Kujua
ni lini nguo ya mwanamke ifuliwe inategemea aina ya nguo, anasema Bi Winnie
Mamkwe ambaye ni mfuaji kwenye kituo cha kufulia nguo. Anaendelea kutujuza kuwa
baadhi ya nguo zinaweza kuvaliwa mara kadhaa wakati nyingine zinatakiwa kufuliwa
kila baada ya kuvaliwa mara moja. Tujielimishe kuhusu ufuaji nguo za wanawake
kuanzia za ndani hadi
ofsini, ili kuzifanya zionekane mpya na za kuvutia wakati
wote.
Nguo za ndani
Hizi ni pamoja na sidiria, chupi na
zile za kubana tumbo/kutengeneza shepu. Kama hutoki jasho sana aidha kutokana
na maumbile au hali ya hewa ya maeneo unayoishi na ulipo muda mwingi, sidiria inaweza
kuvaliwa mara 3 hadi 4 kabla ya kufuliwa. Ila inahitaji kuachwa kwa masaa 24
bila kuvaliwa mara ya pili ili kuruhusu mipira kujirudi vizuri.
Endapo mazingira ni ya jasho, ifue kila baada ya
kuivaa mara moja. Namna unavyotunza sidiria zako ndivyo unapovaa inakupa muonekano
wa ujana.
Ufuaji wa nguo za kutengeneza shepu
unakaribia wa sidiria kwani zote zinavaliwa kugusana na ngozi, zinahitaji
ufuaji wa mara kwa mara lakini bila kusahau umakini ili kufanya mipira ibaki imara.
Chupi inatakiwa kufuliwa kila baada ya kuivaa.
Fulana na jeans
Fulana ni nguo ambayo inakamata
mwili na haipishani sana na zile za ndani. Inanyonya jasho na mafuta yanayotoka
mwilini na ndio maana nayo inapaswa kufuliwa kila baada ya
kuvaliwa mara moja. Unapofua fulana
nyeupe usisahau makwapani ambapo uchafu ukiachwa unaweza kutengeneza rangi ya
njano.
Jeans ni nzuri kuficha uchafu na
madoa. Kama ni ya kushika mwili unaweza kuifua baada ya kuvaliwa mara 4 hata
kama bado inaonekana safi. Kuepuka kupauka, fua na anika ukiwa umeigeuza nje
kuwa ndani.
Blauzi
Blauzi inatakiwa kufuliwa baada ya
kuvaliwa mara moja. Ila kama hutoi jasho sana au unaivaa tu masaa machache
unaweza kuivaa tena kabla hujaifua. Epuka kuzidisha vipodozi vya makwapani
kwani vinaweza kusababisha nguo kuchuja eneo hilo au kutengeneza doa.
Mavazi ya ofsini
Kama mavazi yako ya ofsini unayavaa
katika ofisi ambayo ina viyoyozi, unaweza kuyavaa mara 2 hadi 3 kabla ya
kuyafua, laa iwe umedondoshea lanchi mapajani kwa bahati mbaya. Mara zote
tundika magauni, suruali au makoti ambayo umevaa kwa masaa 24 kabla ya kuvaa
tena. Kwa mfano unaweza kuvaa gauni lako ofsini jumatatu halafu ukaliacha
umelitundika na ukalivaa tena alhamisi. Kama utaona kuna umuhimu wa kupitisha
pasi juu juu kuondoa mikunjo fulani basi fanya hivyo.
Makoti yanaweza kuvaliwa hata mara 4
kabla ya kufuliwa. Kuwa makini kuangalia maeneo yanaoonyesha uchafu kirahisi
kama vile kwenye kola, mikononi na kwenye viwiko ili uwe na uhakika ni kusafi.
Yaachie muda ya kupumua usivae mfululizo. Koti na suruali zinazofanana zifuliwe
pamoja ili kuepuka moja kuchuja na mwenzake kubaki mpya.
Sweta
Sweta inayovaliwa juu ya nguo nyingine,
unaweza kuivaa hadi mara 5 kabla ya kuifua. Ila kama unaivaa yenyewe na
inagusana na mwili moja kwa moja, vaa mara moja au mbili tu baada ya hapo ifue.
Nguo za kulalia
Naamini unafahamu kuwa watu wote
wanatokwa na jasho usiku. Fua pajama au nguo nyingine unayovaa wakati wa kulala
kila baada ya kuivaa mara mbili hadi tatu. Kama unaoga muda ule kabla tu
hujaingia kulala unaweza ukaivaa muda mrefu zaidi.
Nguo za mazoezi
Unapaswa kufua nguo zako za mazoezi
kila baada ya kuzivaa mara moja. Unatokwa na jasho jingi na pia nguo hizi zinashika
mwili kwahivyo ni rahisi kutoa harufu mbaya na pia kuhifadhi vijidudu.
No comments:
Post a Comment