Kuna njia ambazo unaweza kufuata ili kufufua muonekano
wa ndani ya nyumba yako bila kuhusisha kazi kubwa na wala gharama kubwa. Mara
nyingi, kuongeza au kubadilisha tu vitu vichache inatosha kabisa kuleta upya na
mvuto. Zaidi ya mvuto na upya, pia inanyanyua nafsi za wanafamilia wanaoishi
humo. Hata hivyo kwa matengenezo na maboresho makubwa, mwenye nyumba anatakiwa
kukaa atulie ili ajue gharama na
matokeo anayotaka. Njia ninazokupa kwenye
makala hii ni za haraka bila kufikirifikiri sana.
Siku hizi kubadili muonekano kwa haraka na bei nafuu
imerahisishwa sana kutokana na wauzaji na wabunifu wengi wa mapambo ya ndani kuwepo kwenye mitandao mbalimbali wakionyesha kazi
na bidhaa zao. Hii imesaidia kutoa nafasi kwa anayetaka kupendezesha nyumba
yake kuona vitu na njia mbalimbali anazoweza kupitia na hivyo kufanya uamuzi
haraka.
Kuna njia za kupendezesha ndani kwa kutumia mapambo ya
gharama nafuu lakini kwa ubunifu. Tutaangalia kwa haraka njia 4 ambazo unaweza
kutumia ili kuifanya nyumba yako iwe tamu tena na ya kuvutia.
Tumia vitu vyenye rangi na michoro iliyokolea
Kuna maeneo mengi ndani ya nyumba unayoweza kutumia
vitu vyenye rangi zilizokolea ambavyo wala si vya gharama kivile. Vitu vyenye
rangi kama nyekundu, chungwa na zilizopishana kama za pundamilia ni kati ya
rangi zilizokolea. Kwa mfano zulia la rangi zilizokolea, kitambaa cha viti vya
meza ya chakula na kiti kingine chochote, mito, shuka na picha za ukutani. Ni
rahisi sana kununua vitu vyenye rangi na michoro iliyokolea na kubadilisha
kabisa muonekano wa eneo fulani ndani ya nyumba. Rangi zilizokolea zina kawaida
ya kuleta hisia za nguvu.
Pachika vioo
Ingawa ni nyumba chache ambazo wenyewe wameweka vioo
vya mapambo, ni vyema wengi tufahamu kuwa vioo vya kwa lengo la mapambo
vinapendeza sana pale vinapopachikwa kwenye maeneo kama mwisho wa corridor,
chumba cha chakula na sehemu yoyote ndogo au kubwa. Vioo vina tabia ya
kumchanganya mgeni kuhusu uelekeo wa nyumba kwa hivyo anachukua muda kutafakari
mtindo na muundo wa nyumba yako. Zaidi ya hiyo pia vinafanya sehemu ndogo
ionekane kubwa. Tafuta kona ambayo ni nzuri kupamba kwa kioo halafu mtafute
fundi akipachike hapo kwa ukubwa na fremu unayotaka.
Weka taa za mitindo mbalimbali
Taa zinaweza kuonekana tu kama kitu rahisi lakini
zinachukua nafasi kubwa kwenye kufufua muonekano wa ndani. Zipo taa maalum kwa ajili
ya vyumba vya kulala, sebuleni, jikoni na kwenye varanda. Taa popote pale ilipo
iwe ni ya muundo wa kuweka sakafuni, mezani, darini, ukutani inaleta mvuto.
Badili pazia
Pazia mpya ni njia iliyozoeleka na wengi na pia ni
rahisi mno kwa kubadilisha muonekano wa ndani kwa haraka. Pazia ndefu zenye
rangi na michoro maridadi hakuna ubishi kuwa zinafufua muonekano wa chumba chochote
kile. Kwenye ulimwengu za sasa wa mitandao pazia za kila aina na rangi zimeshamiri
madukani na mitandaoni na hii inamsaidia nafuu mno mnunuzi kupata mawazo au
hata ushauri akitaka ya zipi zitamfaa kwa chumba kipi na cha mwanafamilia wa
jinsia gani, kazi inayobaki ni yake kufanya uamuzi.
Kutokana na njia hizi 4 bila shaka unaweza kufufua
muonekano wa nyumba yako kwa haraka mno, kwa gharama nafuu na bila usumbufu
mkubwa wa kuhamisha vitu au watu. Kila mmoja anapenda kuishi ndani ya nyumba
nadhifu, badilisha nyumba yako iwe ya kipekee kwa kutumia ubunifu ya njia hizi
za gharama nafuu na haraka.
Kwa ushauri piga 0755 200023
No comments:
Post a Comment