishe kuwa kitu cha kuvutia na vilevile cha manufaa?
Mpira
unaotengenezea tairi hakika ni
malighafi imara na sahihi kwa matumizi ya nje.
Hakuna tahadhari yoyote ya kutumia matairi haya bustanini. Mara yanapowekwa
mahali hayaozi na kuna uwezekano wa kuwa hapo hadi yakatumika na wajukuu zako
endapo hutayaondoa!
Katika
makala hii nitakuelimisha njia kadhaa za kiuubnifu ambazo unaweza kutumia ili
uweze kutumia tena matairi yaliyokwisha muda wake wa kutumika kwenye magari.
Unaweza
kugeuza hayo matairi chakavu kwa kutengenezea vitu mbalimbali kuanzia vyungu vya
maua, fenicha na hata michezo ya watoto. Unaweza kuyatumia kama mapambo, kuyazungushia
kwenye miti midogo ambapo mti unakua ukiwa umezungushiwa matairimawili au
matatu, pia kutengenezea bembea za
kwenye miti.
Matairi
chakavu yanaweza kutumika bustanini yakiwa pamoja kwa ajili ya kutengenezea
vitanda cha maua au hata mbogamboga kama ni bustani ya mboga. Bustani hizi
ndogo za matairi huwa zinahitaji maji kidogo. Unaweza kuyapaka rangi mbalimbali
matairi haya na kutengeneza kazi ya sanaa yenye mvuto wa aina yake.
Ni
rahisi sana kufanya hata mwenyewe bila msaada unachohitaji ni tairi chakavu,
brashi na rangi kidogo tu.
Kwa
kutumia matairi mawili chakavu yaliyoshikiliwa pamoja, kivuniko cha kioo au
kamba kwa ajili ya kuziba/kufunika pale juu kwenye uwazi na vipande vya chuma
kutengeneza miguu unaweza kutengeneza meza nzuri sana kwa ajili ya bustanini na
hata ndani au kwenye varanda.
Kama
una watoto wadogo au wajukuu nyumbani, unajua ni kiasi gani vifaa vya michezo
ya nje ya nyumba vinavyoweza kuwa gharama kubwa. Badala ya kutumia hela nyingi
kununua michezo unaweza kutumia matairi kadhaa na kuyapaka rangi (ambapo watoto
huzipenda sana rangi hizi) na kuyafunga pamoja kwa bolti kwa ajili ya usalama
ambapo unawatengenezea ngazi ya kuchezea na kupandia kwenye miti
Badala
ya kuacha mpira wa kumwagilia bustanini ukiwa peupe bila kukunjwa huku
ukichomwa na jua kila siku kiasi kwamba unakuwa mgumu na kukatika mapema, tumia
tairi chakavu kwa ajili ya kuuhifadhi mle kwa kuuzungushia. Tairi hilo
likipakwa rangi linakuwa na faida mbili ambazo ni pambo na matumizi.
Unaweza
ukageuza matairi chakavu yasiyotumika tena kuwa mabembea. Watoto wako wadogo
watayafurahia na utakuwa umewatengenezea michezo kwa gharama nafuu. Fundi anakufanyia
kazi hii kwa kuongezea kamba au mnyororo kwenye tairi na kulining’iniza.
Namna
nyingine ya kupendezesha kwa matairi chakavu ni kwa kuyapaka rangi mbalimbali
na kuyatundika kwenye ukuta wa uzio. Vilevile tairi chakavu wakati
likipendezesha bustani, linaweza kutumika pia kama eneo la mbwa kulala.
No comments:
Post a Comment