Friday, July 17, 2015

Faida za bafu lenye bomba la mvua dhidi ya lile lenye sinki la kuogea


Karibu msomaji wangu kwenye makala ya leo ambapo tunaangalia faida za bafu lenye bomba la mvua dhidi ya lile lenye sinki la kuogea. Katika kuandaa makala hii nimefanya mahojiano na ndugu Rogers Mwenana ambaye ni muuzaji ma vifaa vya mabafu ya kisasa  kwenye duka moja katikati ya jiji la Dar es salaam.

Rogers anaanza kwa kutuambia kwamba
awali ya yote tunatakiwa kujua kuwa uchaguzi mzuri zaidi ni kuwa na bafu za aina zote hizi mbili ndani ya nyumba yaani kuwa na bafu la bomba la mvua na kuwa pia na lingine lenye sinki la kuogea. Tufuatane naye kujua ni kwa nini na pia kufahamu faida na hasara za kila aina.

Wakati wa kusanifu jengo, bafu zote yaani ya bomba la mvua na yenye sinki la kuogea ni nzuri na zinaweza kuongeza umaridadi bafuni. Ila jambo la kwanza kabisa la kuzingatia ni eneo. Faida ya kwanza ya kuwa na bomba la mvua ni matumizi mazuri ya nafasi hasa pale ambapo nafasi ya eneo la bafu ni ndogo. Eneo dogo tu la sakafu linatosha kuweka bafu la bomba la mvua wakati lile lenye sinki linahitaji eneo pana. Faida nyingine ya bafu la bomba la mvua ni kuwa bafu la aina hii linawezesha eneo lingine lote la bafu lililobakia kuwa kavu.

Kama kuna uwezekano wa kuwa na bafu za aina zote mbili ndani ya nyumba inasadia kuongeza thamani ya nyumba pale utakapotaka kuipangisha au kuiuza. Wanunuzi wa nyumba wengi wao wanaamini kuwa nyumba yenye bafu zenye sinki za kuogea zimeonekana kuwa na gharama ya juu zaidi ya nyumba zenye mabafu ya bomba la mvua tu. Ingawaje tofauti inaweza isiwe kubwa sana lakini nyumba yenye mchanganyiko wa bafu za bomba la mvua na sinki itauzika haraka zaidi kuliko yenye bomba za mvua tu.

Inashauriwa kuwa na walau bafu moja lenye sinki la kuogea ndani ya nyumba kwa ajili ya familia zile zenye watoto wadogo zinapendelea nyumba za namna hii kwasababu moja ya kuwa ni rahisi zaidi kuogeshea watoto kwenye bafu lenye sinki la kuogea kuliko kwenye bomba la mvua.

Chaguo kati ya bafu lenye bomba la mvua au sinki kwenye eneo la kuogea linaweza kugusa mambo mengi kuanzia kwenye kiasi cha nishati itakayotumika hadi usalama wa wana familia. Wakati bafu lenye bomba la mvua linawakilisha uharaka na urahisi wa matumizi, sinki la kuogea linawakilisha ufahari na kujiloweka kwenye maji., na tofauti ya hizi mbili inahusika zaidi na chaguo la wenye nyumba.

Kupanda na kutoka kwenye sinki la kuogea inaweza kuwa shida kwa wazee, walemavu na wale wote wenye shida ya kusogea kwa haraka . Kwa watu wa aina hii bafu la bomba la mvua linawafaa zaidi na ni salama zaidi ya sinki.

Bafu za bomba la mvua ni rahisi kwa utunzaji. Bafu likishakuwa limesimikwa, kitu kikubwa cha kufanya ili kulitunza ni usafi tu.
Faida nyingine ni kuwa hizi bafu za bomba za mvua ziko za aina nyingi. Kuna zile ambazo kuta zake ni kioo ambapo unaweza kununua zenye vioo vyenye maua ambapo zaidi ya kujisitiri pia linafanya bafu lionekane maridadi. Na endapo hutafanya hivyo basi unaweza kuamua kuweka pazia la bafuni ambapo nalo michoro yake inakuwa kama pambo pia kupendezesha bafu.

Bafu zenye bomba la mvua ni rahisi kusimika na zinakuja kwa bei mbalimbali. Ukilinganisha na sinki la kuogea bafu za bomba la mvua ni gharama nafuu zaidi, anasema Rogers.

Kwa upande wa matumizi ya maji, bafu lenye bomba la mvua lina gharama ndogo ukilinganisha na bafu lenye sinki la kuogea. Sinki la kuogea linabeba maji mengi sana ukilinganisha na maji kidogo tu unayoweza kufungualia bomba la mvua na kuoga na kumaliza. Kwenye bomba la mvua unaweza usitumie maji zaidi ya lita 10. Ila kama unataka kukaa bafuni ndani ya maji muda mrefu basi bafu la sinki ndilo linakufaa zaidi.

Fikiria zaidi unachokipenda wakati wa kuoga na uone ni bafu la aina gani kati ya hizi mbili litakidhi mahitaji yako na ya familia yako. Labda ni aina moja tu au ni mchanganyiko wa aina zote mbili kama ilivyoshauriwa hapa. Fanya uamuzi sahihi ambao hutaujutia baadaye.

Makala hii imeandaliwa na Vivi, kwa maoni au maswali tembelea www.vivimachange.blogspot.com

No comments:

Post a Comment