Wednesday, July 8, 2015

Wakati vikao vya juu vya CCM vya kuchuja wagombea urais vikianza leo, hofu na wasiwasi umezidi


Wakati vikao vya juu vya CCM vya kuchuja wagombea urais vikianza leo, hofu na wasiwasi umezidi kutanda miongoni mwa wagombea, viongozi na wanachama wa chama hicho kuhusu namna ya kuikabili minyukano baina ya wagombea hao na kibarua cha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa miongoni mwa mambo yanayoleta hofu na kusababisha presha kuongezeka kila kukicha ni woga wa kufanya makosa katika uteuzi wa ndani, hali inayoweza kukigharimu chama hapo baadaye hasa kutokana na kuongezeka nguvu ya upinzani.

Kutokana na hali hiyo kumekuwa na shinikizo kutoka katika makundi mbalimbali ya chama hicho kuwa makini kumteua mgombea anayekubalika, msafi na mwenye kuchagulika ambaye atatoa ushindani kwa wagombea wa upinzani, hasa Ukawa.

Vilevile, kumekuwapo na wasiwasi wa baadhi ya wagombea kutishia kukihama chama hicho endapo majina yao yatakatwa, jambo ambalo pia linakiweka njia panda.

Nape: Hakuna shinikizo
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amejibu hoja hizo akisema chama hicho hakitafanya uamuzi kwa kushinikizwa na watu, bali kitafuata taratibu na kanuni.

“Tunazo taratibu, tunazo kanuni zetu. Nataka kuamini kuwa kila mtu aliyegombea anajua kuna kushinda na kuna kushindwa na kuna kuteuliwa na kutokuteuliwa,” alisema jana alipozungumza na waandishi wa habari.

Alisema hataki kuamini kuwa kuna mgombea kati ya 38 walioomba nafasi hiyo ambaye anaamini anaingia kushinda tu.
“Usipokuwa wewe anakuwa mwingine… Asiyekubali kushindwa basi atakuwa si mshindani. Usisahau hizo ni presha za wapambe hazitupi tabu. Tunachojua walioshindwa watapeana mkono na aliyeshinda na chama kitabaki kuwa kimoja,” alisema Nape.

Alisema wananchi waamini chama kitatenda haki, taratibu zitafuatwa na kuwapa mgombea bora.
“Haya ni maneno ya presha za barabarani ninachoamini mwisho wa siku hakuna fujo, hakuna vurugu, vyombo vimejipanga vizuri hakuna vurugu na wapambe kusindikizana ni jambo la kawaida,” alisema na kuongeza kuwa anafahamu kuwa wapo watakaohuzunika kutokana na majina ya watu wao kukatwa lakini hakuna jinsi kwa sababu kanuni za CCM zinasema Kamati Kuu (CC) itapendekeza majina matano kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Pia kanuni hizo zinasema NEC itapendekeza majina matatu kwa mkutano mkuu ambao utachagua mmoja.
“Hatuna ujanja, tungeweza kusema wote 38 nendeni lakini kanuni yetu haituruhusu.

Wengi wa wagombea wanajua, kwa sababu hawajaanza jana,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu kuondoka kwa wanachama ambao wagombea wao au wao wenyewe watakatwa katika mchujo huo, Nape alisema haoni mwanachama atakayeondoka ndani ya chama hicho… “Simuoni mtu atakayeondoka, hizi ni kelele za wapambe… Hii ni sehemu ya kutengeneza presha. Ninachotaka kusema, CCM hatumuoni mtu atakayeondoka na kwa nini aondoke?” alisema.

Haki ya kukata rufaa
Akizungumzia haki ya mgombea kukata rufaa iwapo jina lake litakatwa na asiridhike, Nape alisema kanuni ziko kimya hazisemi kuhusu suala hilo na wala hakuna muda wa kufanya hivyo.

“Katika uchujaji wa majina matano kwenda NEC, hawatoi sababu kwa nini wamelikata jina,” alisema na kufafanua kuwa hakuna kikao kinachokilazimisha kikao kingine kusema sababu ya kuyakata majina ya wagombea.

Alisema kuna watu walihoji kuhusu kukatwa kwa majina yao katika chaguzi kuu za mwaka 1995 na 2005, kwa kukata rufaa NEC lakini kesi ilichukua dakika tatu na kumalizika vibaya.
“Huwa nawaambia watu tusisahau kuwa hiki chama ndicho kiko madarakani, vyanzo vya taarifa zake haviwezi kuwa sawa na Chadema, CUF na wengine, haiwezekani,” alisema.

Hata hivyo, alisema hatarajii kama kuna mtu atakayekata rufaa katika mchujo huo, lakini haikatazwi kwa mwanachama kutoa hoja yake katika kikao chochote.

