- Mizengwe yatawala hadi usiku wa manane Kamati Kuu kufyeka waliodaiwa kuanza kampeni mapema.
Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imejikuta ikiwa
katika kibarua kizito cha kuteua watia nia watano kati ya 38 wa nafasi ya urais
mjini Dodoma jana usiku baada ya kuwapo kwa msuguano mkali juu ya watu wa
kuwaondoa kwa tuhuma za kuanza kampeni mapema.
Hali hiyo inaelezwa kwamba ndiyo kigezo ambacho wajumbe
wa Kamati Kuu waliokutana kwenye ofisi moja nyeti mjini Dodoma waliendelea
kuishikilia kwa lengo la kuwaondoa wagombea wenye dosari hizo.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, baadhi ya wajumbe walikuwa
kwenye mjadala mkali kutokana na hofu kuwa wakiteuliwa watia nia walioanza
kampeni mapema watakiweka chama chao katika hatari ya kuwa na mgombea
aliyepoteza sifa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi mkuu zinazosimamiwa na Tume
ya Taifa ya Uchaguzi.
Hadi kufikia mishale ya saa 7:31 usiku hakukuwa na
taarifa zozote za matokeo ya majina matano yaliyopitishwa na Kamati Kuu kati ya
38 ya waliorejesha fomu ili yapelekwe kwenye kikao cha Nec kwa mchujo zaidi ili
wabaki wanafainali watatu.
USIRI MKUBWA WATAWALA
Kama ilivyotarajiwa, kikao hicho cha Kamati Kuu,
kilifanyika kwa usiri mkubwa kiasi cha kuwafanya waandishi wa habari kuwa na
wakati mgumu kupata taarifa zilizokuwa zikiendelea ndani yake.
Awali kabla ya Kamati Kuu ya chama hicho kukutana kwa
kazi hiyo, siri nzito ilitenda juu ya maamuzi yaliyofanywa na kikao cha Kamati
ya Usalama na Maadili ya CCM kilichoketi juzi usiku chini ya Mwenyekiti wa CCM
Taifa, Rais Kikwete. Kikao hicho cha Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM,
kilikaa kupitia mafaili ya wagombea 38, waliorejesha fomu za kuomba kuteuliwa
na chama hicho kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika
uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kabla ya kikao cha Kamati Kuu, Katibu wa Halmashauri Kuu,
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alipotafutwa na NIPASHE jana kwa njia ya simu
kutoa ufafanuzi iwapo kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili kilifanyika kama
ilivyokuwa imepangwa awali, alisema: “Nianze na hili la Kamati Kuu (CC), mimi
pia sijui kinafanyika wapi na saa ngapi. Halafu hata hicho kikao cha Kamati ya
Usalama na Maadili unachoniuliza hapa; hakikufanyika.”
Kabla ya Rais Kikwete kuongoza Kikao cha Kamati Kuu kwa
ajili ya kufyeka majina 33 ya wagombea wanaoomba kuteuliwa kuwania kiti cha
urais na kubaki matano; alifanya kazi kubwa mbili katika siku ya jana, ikiwamo
kuzindua jengo jipya na la kisasa la CCM, maarufu kama Dodoma Convention Centre
na baadaye jioni kwenda kulivunja Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jumla ya makada 42 wa CCM walichukua fomu kwa ajili kuomba
ridhaa kwa chama hicho kiwateue kuwania urais.
Hata hivyo, kati hao 42, makada 38 ndiyo waliorejesha
fomu huku wanne `wakiingia mitini' na fomu hizo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment