Mmiliki wa Kunonze Bar auawa kwa kuchinjwa Dar
Mwili wake wasokomezwa ndani ya friji
Mstaafu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege aliyekuwa
akiishi Mbezi Makonde jijini Dar es Salaam, ameuawa kinyama kwa
kuchinjwa na mwili wake kushindiliwa kwenye friji (deep frizer)
sebuleni kwake.
Joseph Minja (66) mmiliki wa baa ya Kunonze iliyoko Mbezi Makonde
jijini, aliuawa baada ya watu wasiofahamika kumvamia nyumbani kwake
usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii, ‘kumchinja’na kumwingiza kwenye
friji licha ya miguu kubakia ikining’inia.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura,
alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kueleza kuwa Minja alikuwa
akiishi na kijana ambaye jina lake halikufahamika.
Kwa mujibu wa Wambura, hakuna anayeshikiliwa na polisi na kwamba uchunguzi unaendelea.
Habari zilizopatikana kutoka nyumbani kwa Minja zilisema kuwa,
msaidizi wake pamoja na mtoto wa kiume ambaye wanaishi pamoja
hawajulikani walipo.
Mmoja wa majirani waliokuwa kwenye
msiba huo jana (jina linahifadhiwa), alisema Minja alikuwa mtumishi
mstaafu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege . Alieleza kuwa mwili wake
ulibainika siku ya pili baada ya tukio hilo.
Alisema baada ya watu hao wasiofahamika kumuua mzee huyo, Jumanne
katika hali isiyo ya kawaida, mmoja wa majirani alipokea simu kutoka kwa
mfanyakazi wa baa ya Kunonze iliyopo karibu na nyumba ya Minja akimpa
ujumbe’ kuwa, “jana usiku walivamiwa na majambazi nyumbani lakini
alifanikiwa kutoroka baada ya kukatwa panga la mkono.”
Alisema kijana huyo alimweleza jirani huyo kuwa, amepigiwa simu na mfanyakazi wa kazi wa mzee huyo.
“Kijana huyu wa baa alimweleza jirani huyo kuwa, mwenzake
amemuomba ampigie simu ili aende nyumbani kwa Minja kuangalia hali ya
mzee inaendeleaje baada ya tukio hilo,” alisema.
Aliongeza kuwa, baada ya kupata taarifa hizo, alikwenda kwa Minja
na kukuta mazingira yasiyo ya kawaida pamoja taa zikiwa zimezimwa akaona
asichukue hatua kabla ya kuwaarifu majirani.
Baada ya kufika hapo, walichungulia dirishani na kuuona mguu wa mtu ukining’inia kwenye friji.
“Tuliwataarifu polisi na walipofika walikuta mwili wa Minja kwenye friji uliokuwa umeganda,” alisema.
Jirani mwingine alieleza kuwa pembeni
ya mlango wa kuingilia ndani kulikuwa na bomba la sindano lililotumika.
“Yaelekea watu hawa baada ya kumuua mzee Minja walikuwa wanajaribu
kila njia ya kuuficha mwili wake, wamechimba hapa kwenye karo lakini
bahati nzuri hii imesakafiwa kwa hiyo nahisi walivyoona zoezi ni gumu
wakaamua kuuweka mwili wake kwenye friji,” alisema.
Jirani mwingine alisema kuwa, ndani ya nyumba katika meza ya chakula kulikutwa vyakula ambavyo ni wali, mbogamboga na kuku.
“Watu hawa yaelekea baada ya kula ndipo walipofanya mauaji haya ya
kutisha na ya aina yake, wamemuondolea uhai mzee wetu kwa kifo cha
kinyama na kikatili,” alisema na kuongeza:
“Vijana hawa waliokuwa wanakaa na kufanya kazi kwake, wanatakiwa
kutafutwa wanaweza kuhusika kwa namna moja ama nyingine, kwa nini
wamekimbia wote, sio wa baa wala wa nyumbani, hapa kuna kitu,” alisema.
Chanzo: Nipashe
No comments:
Post a Comment