Tuesday, July 19, 2016

Zulia la kutupia kwenye corridor linavyoweza kupendezesha ndani


Kazi ya kupendezesha nyumba huwa haina kikomo na ni moja kati ya shughuli inayomfurahisha mwenye nyumba kwani inampa nafasi ya kuweka upendo wake ndani ya nyumba yake kwenye vitu anavyovipenda.
Mara nyingi wengi wanakuwa wanaangalia mambo ya rangi, fenicha, sanaa na vitupio kadha wa kadha lakini wanasahau corridor. Corridor hapa namaanisha ile njia iliyo ndani ya
nyumba inayokuelekeza kuingia katika vyumba mbalimbali. Kuendana na muundo wa nyumba, njia hizi zinaweza kuwa zaidi ya moja.

Moja ya njia kuu ya kupendezesha njia za ndani ya nyumba ni kutupia kizulia cha kwenye corridor. Uwepo wa vizulia mbalimbali vya kutandika kwenye corridor kwa ukubwa na mitindo tofauti unafanya muonekano wake kuwa wa kuvutia. Bila kujali mtindo utakaochagua, mazulia haya ni ongezeko muhimu kwenye corridor ya nyumba yoyote ile.

Hapa nakueleza kuhusu kutupia zulia hilo na jinsi linavyoweza kupendezesha nyumba yako kwa jinsi ya kipekee.
Kwanza kabisa kumbuka kuwa mazulia haya yanaipa corridor vipimo vingine. Maana yake ni kwamba corridor ambayo haina zulia ina muonekano mmoja mwanzo hadi mwisho. Muonekano huo unaweza kuwa ni wa marumaru, tazaro, mbao au hata zulia la kufunika kotekote. Kumbuka wakati wa kupendezesha nyumba, watu wanafikiria zaidi mionekano ya sebule, vyumbani, jiko na bafuni huku wakizisahau kabisa njia.

Ikumbukwe kuwa kwenye corridor mara nyingi ndipo eneo la mwanzo la kuweka mguu pale unapoingia ndani ya jengo. Hili ni eneo la kupamba kwa uangalifu ili kuleta matokeo makubwa.
Pia inaonekana kuwa corridor nyingi ni ndefu na nyembamba ikimaanisha kuwa ni ngumu kuweka fenicha au mapambo mengine yoyote makubwa. Zulia la kwenye corridor pamoja na picha au michoro ya ukutani, huwa ndivyo chaguo sahihi la kuongeza staili na mvuto kwenye eneo hili ngumu na linalosahaulika kupendezeshwa.

Mbali na kupendezesha, zulia la kwenye corridor lina faida  ya kusaidia kufanya sakafu ya eneo hili linalokanyagwa zaidi idumu. Maana kuweka zulia ni kwamba unafunika ile sakafu aidha ya marumaru au mbao kwa mfano, ambapo bila hivyo ingekanyagwa moja kwa moja na kupelekea kuichakaza na kubadilika rangi ukilinganisha na maeneo mengine.

Pia ni rahisi kubadilisha zulia likichakaa kwa haraka na rahisi kuliko kubadilisha sakafu ya kudumu. Na mazulia ya kwenye corridor huwa ni madogo na membamba, kwahivyo ni rahisi kubeba na kwenda kulifua mwenyewe au hata kupeleka kituo cha kufulia.

Baada ya kusema haya yote, hakikisha kuwa unachagua zulia lenye vipimo sahihi kuendana na upana na urefu wa corridor unayotaka kuliweka. Pia chagua rangi na michoro unayopenda bila kusahau uimara. Endapo utafanya hivi utagundua kuwa umebadilisha kabisa muonekano wa njia za ndani ya nyumba yako kwa namna ya kipekee.


Kwa ushauri 0755 200023

No comments:

Post a Comment