Kitanda
kilichokamilika kwa ajili ya kupanda na kulala kina muunganiko wa matandiko
mengi. Nimehojiana na Mary Masho, mwanadada mwenye fani ya utunzaji wa nyumba
na hapa anaainisha aina ya matandiko yanayokamilisha
kitanda na namna ya kuyatunza. Twende pamoja tuelimike kama ifuatavyo.
1. Mito
Mafuta na uchafu kutoka kwenye nywele
na nyuso zetu zinazama
hadi kwenye sponji zilizo ndani ya mto uliolalia. Kama
hutumii kofia au kitambaa kichwani cha kuzuia uchafu huu usizame kwenye mto
basi unatakiwa uwe unaufua japo mara moja kila mwezi au kila baada ya miezi
miwili. Kama unakinga mafuta ya nywele yasiingie kwenye mto wako basi unahitaji
kuufua angalau mara mbili kwa mwaka. Foronya zinatakiwa kufuliwa japo mara moja
kila baada ya majuma mawili. Mito inafaa zaidi kufuliwa kwenye mashine za
kufulia, na sio lazima uwe nayo nyumbani unaweza kupeleka kwenye vituo vya
kufulia.
2. Shuka
Kipindi unachotakiwa kufua shuka
baada ya kuzilalia mara nyingi kinategemeana na uamuzi binafsi. Wapo wanaopenda
kufua shuka zao japo mara moja kila juma. Wanapenda ule muonekano wa shuka safi
na huwa wanaweka kitanda kwenye muonekano huo kila juma. Shuka zinapokea mafuta
na uchafu kutoka kwenye miili yetu ambapo inaweza kupelekea madoa makubwa.
Hakikisha unakagua na kushughulikia madoa yoyote kwenye shuka zako kila
unapozifua. Pia epuka kufua shuka kwenye maji ya moto kwani zinaweza kusinyaa.
Unaweza usigundue kusinyaa huko hadi pale unapotaka kuzitandika tena. Maji ya
uvuguvugu ndio yanafaa.
3. Blanketi
Kujua ni kila baada ya muda gani
ufue blanketi lako, unatakiwa ujue matumizi yake yakoje. Kama una blanketi la
kupambia kitanda tu na wala halikunjuliwi na kutumika, basi kulifua kila baada
ya miezi kadhaa itakuwa sahihi. Ila kama blanketi linatumika kila unapolala
inaweza ikakubidi kuliweka kwenye ratiba ya kulifua kila baada ya majuma matatu
hadi mwezi. Kuwa makini kufuata maelekezo ya utunzaji kwenye lebo kama yapo.
Mara nyingi blanketi linatoa vimanyoya au pia kuchuja. Hakikisha unalifua bila
kuchanganya na nguo nyingine.
4. Komfota na duveti
Wengi wanatumia komfota na duveti
kama tandikio la juu la kupendezesha kitanda. Kwahivyo haya si hasa kwa ajili
ya kujifunikia. Kama ndivyo kwa upande wako na kama halijamwagikiwa chochote
huna haja ya kulifua zaidi ya mara moja au mbili kwa mwaka. Mengi ya makomfota
na maduveti yanatakikana kufuliwa kwenye mashine kwani kwanza ni makubwa
kufikicha kwa mikono na pia si rahisi kuyakamua badala yake yatachukua muda sana
kukauka na pengine kupelekea kuvunda ama kukata kamba za kuanikia kwa uzito wa
maji yake.
5. Foronya za godoro
Kuvalisha godoro foronya ni njia
nzuri sana ya kuongeza uhai wa godoro lako. Foronya ya godoro inasaidia kuzuia
uharibifu wa godoro, mzio na pia kuweka godoro safi na nadhifu. Foronya za godoro
zinapaswa kuvuliwa na kufuliwa angalau mara moja kila mwezi. Endapo doa lolote
limetokea unapaswa kulishughulikia papo hapo bila kujali ratiba ya ufuaji.
6. Urembo wa fremu ya kitanda
Urembo wa fremu ya kitanda ambao pia
unajulikana kama sketi ya kitanda mara nyingi huwa ni kwa ajili ya
kukipendezesha na sio kwa kutumika. Huwa hauchafuki ila kama una mzio (allergy)
unaweza kuhitajika kuufua japo mara 2-3 kwa mwezi. Kumbuka kuzingatia aina ya
kitambaa kilichotengenezea urembo huo ili ufue kwa uangalifu. Sketi za
kitanda nyingi zinatengenezwa kwa
vitambaa vyepesi.
Kwa ushauri 0755 200023
No comments:
Post a Comment