Sunday, July 10, 2016

Namna ya kutumia maji kwa uangalifu bafuni


Kuna msemo unasema kuwa maji ni uhai, bila maji sisi na vyote vilivyomo kwenye sayari dunia visingeweza kuwepo.

Ukishakuwa umelijua hilo basi ni vyema kufahamu namna na mbinu za kutumia maji kwa uangalifu ndani ya mabafu ya
nyumba zetu kama ifuatavyo. Twende pamoja!

Kwenye eneo la kuogea
Tumia bafu la bomba la mvua badala ya
lile la sinki la kuogea. Bomba la mvua lenye mzunguko mdogo linatumia maji kidogo kuliko lile lenye mzunguko mpana, anasema Bwana Fauzi Ali ambaye ni mtaalamu wa bomba. Unajua siri ni nini? Msukumo, eneo linapokuwa dogo msukumo unakuwa mkubwa. Wekeza kwenye bomba la mvua lenye kichwa kidogo.

Vilevile uwapo bafuni epuka kuoga muda mrefu na pia huna haja ya kuosha nywele kila siku.

Kwenye sinki
Ili uweze kutumia maji kwa uangalifu, uwapo kwenye sinki unasafisha meno hakikisha wakati unaposugua maji hayako wazi. Loanisha mswaki wako, funga maji, sugua meno halafu ndipo fungua tena maji kwa ajili ya kusuuza mdomo na kusafirisha uchafu uliotema. Kwa ajili tunatumia angalau dakika 3 kusafisha meno yetu utagundua kuwa wale wanaoacha bomba wazi wakati wakisugua meno wanapoteza lita kadhaa za maji bila sababu ya msingi.

Wakati huohuo ziba sehemu yoyote inayovujisha maji, hata iwe ni tone moja kwani mwisho wa siku maji yanayopotea ni ndoo itakuwa imejaa tayari.

Kwenye bakuli la choo
Vyooni ni moja ya maeneo yanayotumia maji mengi zaidi ndani ya nyumba. Choo cha kukaa kinakadiriwa kutumia hadi lita 20 za maji kwa wakati mmoja. Na hapo kumbuka kinatumika si chini ya mara tano kwa siku.

Unachoweza kufanya kama kweli umedhamiria kutumia maji kwa uangalifu, wekeza kwenye vyoo vya maji kidogo, anasema mtaalam Fauzi. Teknolojia imewezesha kuwepo kwa vyoo vya kisasa ambavyo vinatumia maji kidogo huku vikichanganyika na msukumo mkubwa na upepo na kuweza kuflashi uchafu wote bila kuacha alama.

Mara zote cheki kuhakikisha kuwa hakuna maji yanayochuruzika kidogokidogo kuingia ndani ya choo. Wakati mwingine huwa yanachuruzika kidogo sana kiasi kwamba ni ngumu kugundua kama hauko makini

Tunapoweza kuwa na mbinu za kutuwezesha kutumia maji kwa uangalifu ni ushindi kwetu sote.
Ushindi ni haraka na mara moja kwani utapunguza gharama za bili ya maji au hata kama chanzo chako cha maji sio cha bili (labda umechimba kisima binafsi) ni kwamba utakua umeokoa gharama ya umeme wa kusukuma pampu ya kuzalisha maji.
Vingine kwenye sayari yetu navyo vinashinda kwani kwa wewe kutumia maji kwa ungalifu umeweza kufanya misitu na wanyama kuneemeka. Binadamu wenzako nao wanashinda kwa ajili hawawezi kuishi bila maji. Maji yanaweza kuwa ni mengi kwako ila kwa wengine ni janga!


Kwa ushauri wa namna ya kupamba, panga na kupendezesha nyumbani kwako tuwasiliane 0755200023

No comments:

Post a Comment