Mgombea anayeuzika
Baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar wameeleza hofu ya CCM kuanguka katika Uchaguzi wa Oktoba iwapo itashindwa kuteua mgombea anayekubalika ndani na nje ya chama hicho.

Mjumbe Khamis Mbeto Khamis alisema CCM ikishindwa kupata mgombea anayekubalika na wananchi na ndani ya chama ipo hatari ya kuandika historia mpya ya kupoteza dola kama ilivyotokea kwa vyama vilivyopingania ukombozi vya Malawi, Kenya na Zambia.

“Mie sitaki kuwa sehemu ya wajumbe watakaoandika historia ya CCM kuondoka madarakani katika kipindi cha uongozi wetu, tuache mizengwe, chuki na uhasama tupate mgombea bora,” alisema Khamisi.

Alisema mgombea ambaye hana msingi wa kisiasa, mvuto na kukubalika kwa wananchi wa pande mbili za Muungano ni hatari kumsimamisha kutokana na ushindani mkubwa wa kisiasa unaoendelea kujitokeza.

Mwenyekiti wa wenyeviti wa mikoa sita ya kichama ya CCM Zanzibar, Haji Juma Haji alisema CCM inatakiwa izingatie masilahi ya chama na Taifa kwa kusimamisha mgombea mwenye uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya kisiasa.

“Muhimu tuchague anayetakiwa na wananchi, awe anakubalika na mwenye uwezo wa kuendeleza amani na usalama wa Taifa letu,” alisema bila kumtaja mgombea huyo.

Mjumbe mwingine, naibu waziri wa zamani wa Muungano, Dk Maua Daftari aliwataka wajumbe wa vikao vya uteuzi wazingatie sifa 13 zilizowekwa na chama wakati wa kuwajadili wagombea ikiwamo ya kumpata mtu anayekubalika.

“Muhimu tusifanye hiana, tuwe wa kweli na tusiweke chuki katika kutafuta mgombea urais, mazingira ya kisiasa yamebadilika lazima tuangalie mbele na nyuma, sifa bora za uongozi 13 za chama uwe msingi wetu wa kupata mgombea,” alisema Dk Daftari.

Mjumbe mwingine, Rashid Ali Juma alisema CCM inapita katika wakati mgumu hivyo ni lazima apatikane mgombea anayekubalika kwa wananchi ndani ya chama.

Hofu ya wajumbe wa NEC inajitokeza wakati kesho wajumbe 123 wa Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar na wengine 213 wa Mkutano Mkuu wakianza safari kwenda Dodoma kuchagua mgombea urais wa Zanzibar na Muungano.

Ratiba ya vikao
Jana, kikao cha sekretarieti kilichoongozwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana kilikaa kikiwa na ajenda moja ya kupitia maandalizi ya mkutano mkuu ambayo ni pamoja na kuhakiki ratiba, malazi ya wajumbe, makabrasha na nyaraka mbalimbali zitakazotumika katika vikao hivyo.

Leo, kutakuwa na kikao cha Kamati ya Maadili na Usalama kitakachoendeshwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na kesho kutakuwa na ufunguzi ukumbi wa chama hicho na baadaye kikao cha Kamati Kuu (CC) kitakachoteua majina matano ya wanaowania urais.

Kikao cha NEC kitakaa Ijumaa kwa ajili ya kumdhibitisha mgombea wa urais wa Zanzibar, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya 2015 – 2020 na kupigia kura majina matano ambayo yatawasilishwa na CC kwa ajili ya kutoa majina matatu ya wagombea urais, ambayo yatakwenda katika Mkutano Mkuu utakaofanyika Jumamosi hadi Jumapili ambao utakuwa na ajenda mbili, kupitisha Ilani ya Uchaguzi na kupigia kura majina matatu yaliyopendekezwa na NEC kumpata mgombea urais.

“Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa tumejipanga vizuri, tutatoka tukiwa wamoja na ushindi,” alisema Nape na kuwahakikishia wajumbe kuwa hakuna atakayekosa malazi.

Ulinzi na usalama
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa aliwatahadharisha watu wanaojipanga kushiriki vitendo vya uvunjifu wa amani na utulivu kuwa watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

“Asiye mjumbe wa mikutano na wala siyo mwalikwa ni bora asije kabisa Dodoma. Sasa kama huna sehemu ya kufikia, hujaalikwa huna sababu ya kuja kutuletea vurugu,” alisema Galawa.

Shamrashamra
Katika uzio wa jengo la Makao Makuu ya CCM maarufu White House, wajasiriamali wamepanga bidhaa mbalimbali nyingi zikiwa ni sare za chama hicho.
Pia, idadi kubwa ya bendera za chama hicho zinapepea ndani ya uzio wa jengo hilo.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment