POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu
watatu kwa tuhuma za kumuua mmiliki wa shule ya Mtakatifu Zion, Anna Mizingi
(48) kisha kumtumbukiza katika shimo la choo cha shule hiyo.
Katika taarifa yake
kwa vyombo vya habari, Kamishna wa Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema, Februari,
mwaka huu mtoa taarifa alifika katika kituo cha Polisi na kueleza kuwa Mwalimu
Anna aliondoka tangu Desemba 26, mwaka jana akiwa na mmoja wa watuhumiwa na hakuonekana
tena.
Kutokana na taarifa
hizo polisi walifungua jalada la uchunguzi, ambapo wakati wakiendelea na
uchunguzi zilipatikana taarifa zilizosaidia kukamatwa kwa watuhumiwa hao huko
Uchira Mawaleni, wilaya ya Moshi, Kilimanjaro.
Taarifa hiyo
ilieleza kuwa watuhumiwa hao walipokamatwa na kuhojiwa mmoja kati yao alikiri
na kutoa maelezo kuwa siku ya tukio aliondoka na Anna kuelekea katika shule ya
Mt Zion.
Kwamba walipofika
shuleni hapo walivamiwa na watu wapatao wanne na kuanza kupigwa lakini yeye
alifanikiwa kutoroka na kujificha katika uzio wa shule hiyo.
“Akiwa katika uzio
huo aliwaona watu hao wakiendelea kumpiga Mwalimu Anna na kisha kumtupa katika
shimo la choo. Baada ya kitendo hicho watu waliotenda uhalifu huo waliondoka na
gari la Mwalimu Anna na kutokomea kusikojulikana,” ilieleza taarifa hiyo.
Kamanda Kova
alisema, Juni 22, mwaka huu mabaki ya mwili wa marehemu yalipatikana eneo la
Ununio baada ya Polisi kwa kushirikiana na kikosi cha Zimamoto kubomoa shimo la
choo cha shule hiyo.
Aliwataja waliokamatwa
kuwa ni Daniel Mkilindi (25) mganga wa kienyeji mkazi wa Uchira, Said Omary
maarufu kama Said Ntimizi (34) mfanyabiashar ana mkazi wa Mbweni na Erick
Mziray (40) mfanyabiashara mkazi wa Kurasini.
“Watuhumiwa hawa
wanaendelea kuhojiwa ili kupata undani wa tukio hili, ikiwa ni pamoja na
kuwatafuta na kuwakamata watuhumiwa wengine wanaohusiana na tukio hili. Mara
baada ya uchunguzi kukamilika jalada la shauri hili litapelekwa kwa mwanasheria
wa serikali kwa hatua zake za kisheria,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment