KIKAO Maalumu cha Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kimeanza jana Mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake Jakaya Kikwete, kwa
ajili ya kupitisha Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015.
Kikao hicho ni mwanzo wa vikao vinavyotarajiwa kuanza mapema
wiki ijayo, kwa ajili ya kuchuja majina ya walioomba kuteuliwa na chama hicho
kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya muda wa kurejesha fomu kwa wanaowania kuteuliwa
kugombea urais kumalizika, vikao mbalimbali vya uchujaji wa majina ya wagombea
vinatarajiwa kuanza vikitanguliwa na Kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili
kitakachokutana Julai 8, mwaka huu.
Kikao cha Kamati Kuu kinachotakiwa kujadili wagombea 38 na
kuja na majina yasiyozidi matano kinatarajiwa kukutana Julai 9.
Majina hayo yasiyozidi matano, yanatarajiwa kuwasilishwa
katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, ambayo itakutana Julai
10.
Kikao hicho cha NEC, kinatarajiwa kupitia majina hayo na kuja
na majina matatu, yatakayopelekwa katika Mkutano Mkuu wa CCM utakaofanyika
Julai 11 na Julai 12 utakaoteua jina moja la mgombea urais wa CCM, baada ya
kupigiwa kura na wajumbe wote wa mkutano huo.
CC maalumu Zanzibar
Wakati huo huo, Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) ya (CCM) Zanzibar, inatarajiwa kukutana kesho mjini Zanzibar kupendekeza
jina la mgombea wa urais Zanzibar kwa tiketi ya CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la Makao
Makuu ya CCM, White House Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Vuai Ally
Vuai, alisema kikao hicho maalumu kitafanyika katika ukumbi wa Ofisi Ndogo ya
chama hicho Kisiwandui Zanzibar.
Alisema mpaka sasa kuna mgombea mmoja ambaye ni Rais aliyepo
madarakani, Dk Ali Mohammed Shein, ambaye alichukua fomu na amesharudisha.
Kwa mujibu wa Vuai, Kamati hiyo itapendekeza jina
litakalopelekwa kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa na baadaye jina hilo
litaenda mbele ya kikao cha NEC kitakachofanya uamuzi wa mwisho.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 114 (b) Kamati hiyo pamoja na kazi
nyingine, ina kazi ya kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya Taifa, juu ya wanachama wanaoomba nafasi ya Rais wa
Zanzibar, ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar,” alisema Vuai.
Wajumbe wa Kamati hiyo Maalumu kwa mujibu wa Ibara ya 113, ni
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Rais wa
Zanzibar anayetokana na CCM na Makamu wa Rais wa Zanzibar anayetokana na CCM.
Wengine ni wajumbe wa Kamati Kuu ya NEC wanaotoka Zanzibar,
wenyeviti wa CCM wa mikoa ya Zanzibar, Makatibu wa CCM wa Mikoa ya Zanzibar na
wajumbe wote wa NEC Taifa wanaotoka Zanzibar.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment