Jinsi ya kuchagua
uzio sahihi wa nyumba yako kwa bajeti yako
Uzio ni moja ya sura au tuseme kipengele cha makazi ambacho
kinaweza kuwa kwa ajili ya kazi na pia kwa ajili ya urembo kwa jinsi ambavyo
unataka kiwe. Kutegemea na bajeti yako, ubunifu, hitaji la ulinzi na pia ladha
yako binafsi kuna aina nyingi za uzio kwa ajili yako kuchagua. Hapa ni baadhi
ya dondoo zangu ninazoamini zitakuwezesha kupata uzio utakaokufaa.
Kwa ujumla walau kila nyumba inawezekana kuzungushiwa uzio, iwe ni kwa ajili
ya ulinzi, usalama, faragha au muonekano. Uzio ulio imara unaongeza pia thamani
ya mali
yako hiyo.
Ili mpango wako wa kuweka uzio ufanikiwe na
bila kujutia hela yako jiulize mambo yafuatayo kabla ya kuweka uzio wako:
Jambo la kwanza kabisa jiulize ni nini nia yako ya kuweka huo uzio. Je unataka
kujiweka mbali na macho ya majirani wapelelezi? Kuzuia mbwa wako wasitoroke
unapowafungulia? Au ni kwa ajili tu ya kuongeza urembo wa makazi yako? Kwa
hivyo kabla hujaamua kuchagua mtindo au vifaa vya kutengenezea uzio wako hakikisha
umejua kuwa lengo lako la kuweka uzio ni nini. Hapana shaka kuwa wewe msomaji
wangu umeshawahi na bado unaona uzio zilizowekwa zikaacha maeneo ya wazi ambayo
baadaye wenyeji wameamua kuyaziba ama kwa makuti au kwa bati.
Jambo la pili la kufikiria ni utunzaji wa uzio wako. Aina ya uzio utakayochagua
itasema ni gharama kiasi gani ya utunzaji wake uko tayari kuitumia. Kwa mfano
uzio wa mbao unatakiwa kupakwa rangi mara kwa mara na pia mbao zinaoza baada ya
wakati kwa hivyo zinahitaji maboresho ya muda mfupi mfupi. Wakati huo huo uzio
za wavu (chain-link) hauna gharama kubwa kwenye utunzaji kwani nguzo zake ni za
zege na zile chuma hazipati kutu lakini huenda usikupe faragha sahihi. Orodheha
gharama ya vifaa mbali mbali na linganisha bajeti yako na hitaji lako ili
kupata uzio sahihi.
Jambo la tatu la kuzingatia kabla ya kuweka uzion ni muundo au mtindo wa uzio
wenyewe. Kwa kuwa imeonekana watu wengi wanaendeleza sehemu za nje ya nyumba
zao kwa shunguli nyingi za maisha ya kila siku kwa (mfano makala iliyopita
tulizungumzia watu kuwa na eneo la kukaa kwenye bustani), muonekano wa uzio
umekuwa ni jambo la kuzingatia kuliko ilivyowahi kuwa. Lango kuu na taa nazo zinaboresha
muonekano huu. Na kwa kupunguza gharama labla au hata kupata hewa safi unaweza ukaweka uzio wa
aina fulani eneo la mbele
na aina nyingine
eneo la nyuma. Kwa mfano, nimeona baadhi ya watu walioweka uzio wa gharama
kubwa eneo la mbele ya nyumba na upande wa uani wakaweka uzio wa
chain-link ikishirikiana na miti ya uzio aina ya michongoma.
Hii itategemea ni kwa jinsi gani uzio wako wa eneo hilo utakavyoweza kukubaliana na lengo na
bajeti yako.
Jambo la nne ni kuhusu
faragha na ulinzi. Jua ni nini uzio wako utaruhusu uweze kuacha nje ya nyumba
na ni nini lazima kiingizwe ndani. Uzio
unaoacha nafasi nafasi au matundu matundu hauna faragha na wala hauwezi kukulinda
vya kutosha, ila unakupa starehe ya kuangalia kinachoendelea nje ya makazi yako
unapokuwa umejipumzisha bustanini.
Baada ya kuweka akili sawa
kwa hayo mambo manne ya kuzingatia, anza kufanya utafiti wako wa aina za uzio
zilizopo. Kwa mazingira yetu ya Kitanzania zipo uzio za aina mbali mbali kama vile tofali, mbao, miti, makuti, chuma, aluminiam, wavu,
bati, PVC na kadhalika. Karibia kila aina ya uzio ina faida na hasara zake linapokuja
swala la bei, utunzaji, umaridadi na lengo lake. Fikia ni uzio upi ungependa
kuweka na tembelea masoko si chini ya matatu ili ulinganishe gharama kabla ya
kufanya uamuzi wa mwisho.
Sasa umeshafanya utafiti
wako wote na uko tayari kuanza kujengea uzio wako. Jambo la mwisho lakini sio
dogo ni juu ya ujirani mwema. Kabla hujaweka uzio wako cheki na majirani
kuhakikisha kuwa uzio unaoamua kuweka hautaleta usumbufu kwao. Kwa mfano, uzio
wa miti itayooteshwa karibia kabisa na nyumba ya jirani huenda ikaleta mgogoro.
Na pia kuna uzio ule ambao vibati vinawekwa juu tuseme uzio ni wa ukuta na una
marembo yake, wenye nyumba wengine wanapendelea kuweka vibati vya plastiki kwa
juu ili ukuta usiloe ukaoza. Maji ya mvua kwenye hivi vibati kama
yameelekezwa kumwagika kwa jirani inaweza ikaleta kero. Jua mipaka yako kwa
kukumbuka kuwa uzio usiloleta kero kwa jirani unafanya ujirani mwema, kuwa
jirani mzuri kwa kuweka uzio ambao hautamkera jirani yako.
Zaidi ya yote fahamu sheria
za mipango miji juu ya kujenga uzio. Kwa mfano uzio wa tofali wa urefu fulani
hauruhusiwi kwenye makazi.
Sio siri
kuwa kuchagua uzio kwa ajili ya nyumba yako inaweza kuwa uzoefu mgumu. Kuwa na
dongoo hizi kichwani, pamoja na bajeti yako na kipaumbele cha staili itakuhakikisha
kuchagua uzio sahihi kwa ajili ya nyumba na familia yako.
Makala
hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa
magari, nguo na mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya
nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk