MLINZI wa usiku katika Ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Florence Kazonde (35)
amejinyonga baada ya kumuua kikatili kwa kumkaba koo mkewe aliyekuwa na
ujauzito wa miezi tisa, Emilia Mzui (30).
Chanzo cha mauaji hayo kimeelezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Tukio hilo limethibitishwa na Jeshi la Polisi mkoani Rukwa, majirani na ndugu
wa karibu wa familia ya marehemu hao waliokuwa wanaishi katika Kitongoji cha
Namlangwa mjini Matai yalipo makao makuu ya wilaya ya Kalambo.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Halmashauri hiyo, Ramadhan
Juma, alikiri kuwa Kazonde alikuwa mlinzi wa ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa
halmashauri hiyo zilizopo nje kidogo ya Mji wa Matai, lakini hakuwa mwajiriwa
wa halmashauri hiyo.
“Kazonde alikuwa anatoka katika kampuni moja ya
ulinzi…hakuajiriwa na Halmashauri hii,“ alisisitiza Juma. Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alieleza kutokuwa na taarifa za mkasa huo kwamba
akizipata atazitolea taarifa.
Hata hivyo taarifa kutoka Jeshi hilo la Polisi mkoani humo
limethibitisha kutokea kwa tukio hilo. “Kweli kuna hilo tukio limetokea
wilayani Kalambo … taarifa zipo tayari lakini kwa kuwa mie si msemaji wa Jeshi
hili siwezi kutoa maelezo zaidi ya kina lakini nikiri kuwa tukio hilo limetokea
…Kwa utaratibu wa Jeshi letu ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa ndiye msemaji na si
vinginevyo.
Baadhi ya majirani na ndugu wa karibu kwa masharti ya
kutoandikwa gazetini walieleza kuwa walibaini vifo hivyo baada ya kufika
nyumbani kwa wanandoa hao ili kuwasabahi lakini walikuta milango ya nyumba hiyo
imefungwa kwa ndani.
“..Tulihisi labda walikuwa bado wamelala lakini kila
tukibisha hodi ni watoto tu waliokuwa wakiitikia …… “Mazingira hayo yalitutia
mashaka makubwa tukahisi kuwa kwa kuwa mke wake siku zake za kujifungua
zilikuwa zimekaribia tuliamini kuwa walikuwa wamekwenda hospitali na kuwaacha
watoto wakiwa wamejifungia ndani na kushindwa kufungua milango hiyo, “ alisema
mtoa taarifa.
Ilielezwa kuwa ndugu na majirani hao waliamua kufungua mlango
kwa nguvu ili wawatoe watoto hao wadogo nje ambao walikuwa wawili.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa baada ya kufungua mlango wa nyumba
hiyo kwa nguvu mmoja wa watoto hao aliwaonesha ishara kuwa chumbani kwa wazazi
wao kuna kitu cha kutisha ndipo walipolazimika kuingia chumbani humo na kuona
mwili wa Kazonde ukiwa umening’inia darini ukiwa na kamba ya katani shingoni
ambapo mwili wa marehemu mkewe ulikuwa kitandani.
“Inatisha na kusikitisha sana ….tuligundua kuwa wote wawili
walikuwa wafu tukatoa taarifa mara moja katika Kituo cha Polisi hapa mjini
Matai …… askari Polisi walifika na waganga ambao walifanyia uchunguzi miili
hiyo na kuthibitisha kuwa Kazonde alikuwa amejinyonga baada ya kumuua mke wake
kikatili kwa kumkaba koo,” aliongeza mmoja wa ndugu wa karibu.
Taarifa kutoka eneo hilo la tukio zinaeleza kuwa kwa muda
mrefu wanandoa hao walikuwa wakigombana mara kwa mara ambapo mume alikuwa
akimtuhumu mkewe kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine na kwamba
kati ya watoto wao wawili mmoja sio wake ni wa mwanamume mwingine.
“Kazonde hivi karibuni alisikika akimtuhumu mkewe kuwa hata
ujauzito aliokuwa nao sio wa kwake (Kazonde ),” alieleza mtoaji taarifa .
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo hilo la tukio baada ya
uchunguzi huo wa kitabibu mwili wa mke wa Kazonde ulifanyiwa upasuaji na kumtoa
mtoto wa kiume akiwa amekufa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi mkoani
Rukwa baada ya upekuzi wa kina walikuta ujumbe wa maandishi unaosadikiwa
kuandikwa na Kazonde kwa kutumia wino wa bluu pia aliacha ujumbe wa maandishi
ukutani na sakafuni aliouandika kwa kutumia mkaa.
Ujumbe huo ulisomeka “Msijiulize sababu za vifo vyetu,
vimetokana na tabia ya mke wangu kufanya mapenzi na ndugu (Jina limehifadhiwa)
kwa kushirikiana na ndugu (jina limehifadhiwa).”
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment