MTUHUMIWA Tissi Mallya ambaye
alitoroka baada ya kumuua polisi, G.7168 Koplo Joseph Swai, ameauwa usiku wa
kuamkia jana na wananchi alipokuwa amejificha akiwa na panga lenye damu
lililotumika kwenye mauaji hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma
kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David
Misime alisema hayo jana
katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Kamanda Misime alisema baada ya
Malya kutekeleza mauaji hayo alikimbia lakini ilipofika saa 5.00 usiku wananchi
walimuona maeneo ya Mtimkavu Mailimbili akiwa bado na panga alilotumia kumuua
Koplo Joseph.
“Wananchi walichukua sheria mkononi
na kumshambulia hadi polisi walipofika eneo la tukio wakamchukua na kumkimbiza
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma lakini aligundulika tayari
amekwisha kufariki dunia,” alisema.
Kamanda Misime alisema katika
kumbukumbu zilizopo, mwaka 2006 Mallya aliwahi kufungwa miaka mitatu kwa
kujeruhi, pia mwaka 2009 alifungwa miezi sita kwa kutishia kuua.
Nawapongeza wananchi walioonyesha
kuchukizwa na kitendo alichotendewa askari wetu lakini waache kujichukulia
sheria mkononi,” alisema.
Pia alitoa wito kwa wananchi
kuchukua hatua kurekebisha maadili kuanzia ngazi ya familia kwa sababu
imebainika mtuhumiwa alikuwa mvuta bangi kiasi kwamba alikuwa anafanya vitendo
ambavyo ni kinyume na maadili ya jamii.
Diwani wa Kata ya Mnadani, Steven
Masangia, alisema alimfahamu polisi aliyeuawa kama kijana mchapakazi ambaye
alijitolea kutoa elimu hata kwenye mitaa juu ya ulinzi shirikishi.
“Alipokuwaa Mnadani alipambana
kuhakikisha uhalifu unakomeshwa na hata vijana wanaovuta bangi
aliwasambaratisha, na alikuwa akifundisha polisi jamii kwenye mitaa ya kata,”
alisema na kuongeza:
“Alikuwa na cheo kidogo lakini kazi
alizokuwa akifanya zilikuwa ni kubwa ikilinganishwa na cheo na umri wake”
alisema .
Katika mkasa huo uliotokea juzi
asubuhi, askari huyo aliitikia wito wa kuwapo kwa dalili za tendo la jinai
nyumbani kwa mkazi mmoja wa Chang’ombe Juu.
Alipofika nyumbani kwa mkazi huyo
ndipo mkasa huo ulipomtokea alipotaka kumuokoa mtoto mchanga ambaye alikuwa
auawe na baba yake kwa panga.
No comments:
Post a Comment